Tafuta

Maelfu ya watu wamerundikana huko Kanyaruchinya  DRC ambapo hali halisi ni ngumu kutokana na vikundi vya wanamgambo wa M23. Maelfu ya watu wamerundikana huko Kanyaruchinya DRC ambapo hali halisi ni ngumu kutokana na vikundi vya wanamgambo wa M23. 

Congo DRC:Caritas Australia imezindua wito wa dharura kwa watu Congo

Jamii za vijijini DRC zimekabiliwa na mashambulizi yanayoendelea kutokana na makundi yenye silaha huko Kivu Kaskazini,eneo linalopakana na Uganda na Rwanda.Tangu 20 Oktoba mzozo huo umeongezeka licha ya ahadi za kusitisha mapigano hayo.Kwa maana hiyo Caritas Australia imezindua wito wa dharura wa kusaidia jamii hiyo zinazoteseka bila hatia.

Na Angella Rwezaula; – Vatican.

Caritas Australia imetoa wito wa dharura kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mnamo tarehe  16 Disemba 2022 , katika kutoa jibu la kusaidia jamii nchini DRC ambayo imekuwa  ikikabiliwa na mzozo unaoongezeka na watu waliokimbia makazi yao tangu kundi la waasi la M23 kuteka eneo la mashariki mwa nchi hiyo zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Jamii za vijijini zimekabiliwa na mashambulizi yanayoendelea kutokana na makundi yenye silaha huko Kivu Kaskazini, eneo linalopakana na Uganda na Rwanda. Tangu  tarehe 20 Oktoba mzozo huo umeongezeka licha ya ahadi za kusitisha mapigano hayo. Inaaminika kuwa zaidi ya watu 300 waliuawa katika shambulizi dhidi ya kijiji kimoja mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini mapema mwezi Disemba.

Maelfu ya watu huko Kanyaruchinya wakikimbia wanamgambo wa silaha M23
Maelfu ya watu huko Kanyaruchinya wakikimbia wanamgambo wa silaha M23

Mapigano ya karibu mara kwa mara yamewalazimu watu 188,000 kutoka katika makazi yao. Takriban watu tisa kati ya kumi kwa sasa wanakaa katika makazi yenye watu wengi na maeneo yaliyoboreshwa, wengi hata kulala nje. “Wakati dunia ina shughuli nyingi na hakuna anayeangalia, kuna M23 wanaovamia vijiji na kuwalazimisha watu kukimbia kwa wingi kutoka kwa makazi yao. Lazima tuchukue hatua haraka, kwa sababu katika kambi moja kuna karibu watu 20,000 wamejazana katika sehemu moja, bila maji, usafi wa mazingira au hata makazi. Hiki ni kichocheo cha maafa,” alisema hayo Lulu Mitshabu, Mratibu wa Programu wa Caritas Australia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Aidha aliongeza kusema kuwa “Idadi kubwa ya watoto wamepoteza wazazi wao kwa migogoro au ugonjwa na sasa wako katika hatari kubwa bila msaada wowote”.

Watoto hawana ulinzi na usalama kwenye makambi ya ukimbizi

Watu hawa hawajui wapi na jinsi ya kupata huduma na kiukweli wanapata tatizo na mahitaji msingi. Katika moja ya kambi, watu sasa wanawakaribisha watoto ambao wamepoteza wazazi wao, ambayo pia inazua maswala mengi kuhusu usalama. Takriban kaya 18,000 zimepata hifadhi huko Kanyaruchinya, kaskazini mwa mji wa Goma. Kati ya watu 80,000 na 100,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wanakaa Kanyarucinya wakiwa na uwezo mdogo wa kupata misaada ya kibinadamu. Mashirika ya Caritas na WFP yamesambaza chakula cha dharura kwa kaya 14,000 katika kambi hiyo, lakini watu bado hawana huduma za usafi, maji safi ya kunywa, vifaa vya kulala, ulinzi kwa watoto na elimu.

Bila uingiliaji kati wa haraka wanawake na watoto wako hatarini

Kwa mujibu wa mratibu huyo Bi Mitshabu amebainisha kuwa: “Bila ya uingiliaji kati wa haraka watu wengi watasukumwa zaidi katika umaskini, na wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wanaachwa bila msaada. Watu wanahitaji haraka makao ya dharura, vifaa vya kulala, maji safi na chakula.” Mshirika wa Caritas Australia CAFOD yuko tayari kujibu jumuiya zinazohitaji usaidizi wa haraka na kutathmini mahitaji ya dharura zaidi. Kwa maana hiyo wanabainisha kwamba “Usaidizi wako wa ukarimu unaweza kusaidia kutoa usaidizi wa dharura ili kusaidia familia kupona na kujijenga upya kutokana na maafa. “Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya :caritas.org.au/donate/emergency-appeals/democratic-republic-of-congo/ au piga simu 1800 024 413 bila malipo ili kutoa usaidizi unaohitajika kwa ajili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuchangia Wito wetu wa Dharura ya Afrika”.

OKOA WATOTO DRC
17 December 2022, 15:14