Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 37 Vijana Duniani yamenogeshwa na kauli mbiu: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39) Maadhimisho ya Siku ya 37 Vijana Duniani yamenogeshwa na kauli mbiu: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39)  

Kongamano la VIWAWA Jimbo Kuu la Mwanza: Changamoto za Vijana "Bongo Country"

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, anasema makongamano na semina za vijana ni fursa ambazo vijana hupata nafasi ya kushirikishana na kujijenga zaidi kiroho, kiutu na kijamii. Hizi ni fursa ambazo vijana wanapaswa kuzichangamkia. Utume wa vijana katika ngazi mbalimbali unapaswa kuvaliwa njuga, ili kuwasaidia vijana kutekeleza nyajibu zao.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama – Pozzuoli, Napoli, Italia.

Maadhimisho ya Siku ya 37 Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yamenogeshwa na kauli mbiu: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39) na siku hii imeadhimishwa tarehe 20 Novemba 2022 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anawaalika vijana kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kuinuka kwa haraka na kuanza kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao; kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika furaha ya Fumbo la Ufufuko, ili kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwaongoza katika huduma ya upendo, kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na neema ya Roho Mtakatifu iliyoko ndani mwao, wakiwa tayari kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao, kielelezo msingi cha imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume: “Dilecti Amici,” yaani “Marafiki Wapendwa” wa tarehe 31 Machi 1985 ambayo aliwaandikia Vijana wa Ulimwengu kuelekea Maadhimisho ya “Mwaka wa Kimataifa wa Vijana” uliotangazwa na Umoja wa Mataifa, anasema “ujana ni hazina mahususi” na kukazia kuwa ni ujana ni “hazina ya kugundua na wakati huo huo ya kuandaa, kuchagua, kutabiri na kufanya maamuzi ya kwanza ya kibinafsi, maamuzi ambayo yatakuwa muhimu kwa siku zijazo katika mwelekeo binafsi wa uwepo wa mwanadamu” (Dilecti Amici, namba 3).

Vijana wajibidiishe kushiriki katika semina na makongamano mbalimbali
Vijana wajibidiishe kushiriki katika semina na makongamano mbalimbali

Kwa upande wake, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, anakaza kusema makongamano na semina za vijana ni fursa ambazo vijana hupata nafasi ya kushirikishana na kujijenga zaidi kiroho, kiutu na kijamii. Hizi ni fursa ambazo vijana wanapaswa kuzichangamkia. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa mwaka 2021 alitangaza kuwa sasa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yatafanyika katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu ikiwa na nia ya kumwalika Kristo Yesu kutawala na kuongoza maisha ya vijana. Hapo awali maadhimisho haya yalikuwa yakifanyika Dominika ya Matawi. Ni katika kuitikia mwaliko huu wa Baba Mtakatifu Francisko Jimbo Kuu Katoliki Mwanza limewakutanisha vijana kutoka parokia mbalimbali za Jimbo katika Kongamano la Vijana Kijimbo lililoanza Ijumaa 18 Novemba 2022 na kuhitimishwa Jumapili Novemba 20 kwa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu katika Parokia ya Kristo Mfalme Kiseke, misa ambayo imeongozwa na Askofu mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu la Mwanza. Mara baada ya kuwasili siku ya Ijumaa jioni VIWAWA walipata fursa ya kupatiwa semina juu ya Mahusino na Ndoa, moja ya changamoto zinazowakabili vijana katika zama za leo. Siku ya Jumamosi Novemba 19 vijana hawa walikuwa na mazungumzo na Askofu Mkuu Renatus Nkwande ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zake za kuyafikia makundi yote yanayoshiriki utume wa Kanisa.

Vijana wanahamasishwa kuwa ni wajumbe na vyombo vya furaha ya Injili
Vijana wanahamasishwa kuwa ni wajumbe na vyombo vya furaha ya Injili

Katika mazungumzo kati ya VIWAWA na Askofu mkuu, Baba Askofu mkuu Nkwande amewatahadharisha vijana kuwa makini kwani wapo baadhi yao ambao wanatumika kuihujumu imani na Kanisa kwa ujumla kwa ushawishi wa nguvu ya pesa. Askofu mkuu anasisitiza kuwa, “Mkristo mkatoliki lazima akae imara, aipende imani yake, aitetee imani yake, ailinde na hata ikiwezekana kuifia.” Askofu mkuu Nkwande anaongeza kusema kuwa ni fedheha kijana mkatoliki kutumika kuihujumu imani kwa kununuliwa kwa pesa. Katika mazungumzo hayo Askofu mkuu Nkwande amewataka pia vijana kujijenga katika fadhila ya nidhamu akisema kila kijana anapaswa kuwa na shauku ya kuonekana kuwa ni mtu wa nidhamu. Askofu anasema, “ni jambo linaloleta faida ikiwa kijana atajulikana kama mtu mwenye nidhamu, utu, utulivu na ucheshi.” Katika kukabiliana na mahitaji ya vijana na changamoto zao Askofu mkuu Nkwande amesema ipo ndoto ya kuanzisha Kituo cha vijana katika Jimbo la Mwanza ambacho kitakuwa na miundo mbinu inayofadhilia utume, malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya katika nyanja zote za kielimu, kimaadili, kimwili na kiroho. Ameongeza kuwa kati ya huduma zitakazotolewa katika kituo hicho ni huduma ya ushauri nasaha ili kukabiliana na changamoto za vijana hasa: ulevi na uvutaji bangi na nyinginezo zinazowaathiri vijana. Kadhalika Askofu Nkwande amewataka vijana kutoona aibu kufanya shughuli mbalimbali halali kwa lengo la kujikomboa kiuchumi, hata kama shughuli hizo zinadharaulika katika jamii.

Ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya
Ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya

Katika mazungumzano hayo kati ya Askofu mkuu Nkwande na VIWAWA, vijana nao walipata fursa ya kumshirikisha Askofu mkuu mahangaiko na changamoto zao. Vijana wameeleza kuwa katika baadhi ya parokia hakuna usimamizi mzuri wa utume wa vijana na hivyo kumwomba Askofu mkuu kuwahimiza Mapadre kuutazama kwa namna ya pekee utume wa vijana ili kuleta ufanisi. Na hata Askofu mkuu mwenyewe ameonesha masikitiko yake kwa idadi ndogo ya vijana waliohudhuria kongamano hilo na amewakumbusha Mapadre kuuthamini utume wa vijana kwani unasaidia “kuandaa Kanisa linalofuata.” Lakini pia Askofu mkuu amewasihi vijana kuwa na utayari wa kushiriki semina na makongamano mbalimbali katika ngazi za parokia na jimbo kwani kuna wakati mwitikio wao unawakatisha tamaa Mapadre. Askofu mkuu Nkwande anakazia kusema kuwa makongamano na semina za vijana ni fursa ambazo vijana hupata nafasi ya kushirikishana na kujijenga zaidi. Vijana pia wamependekeza somo juu ya vyama vya kitume liongezwe katika mitaala inayotumika kufundishia imani ili tangu mwanzo mwamini ajue umuhimu wa kushiriki katika vyama mbalimbali vya kitume. Vijana wamebaini kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira ni moja ya mahangaiko yao ambayo kwa namna moja au nyingine yanadhoofisha utume wao katika kanisa. Hivyo wameomba Jimbo liangalie namna ya kuwawezesha vijana hasa katika sekta ya kilimo kwa kuangalia upatikanaji wa rasilimali ardhi ambayo inaweza kutumiwa na vijana kwa kilimo.

Vijana wanaomba kuwezeshwa ili wajikite katika kilimo.
Vijana wanaomba kuwezeshwa ili wajikite katika kilimo.

Katika kuhitimisha mazungumzo na vijana, Askofu mkuu Nkwande ametoa wito kwa vijana wa Jimbo Kuu la Mwanza kujiandaa na hatimaye kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Siku ya Vijana Duniani litakaloadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1-6, Agosti 2023 kutokana na kushindwa kufanyika mwaka 2022 kufuatia maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Vijana Duniani kwa mara ya kwanza yalifanyika katika mji wa Boenos Aires huko Argentina na hufanyika kila baada ya miaka miwili.  Askofu mkuu Nkwande anasema endapo kijana ataanza kujipanga mapema anaweza kufanikisha adhima ya kushiriki kongamano hilo ambalo ni fursa ya kukua kiimani, kiutu na kujenga mafungamano ya kijamii pamoja na kupata mwono mpya wa maisha. Kijana inuka, shughuli hii inakuhusu!

23 Novemba 2022, 16:13