Tafuta

2022.11.03 Uzinduzi wa Kimataifa wa tamko la UISG  la Watawa kwa ajili ya Mazingira:Kufungamanisha sauti za walio pembezoni utakaopelekwa kwenye COP27 2022.11.03 Uzinduzi wa Kimataifa wa tamko la UISG la Watawa kwa ajili ya Mazingira:Kufungamanisha sauti za walio pembezoni utakaopelekwa kwenye COP27 

UISG kuwa sauti ya kinabii kwa wanyonge&inapeleka kilio cha maskini katika COP27

Umoja wa Mama wakuu wa Mashirika Kimataifa wamezindua taarifa iliyokusudiwa kutafakari na kufafanua majibu ya watawa katoliki katika changamoto za mazingira za wakati wetu.Tamko lao litapelekwa kwenye Mkutano wa COP27 unaonza tarehe 6/18 Novemba huko Cairo nchini Misri.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Alhamisi  tarehe 3 Novemba 2022 alasiri siku chache tu kabla ya kuanza kwa Mkutano kuhusu Tabianchi COP27 nchini Misri, Umoja wa Mama Wakuu wa Mashitika UISG, Kimataifa walizindua tamko lao kwa niaba ya Masista wanaharakati wa Mazingira ili Kuunganisha Sauti kutoka Pembezoni kama kauli mbiu. Hafla hiyo ilifanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mama wakuu [UISG], jijini  Roma, na watu walihudhuria kwa sehemu mbili,  ya ana kwa ana na kupitia mtandaoni. Sr. Pat Murray alitoa utangulizi wa tukio hilo, akitangaza kwamba wanapokutana na wale walio pembezoni mwa maisha, wanawabadilisha. Maisha ya nadhiri za kitawa zinawaalika kuwa manabii,  na kuwa sauti kwa wale wanaopuuzwa au kutengwa. Moja ya maeneo ambayo watawa wanatafuta kutetea kwa niaba ya wale ambao hawako kwenye meza ya mazungumzo ni katika mabadiliko ya tabianchi.

Uzoefu wa kimataifa wa utetezi wa mazingira

Taarifa ambayo  Umoja wa Mama wakuu wa mashirika ya kitawa kimataifa [UISG] wametoa siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano kuhusu Tabianchi COP27 nchini Misri, utakaoanza tarehe 6 hadi 18 Novemba, inajumuisha ari ya ushirikiano wanayotaka kukuza, wakitegemea ushirikiano kati ya ofisi za  Umoja wao UISG, washirika na wafadhili, lifafanua Sr. Pat Murray. Zaidi ya hayo, kiini cha kauli mbiu yao kinatokana na uzoefu wa kimataifa wa utetezi ambao umeungana kwenye kampeni ya mazingira ya  Umoja huo UISG yitwayo Sowing Hope for the Planet, yaani Kupanda Matumaini katika Sayari iliyozinduliwa  mnamo mwaka 2018. Kampeni hiyo imehamasisha  na kushiriki wingi wa mipango na mbinu bora zilizoanzishwa na Masista na washirika yao  kwa kujibu Waraka wa Papa Francisko wa  Laudato si' hukusu  utunzaji Bora wa Mazingira nyumba yetu ya Pamoja.

Inahitajika mikakati ya muda mfupi na mrefu kwa vizazi vyote

Aliyejiunga na uzinduzi huo alikuwa Francesca di Giovanni, Naibu Katibu wa Vatican katika Masuala ya Kimataifa katika Kitengo cha Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Kwa upande wake alikubali kwamba wanawake wengi watawa wanafanya kazi moja kwa moja na watu walioathiriwa na kujaribu kuleta mabadiliko kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi kiukweli alikiri  yanaathiri isivyo sawa wale walio pembezoni  na  yakihitaji mikakati ya muda mfupi na mrefu na ya vizazi vya sasa na vijavyo. Watawa wanaweza kuitikia kilio cha dunia na kilio cha maskini, na pia kukuza mtindo wa maisha unaopatana na asili.

Watu wengi wa asilia wanafahamu ikolojia

Naye Bi Chiara Porro, Balozi wa Australia anayewakilisha nchi yake jijini Vatican pia  alikuwepo, akiwakilisha eneo linalokabiliwa na athari nyingi za mabadiliko ya tabianchi. Sauti za wale walio pembezoni zinaweza kusikika kupitia vikundi, kama vile vya Umoja wa Mama wakuu wa mashirika Kimataifa UISG, vinavyowatetea katika kumbi za mikutano ya kidunia, kama vile ya COP27 ijayo nchini Misri. Bi Porro aliweka bayana jinsi mtawa , Sr Adele Howard, wa shirika la Huruma  nchini Australia, ambavyo amekuwa akikusanya takwimu  kuhusu maoni ya watawa katika muktadha wa sayari inayoshikiliwa na watu wa kiasili. Kwa hivyo ameweza kuunganisha kile anachoita ufahamu wa kiikolojia ambao watu wengi wa asilia hushikilia. Kazi yake,inaonesha wazi kwamba kupotea kwa ardhi yetu ni kupoteza maana ya sisi ni nani, alisistiza Balozi huyo.

Mikutano wa COP27 Misri na COP15 Canada

Akiwasilisha Taarifa yenyewe ni Sr Sheila Kinsey, mratibu wa  Kupanda Matumaini ya Sayari Sowing Hope for the Planet, ambaye alianza kwa kueleza jinsi watawa wanavyoshirikishwa katika mipango mbalimbali ya kiikolojia. Taarifa ya sasa, alifafanua, inalenga kutafakari na kufafanua majibu ya Masista wakatoliki kwa ajili ya changamoto za mazingira za wakati wetu, lakini pia inashughulikia udharura wa wakati wa sasa, na kutambua COP27, juu ya mabadiliko ya tabianchi  na COP15 itakayofanyika mwezi Desemba ijayo nchini Canada  kuhusu  bioanuwai kama umuhimu wa fursa za kugeuza wimbi la uharibifu linaloharibu Dunia yetu. Kabla ya kusoma maandishi ya taarifa hiyo, Sr Sheila Mratibu wa Kapendi ya Kupanda Matumaini kwa ajili ya Sayari alizindua wito kwa wengine kuungana  mkono na watawa katika kutafuta suluhisho  ili kuhakikisha mustakabali ulio salama na mzuri kwa watu wote na kwa sayari yetu.

Maskini wanaathiriwa na mzozo wa kiikolojia

Pia katika hafla hiyo kulikuwa na shuhuda za wanawake mbalimbali watawa. Kwa mfano Sr Nathalie Kangaji, mwanasheria wa Mtakatifu Augustino wa Shirika la  Notre-Dame, kutoka DCR alishirikisha  jinsi anavyosaidia jumuiya mahalia  kuunda na kuunganisha kamati shirikishi za serikali, ili waweze kuunda vikundi vya shinikizo kwa  ajili ya ulinzi wa mazingira na utawala bora. Naye  Sr  Jyotisha Kannamkal wa Shirika la Mama Yetu [Notre Dame] alibainisha kwamba kujibu kilio cha dunia na kilio cha maskini kama mwelekeo muhimu wa kujitoa kwake  katika kupyaisha  uso wa dunia. Alishirikisha aidha  jinsi maskini wanavyoathiriwa na mzozo wa kiikolojia na kusumbulia. Sauti yake ya ndani, kwa maana hiyo  inamwihimiza kujitoa kikamilifu katika utetezi wa ikolojia fungamani. Wanachama wa UISG wanapanga kwa njia hiyo kutuma ujumbe kwenye Mkutano wa  COP27. Atakaye wawakilisha ni Sr. Jean Quin wa Shirika la Mabinti wa  Hekima. Atakwenda huko kwa hakika kwenye mkutano kama hija na mahali pa changamoto alielezea.  Kwa mujibu wake alibanisha kwamba sauti za kinabii zitasikika. Baada ya mikutano mingi ya COP, Sr.  Jean alibainisha kuwa ni wakati wa utekelezaji. Kwa kuongezea, kuondoa deni kutoka  mataifa yaliyoelemewa na madeni pia kutawawezesha kuanza kuwekeza katika sera za mabadiliko ya tabianchi.

UISG NI SAUTI ZA KILIO CHA MASKINI
04 November 2022, 14:35