Argentina:tusiondoe mtazamo wetu kwa watoto wanaoishi katika umaskini na kunyonywa
Na Angella Rwezaula; - Vatican News
“Tumwombe Yesu, aliyezaliwa hivi karibuni Bethlehemu, alinde maisha ya watoto wachanga, wale wanaoteseka kutokana na udhalimu wa vita na, kama Papa Francisko asemavyo, kwamba wasipoteze uwezo wao wa kutabasamu. Tusiwaondoe mtazamo kamwe wavulana na wasichana wanaoishi katika umaskini, wanaonyanyaswa kingono kazini. Ni maneno ya wito uliozinduliwa na Tume ya Maisha, Walei na Familia ya Baraza la Maaskofu nchini Argentina katika siku ambayo Mama Kanisa anawakumbuka Mashahidi Watakatifu wasio na Hatia inayoadhimishwa tarehe 28 Desemba. Katika siku kuu hii Kanisa linawakumbuka wale watoto wote ambao Herode, katika jaribio la kutaka kumuua Mtoto Yesu, aliamuru kuua kikatili, kama ilivyosimulia katika Injili kwamba: “Herode alipotambua kwamba wale mamajusi walikuwa wamemdhihaki, alikasirika sana na alituma kuwaua watoto wote waliokaa Bethlehemu na katika mipaka yake yote, waliokuwa na umri wa miaka miwili kwenda chini zaidi, sawasawa na muda aliopewa na mamajusi. Ndipo likatimia neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yeremia: “Kilio kilisikika huko Rama, kilio na maombolezo makubwa: Rakheli anawaomboleza watoto wake, na hataki kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” (Mt 2, 15-18).
Kuomba mbingu kwa ajili ya watoto wanaoteseka
Katika Ujumbe wa Baraza la Maaskofu nchini Argentina ambao umechapishwa tarehe 28 Desemba katika siku Kuu ya Watoto Mashahidi wasio na Hatia, unaweka wazi kwamba katika sherehe ya Noeli wamepyaishwa shauku kubwa ya kutunza maisha, kusaidia kuzaliwa na kukua. Kwa njia hiyo katika sikukuu hiyo ya Watakatifu Wasio na Hatia ni kurudi tena kuomba mbingu kwa ajili ya wavulana na wasichana wanaoteswa ambao zawadi ya uhai inaondolewa kwao kwa njia nyingi. Hatimaye, maandisho yao yanaomba maombezi ya Mashahidi Watakatifu wasio na hatia ili “walinde roho za wale wanaoishi katika mahali patakatifu pa umbu na wao waombee wote, ili kwa ujasiri wote waweze kutunza na kulinda kila maisha ambayo yapo ndani ya nchi yao.
Milioni16.5 za watoto Barazani Amerika Kusini wanahitaji msaada kwa 2023
Ikukumbukwe kwamba katika nchi za Amerika ya Kusini, makumi ya mamilioni ya watoto na vijana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaishi katika umaskini. Hata nchi ambazo zimeona maboresho ya hali zao za maisha haziwezi kuwashirikisha watoto wadogo katika mchakato huo, ambao kwa kiasi kikubwa wananyimwa haki zao za kimsingi. Kutokana na ongezeko la mtiririko wa uhamiaji, vurugu na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya hali ya tabianchi, UNICEFinakadiria kuwa watoto na vijana milioni 16.5 katika bara la Amerika ya Kusini watahitaji msaada wa kibinadamu katika mwaka ujao 2023.
Unicef:Kiwango cha mauaji ya watoto ni chanzo cha vifo kwa vijana miaka 10-19
Ripoti ya kikanda ya UNICEF ya mwezi Novemba 2022 pia iligundua kuwa watoto katika bara la Amerika ya Kusini na visiwa vyake Carribien wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili nyumbani, shuleni na mitaani kuanzia umri wa mwaka mmoja na kuendelea. Takriban watoto 2 kati ya 3 walio na umri wa miaka 1-14 katika eneo hilo hupitia adhabu ya nyumbani. Mbali na adhabu za kimwili na mashambulizi ya kisaikolojia katika utoto, unyanyasaji wa kijinsia na mauaji huathiri mamilioni ya watoto na vijana pia. Kiwango cha mauaji ya kikanda cha watoto na vijana (12.6 kwa 100,000) ni mara nne zaidi ya wastani wa kimataifa (3 kwa 100,000). Na mauaji ndio chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 10-19, Unicef inabainisha.
Hii ni siku ya kutangaza maisha na kuwa na mshikamano kwa wanaoteseka
Katika sikukuu hii ya Mashahidi ya watoto wasio na hatia, ambayo uhadhimishwa kila tarehe 28 Desemba, Kanisa nchini Colombia pia linachukua tahadhari hasa kwa mfano huo wa Watakatifu wasio na hatia kutoa heshima kwa ajili ya maisha na kutoa wito wa kuheshimu hadhi ya kila mtu. Padre John Jaime Ramírez Feria, mjumbe wa mawasiliano wa Jimbo kuu la Ibagué, ametoa tafakari inayojikita katika usomaji wa kifungu cha Injili kutoka Mtakatifu Mathayo: “Injili inabainisha wazi kuhusu hadhi ya kila mtu, ambapo leo hii tunashuhudia vurugu nyingi, ukatili mwingi, tangu kutungwa mimba, kutoheshimu maisha, kwa waathrika wengi wa utoaji mimba, lakini pia kwa wengi wanaoteseka kutokana na jeuri, wanawake wengine kama Rachel, wanaoomboleza vifo vyo vya watoto wao. Kwa hiyo hii ni siku ya kutangaza maisha na kuamsha mshikamano na wale wote wanaoteseka.