AMECEA:Uzinduzi wa Jubilei ya miaka 25 ya Seminari ya Bakanja
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Katika uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya shaba au ya miaka 25 ya Seminari ya Mwenyeheri Bakanja AMECEA (BBAC) iliyopo Jimbo Kuu la Nairobi nchini Kenya, Balozi wa Vatican nchini Kenya aliwahimiza wanaseminari kutoka nchi mbalimbali ndani ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki( AMECEA) na kwingineko kuthamini utofauti wa kiutamaduni wa seminari na wakati huo huo kuwa mifano ya kuigwa katika njia yao ya kuishi. Askofu Mkuu Hubertus van Megen alisema hayo kwa waamini, Jumamosi tarehe 17 Desemba 2022 wakati wa mahubiri yake alipokuwa akiongoza maadhimisho ya Ekaristi ya uzinduzi wa maandalizi ya mwaka mmoja kuelekea miaka 25 tangu kuanza kutoa huduma ya seminari hiyo itakayoadhimishwa mnamo tarehe 16 Desemba 2023.
Kwa njia hiyo Balozi wa Vatican nchini Kenya alibainisha kuwa Bakanja kuwa seminari ya kimataifa ina maana kwamba inawaunda na kuwafunda kuelewa tamaduni tofauti na jinsi wanavyohitaji kuheshimu njia ya maisha ya watu wengine na jinsi ya kuwa waangalifu katika miitikio yao wenyewe mbele ya wengine wanaotoka tamaduni zingine. Kipengele cha kimataifa cha seminari kwa namna fulani kinaunda pia mustakabali wa Kanisa la kiulimwengu. Katika ujumbe wake, Askofu Mkuu Van Megen hata hivyo aliweka wazi kwamba masharika mengi yana matatizo yanayotokana na ukosefu wa utambulisho wa kiroho, ukosefu wa utambulisho utawa na ukosefu wa nidhamu, hivyo aliwahimiza waseminari wa Bakanja kuwa waaminifu kwa wito wao, kwa utawala wa maisha na utawala bora kwa katiba na sheria za makutaniko yao mbalimbali.
Zaidi ya hayo Askofu Mkuu Van Megen alisema, “Wafundaji na wakuu lazima waishi maisha ya kuigwa mfano” na zaidi alitoa wito kwa wote ili kuishi maisha ya kujitolea na ya uwazi, maisha ambayo wanamwachia Kristo nafasi ya kwanza yaani kipaumbele cha Maisha yao. Aidha Askofu Mkuu van Megen ambaye pia ni mwakilisha wa Vatican nchini Sudan Kusini alisisitiza hitaji la kuwa na Kristo na ambaye aigwe na kuwa kitovu cha maisha ya k ila siku Katika mahubiri yake wakati wa Adhimisho la Ekaristi, Askofu Mkuu Van Megen alibainisha kuwa kuadhimisha miaka 25 kunamaanisha kwamba Seminari ina mambo mengi ya kutazama nyuma, mengi ya kuombea na mengi ya kutazamia hasa katika kumshukuru Mungu kwa zawadi nyingi zilizotolewa na ambazo zinapokelewa. Baadaye alizindua na kubariki vitu mbalimbali vitakavyotumiwa wakati wa matayarisho ya mwaka mmoja ikiwa ni pamoja na sala ya Jubilei, kauli mbiu, nembo, na wanakamati wa maandalizi walipewa jukumu la kuongoza shughuli za Jubilei ijayo. Mwaka wa Jubilei ya Fedha unaongozwa na kauli mbiu: “Tutazame miaka 25 iliyopita kwa shukrani, kuishi sasa kwa shauku, kutazama siku zijazo kwa matumaini”.