Tafuta

Kiturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Maandiko Matakatifu tunayoyapokea katika dominika hii nayo yanaelekeza mawazo yetu katika mambo ya mwisho: Kiturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Maandiko Matakatifu tunayoyapokea katika dominika hii nayo yanaelekeza mawazo yetu katika mambo ya mwisho:   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 33 Mwaka C wa Kanisa: Siku ya Wokovu: Saburi, Matumaini na Furaha

Siku ya VI ya Maskini Duniani: Umaskini wa Kristo uwawajibishe waamini kushirikiana na kushikamana katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha tunu msingi zinazosimikwa katika mshikamano, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Siku ya Bwana ni kielelezo cha utimilifu wa kazi ya uumbaji na ukombozi wa mwanadamu, siku ya furaha.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ni dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa, dominika inayotusogeza karibu kabisa na mwisho wa mwaka wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yanaongozwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Baba Mtakatifu anachambua jinsi UVIKO-19 ulivyo sababisha ongezeko la maskini duniani; vita inavyoendelea kuwatumbukiza watu katika baa la umaskini na kwamba, umaskini wa Kristo uwawajibishe waamini kushirikiana na kushikamana katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha tunu msingi zinazosimikwa katika mshikamano, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Maandiko Matakatifu tunayoyapokea katika dominika hii nayo yanaelekeza mawazo yetu katika mambo ya mwisho: yanatuandaa kuijongea Siku ya Bwana, siku ambayo kazi nzima ya uumbaji na ukombozi wa mwanadamu itafikia ukamilifu wake.

Siku ya Bwana ni Siku ya Hukumu, Saburi na Matumaini na Furaha
Siku ya Bwana ni Siku ya Hukumu, Saburi na Matumaini na Furaha

UFAFANUZI WA MASOMO: Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii Malaki (Mal. 4:1-2),  Nabii ambaye kwa namna ya pekee ameikita kazi yake ya unabii kutangaza siku ya Bwana. Katika mafundisho ya manabii, Siku ya Bwana ilimaanisha siku ya hukumu. Taifa la Mungu Israeli lilitambua kuwa ipo siku inakuja ambapo taifa zima na kila mmoja ataalikwa kutoa hesabu ya maisha yake. Kama kawaida ya mwanadamu, kujisahau huwa kupo. Katika somo la leo, nabii anawatahadharisha Waisraeli kuwa siku hiyo ya Bwana ipo, inakuja na itakuwa ni siku ya hukumu.. Itakuwa ni hukumu kwa wenye kiburi na wote watendao maovu. Kwa wale wanaomcha Bwana, siku hiyo haitakuwa kwao siku ya hukumu bali itakuwa siku ya mwangaza wa haki, itakuwa siku ya kupokea tuzo. Katika somo hili tunaona mojawapo ya sifa kuu ya unabii: kutangaza hukumu au adhabu na hapo hapo kutoa matumaini kwa watu. Hakuna unabii wa kimungu unaotangaza mabaya tu: hukumu, laana, adhabu, maangamizi na uovu tu wa watu. Hali kadhalika hakuna unabii wa kimungu unaotangaza neema tu: uponyaji, utajiri, fanaka na kadhalika. Nabii huwaonesha watu msingi wa maisha ambao ni Mungu mwenyewe. Huwaonya watu pale wanapomwacha na huwaalika kumrudia ili waepuke kuyapoteza maisha yao.

Siku ya Bwana ni siku ya matumaini yanayosimikwa katika ushuhuda wa imani
Siku ya Bwana ni siku ya matumaini yanayosimikwa katika ushuhuda wa imani

Katika somo la pili (2 Thes 3:7- 12) tunayasikia maneno ya Mtume Paulo, “ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula." Mazingira ya kauli hii ni katika jamii ambapo waliibuka watu wakaanza kufundisha kuwa Siku ya Bwana ipo karibu kufika. Waliendelea kuwaaminisha watu kuwa hakuna haja ya kujisumbua na mipango wala mambo ya muda mrefu kwa kuwa siku ya mwisho imefika. Hawa hawakufanya tena kazi na walianza kuishi maisha kama walivyotaka wao. Mtume Paulo alikwisha fundisha kuhusu nini maana ya Siku ya Bwana. Katika somo la leo anaukemea mwenendo wa kuyatumia vibaya Maandiko Matakatifu au mafundisho ya kimungu kana kwamba ni mafundisho ambayo hayana mantiki na hayaendani na hali halisi. Anawakumbusha watesalonike umuhimu wa kuishi kwa kufuata utaratibu na kwa kushika nidhamu ya kazi na ya maisha ya kawaida kwa ujumla.  Katika upande mwingine, somo hili linaendeleza fundisho msingi la Paulo kwa watesalonike: kutokukubali kuyumbishwa katika imani na katika mwenendo mwema wa maisha. Na myumbo huu unaweza kutokea hata chini ya mwamvuli wa mafundisho ya imani. Kuhusu jambo hili Mtume Yohane alionya “msiziamini kila roho, zichunguzeni” (rej. 1 Yoh 4:1).

Waamini wawe  makini wasidanganywe na mafundisho potofu
Waamini wawe makini wasidanganywe na mafundisho potofu

Somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Luka (Lk. 21:5-19). Ni somo linalotoa hotuba ndefu ya Yesu inayojikita katika mambo ya siku za mwisho. Kwa Wayahudi kulikuwa na matumaini kuwa siku ya mwisho inapokaribia kutakuwa na alama na yataanza kutokea mambo yasiyo ya kawaida.  Hivyo kila aliyejitokeza akionesha uwezo wa kusoma na kutafsiri alama alionekana kama ndiye mwenye ufunguo wa kuwasaidia watu kuijongea siku hiyo wakiwa wamejiaandaa. Sasa walipomsikia Yesu anazungumza juu ya mwisho wa hekalu, kwamba siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe, basi wakajua ni yeye anayepaswa kuwapa majibu ya maswali yao. Hapo hapo wakamuuliza “mwalimu mambo haya yatakuwa lini? nayo ni nini ishara ya kuwa siku hiyo ipo karibu?” Kwa Yesu, kujua siku na alama ya matukio siyo namna ya kuingojea siku ya Bwana. Ndiyo maana mara moja anawaambia “angalieni msije mkadanganyika”. Namna ya kuingojea siku ya Bwana ni kwa saburi na matumaini. Matukio ya kuogopesha, ujio wa manabii wa uongo, ishara za kutisha, mateso na vifo vya mashahidi wa Kristo na mambo mengine kama hayo vinapaswa kupokelewa kama mwaliko wa kudumu wa kuwa na saburi na matumaini katika kuuishi ukristo na ufuasi wa imani. Anasema Yesu mwenyewe kuwa mambo hayo hayana budi kutokea kwanza lakini ule mwisho hauji upesi. Hayana budi kutokea kwa sababu ni sehemu ya njia ya ufuasi na ushuhuda wa imani. Siku ya mwisho ni siku ya wokovu na siku ya kuiponya nafsi iliyoishi kwa saburi na uvumilivu. “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.”

Siku ya Bwana: Ushuhuda wa imani katika matendo
Siku ya Bwana: Ushuhuda wa imani katika matendo

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tumeeleza mwanzoni mwa tafakari hii kuwa tunaukaribia mwisho wa mwaka wa kiliturujia wa kanisa na Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanazungumzia habari za mambo ya mwisho – ujio wa siku ya Bwana na tafakari nzima ya mambo ya mwisho. Lugha hii ya mambo ya siku za mwisho ni lugha inayoendana kabisa na fikra za kawaida za binadamu kuyapima mambo katika mizani ya “mwanzo na mwisho”. Na fikra hii inajieleza vizuri katika msemo wetu uliozoeleka: “kila chenye mwanzo, kina mwisho”. Na hii wakati mwingi huleta huzuni na masikitiko hasa pale tunapoona kuwa jambo au hali fulani njema ambayo mtu anaifurahia itafikia mwisho wake na haitakuwapo tena. Hisia zinakuwa ngumu zaidi hasa tunapofikiria juu ya maisha yenyewe. Lakini mtazamo au fikra ya kiimani ambayo hasa ni fikra ya kimungu haiko hivyo. Fikra ya kimungu haipo katika mizani ya “mwanzo na mwisho”.  Badala ya “mwisho” wa mambo, yanyewe imejikita katika “ukamilifu” au utimilifu wake. Katika fikra hii ya kimungu mambo hayaelekei kufikia mwisho bali kufikia ukamilifu.

Siku ya mwisho ni utimilifu wa kazi ya uumbaji na ukombozi
Siku ya mwisho ni utimilifu wa kazi ya uumbaji na ukombozi

Ujio wenyewe wa Kristo ni ujio uliokuja kukamilisha ufunuo wa Mungu ulioanza na uumbaji na kufunga na mwanadamu Agano Jipya na la milele. Amekuja kutimiliza. Mwanzo kabisa wa mahubiri yake alisema “leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk. 4:21), kuhusu torati anasema “sikuja kutangua”..kuihitimisha “bali kutimiliza”(Mt. 5:17) na hata alipokuwa anakata roho pale msalabani neno lake lilikuwa “yametimia” (Yn 19:30). Ni katika mwanga huu imani yetu inatualika tuingojee siku ya Bwana kama ni siku inayokuja kuukamilisha ulimwengu na kutukamilisha sisi wenyewe. Na ukamilifu huu ni kufananishwa naye na kumwona Yeye kwa jinsi alivyo. Tukiwa na imani na matumaini haya, tafakari ya siku ya Bwana na kuhusu mambo ya siku za mwisho haiwezi kuwa kwetu sababu ya hofu, vitisho wala kuvunjika moyo bali mwaliko hai daima wa kujiandaa kuufikia ukamilifu wa uumbaji na ukombozi wetu kwa njia ya Kristo.

Liturujia D33
11 November 2022, 16:05