Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 32 ya Mwaka C: Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele ni ushiriki wa heri za mbinguni. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 32 ya Mwaka C: Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele ni ushiriki wa heri za mbinguni. 

Tafakari Dominika 32 ya Mwaka C wa Kanisa: Ufufuko Wa Wafu: Ushiriki wa Heri Mbinguni

Tunakiri: “nangojea na ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo. Amina.” Kwa kifo mwili na roho ya mtu hutengana. Mwili huoza lakini roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Ufufuko ni pale ambapo Mungu kwa uwezo wake atairudishia kwa hakika miili yetu uzima usioharibika kwa kuiunganisha na roho zetu kwa nguvu ya ufufuko

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Dominika ya 32 ya mwaka C wa Kanisa inatuletea fundisho kuhusu tumaini la ufufuko na uzima wa milele baada ya maisha ya hapa duniani. Ni masomo yanayotuonesha hadhi ya pekee ambayo Mungu amempa mwanadamu kushiriki naye heri ya milele mbinguni. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya masomo ya dominika hii na katika kulipokea Neno la Mungu, Neno ambalo ni taa na mwanga wa kuyaongoza maisha yetu kuifikia heri aliyotuandalia Mwenyezi Mungu. UFAFANUZI WA MASOMO:  Somo la kwanza tunalisikia kutoka katika Kitabu cha Kwanza cha Wamakabayo (2Mak. 7:1-2, 9-11). Linaeleza habari ya ndugu saba waliokubali kufa wakitetea imani na tamaduni zao njema walizorithi toka kwa wazee wao. Ndugu hawa saba wanateswa vikali na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe. Suala hapa halikuwa nyama ya nguruwe kama nguruwe bali lilibeba maana pana zaidi ya kulazimishwa kufanya vitu ambacho kwa mapokeo yao kama taifa teule la Mungu, linaloishi chini ya Agano na Torati ya Musa, hawakupaswa kufanya. Wote saba wanakataa na wanakuwa tayari kukikabili kifo. Pamoja na uaminifu kwa imani na mapokeo  yao, ndugu hawa pia wanaeleza msukumo wa uaminifu wao huo kuwa ni imani ya kuwa kuna na maisha baada ya kifo.

Maisha na uzima wa milele ni kushiriki heri za mbinguni
Maisha na uzima wa milele ni kushiriki heri za mbinguni

Tunasikia yule kijana mkubwa anamwambia mtesi wake “unatuua katika maisha ya sasa lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake hata tupate uzima wa milele.” Somo hili ni kichocheo kwetu kuwa thabiti katika imani: kushika imani na mapokeo yake yote kiaminifu dhidi ya vitisho vya nguvu au ushawishi laini wa kufuata mkumbo bila kujali madhara yake kwa imani na mapokeo yetu. Zaidi ya hapo, somo hili ni mojawapo ya vifungu katika Agano la Kale vinavyozungumzia tumaini la ufufuko na maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Katika somo la pili (2 Thes 2:16- 3:5), Paulo anarejea bado mkanyanyiko na upotoshaji uliyoikumba jumuiya ya Thesalonike kuhusu mwisho wa dunia, kuhusu siku ya kurudi Bwana imekaribia. Paulo katika somo hili anahitimisha mafundisho na ufafanuzi wake kuhusu mkangayiko huo. Na ahahitimisha kwa kuwaasa watesalonike wasifadhaishwe na uvumi huo na wala wasivunjike moyo. Anawakabidhi kwa Kristo, faraja ya milele na tumaini jema ili awafariji na kuwaimarisha katika kuendelea na maisha yao. Anawaomba pia waombeane. Waombeane ili Mungu awalinde na yule mwovu kwa sababu hakuna mwingine anayeweza kuleta mkanganyiko na mvurugano katika jumuiya isipokuwa yule mwovu. Anawaomba wadumu kuombeana ili Mungu awakinge na mwovu na awaongoze mioyo ili walipate pendo lake na saburi ya Kristo.

Waamini wanaalikwa kujiandaa vyema ili kushiriki karamu ya heri ya mbinguni
Waamini wanaalikwa kujiandaa vyema ili kushiriki karamu ya heri ya mbinguni

Somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Luka Injili (Lk 20:27-38). Ni somo linalotoa fundisho juu ya ufufuo wa wafu na maisha baada ya kifo. Injili inaleta fundisho hili kupitia majibizano kati ya Yesu na Masadukayo. Katika uyahudi kulikuwa  na vikundi mbalimbali vyenye mitazamo tofauti katika masuala ya kidini. Wasadukayo walikuwa ni mojawapo ya vikundi hivyo. Hawa ni wale ambao hawakuamini kuhusu ufufuko wa wafu, kuhusu malaika n.k. Kitovu cha dini, kwao kilikuwa ni ibada za hekalu na ni humo tu waliamini Mungu yumo na wala si mahala pengine. Hawa bila shaka walikwishamsikia Yesu akifundisha juu ya ufufuko na maisha baada ya kifo. Kuhusu maisha baada ya kifo, nadharia iliyokuwapo kabla ya Kristo ni kuwa mtu akifa aliendelea kuishi katika uzao wake. Hata hivyo nadharia hii haikuwa juu ya ufufuko bali kama kumbukumbu tu ya maisha ya mtu. Wanamfuata Yesu na kumuuliza huo ufufuko anaoufundisha utakuwaje na mtu ataendeleaje kuishi iwapo hatakuwa hata ameacha uzao duniani? Yesu anawafundisha akiwaonesha kuwa maisha baada ya kifo sio mwendelezo wa vipengele vya maisha ya hapa duniani na wala hayapimwi kwa vigezo vya maisha ya hapa duniani. Anasema “wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa lakini wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule na kule kufufuliwa katika wafu, hawaoi wala hawaolewi”. Hayo ni maisha ya utukufu na ndiyo maana anasema watakuwa sawasawa na malaika. Hali kadhalika Yesu anawaonesha kuwa Mungu mwenyewe alikwisha jifunua kuwa ni Mungu wa walio hai pale anapojitambulisha kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, wa Isaka na wa Yakobo kwa maana wote wamwaminio kwake huishi, wako hai daima.

Kanisa linasadiki katika ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele.
Kanisa linasadiki katika ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Masomo ya leo yanatualika tutafakari imani ya Kanisa juu ya ufufuko na uzima wa milele. Tunaposali kanuni ya Imani huwa tunaihitimisha kwa kukiri “nangojea na ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo. Amina.” Kwa kifo mwili na roho ya mtu hutengana. Mwili huoza lakini roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Ufufuko ni pale ambapo Mungu kwa uwezo wake mkuu atairudishia kwa hakika miili yetu uzima usioharibika kwa kuiunganisha na roho zetu kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu (rej. KKK. 997). Namna ya ufufuko itakuwa ni namna ile ile ya ufufuko wa Kristo. Alifufuka na mwili wake lakini hakuurudia uzima wa kidunia. Kumbe wote watafufuka pamoja na miili yao waliyo nayo sasa lakini mwili huo utageuzwa katika mwili wa utukufu, mwili wa kiroho (rej. KKK. 999). Fundisho kuhusu ufufuko na uzima wa milele pamoja na mafundisho kuhusu mambo ya mwisho kwa kiasi fulani huleta hisia tofauti kwa watu na wapo baadhi wanaolipokea kwa hofu. Tofauti na kutia hofu, fundisho hili linajaza matumaini. Tumani kuwa maisha ya mwanadamu hayapotei baada ya kukamilika maisha ya hapa duniani, mwishowe ni uwinguni kuliko na maisha yasiyo na mwisho. Katika nafasi nyingine, ni mwaliko  wa kujua kuyachukulia vema maisha yetu hapa duniani kwani pamoja na kuishi kikamilifu kadiri ya wito wa kila mmoja wetu, maisha ya duniani yanapaswa kuonekana kama hatua ya kuyaandaa maisha yajayo yasiyo na mwisho pamoja na Mungu Baba. Ya hapa duniani yana mwisho na mwisho wake ni kuingia katika yale yasiyo na mwisho.

Liturujia D32
05 November 2022, 07:57