Dhamira ya sala ambayo Maandiko Matakatifu yametupatia pamoja na dhamira ya umisionari wa Kanisa tunayoiadhimisha katika dominika hii havipingani, bali vinakamilishana. Dhamira ya sala ambayo Maandiko Matakatifu yametupatia pamoja na dhamira ya umisionari wa Kanisa tunayoiadhimisha katika dominika hii havipingani, bali vinakamilishana. 

Tafakari ya Dominika 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala na Umisionari

Tafakari katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, inajikita katika kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya: “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu (Mdo. 1:8). Katika maneno hayo ambayo Kristo aliwaambia Mitume kabla ya kupaa kwake mbinguni, Baba Mtakatifu anatualika tutafakari mambo matatu: Ushuhuda wa Mkristo, Mpaka miisho ya Dunia & Roho Mtakatifu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kila mwaka dominika inayotangulia dominika ya mwisho ya mwezi wa kumi, Kanisa huadhimisha dominika ya misioni. Neno misioni linatokana na neno “kutuma”. Katika dominika hii kanisa linakumbuka asili yake, kwamba lenyewe ni chombo ambacho Kristo amekituma kiende na kusambaa ulimwenguni kote kupeleka Habari Njema ya wokovu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). 1. Baba Mtakatifu anasema "Mtakuwa mashahidi wangu" ni wito na mwaliko wa kila mkristo mbatizwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Hili ni wazo kuu na kiini cha mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake kwa kurejea katika utume wao. Wafuasi wanapaswa kuwa mashuhuda wa KristoYesu, kwa kutegemea neema ya Roho Mtakatifu watakayempokea. Baba Mtakatifu anasema "Mpaka miisho ya dunia" ni dhana inayoonesha umuhimu wa udumifu wa utume wa uinjilishaji wa ulimwengu wote.

Sala na umisionari ni chanda na pete vinakamilishana
Sala na umisionari ni chanda na pete vinakamilishana

UFAFANUZI WA MASOMO: Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanaendelea kutupatia ujumbe kuhusu sala, ujumbe ambao tumeanza kuutafakati katika dominika iliyopita ya 29 ya mwaka C. Fundisho kuhusu sala ni fundisho pana na kila mara tunapolipokea linakuja kusisitiza kitu kile kile katika vipengele au nyanja tofauti tofauti. Somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha Yoshua bin Sira (YBS 35:15b-17, 20-22°) linakuja kutuonesha ni nini ambacho sala inabeba. Na linatuonesha kuwa sala inamletea mwombaji matumaini ya Mungu anayeokoa. Kitabu hiki kinarejea kipindi cha kihistoria ambapo dola ya Wayunani (Wagiriki) walitawala karibu dunia nzima. Katika Uyahudi Wayunani hawa walitawala kimabavu na walitafuta kila njia kufuta tamaduni za Kiyahudi na kuleta tamaduni zao za kiyunani. Ni kipindi ambacho Uyahudi ilitawaliwa kwa uonevu na kila aina ya uvunjifu wa haki. Ni katika kipindi hiki wayahudi wanaikumbuka Torati na wanarudi kujishikamanisha nayo katika sala. Ni hapa wanapoongozwa kulirudia Agano, agano ambalo Mungu alijitambulisha kuwa ni Mungu aliye karibu na wote wanaomlilia. Ni Mungu ambaye huisikiliza sala ya mtu mnyenyekevu, mtu asiye na msaada, mtu ambaye kimbilio pekee alilonalo ni kwake kama walivyokuwa wao katika kipindi hicho kigumu. Ni hapo waliporejeshewa tumaini la kuendelea kumwamini Mungu na kumtumainia yeye katika nyakati ngumu za maisha yao ya kijamii na ya kisiasa. Sala inainua matumaini ya waliokata tamaa.

Sala inawainua wale waliovunjika na kupondeka moyo
Sala inawainua wale waliovunjika na kupondeka moyo

Somo la Injili (Lk 18:9-14),  lenyewe linakuja kutuonesha ni kwa namna gani tumjongee Mwenyezi Mungu wakati wa sala? Yesu anatoa mfano wa watu wawili waliokwenda hekaluni kusali, mmoja alikuwa farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. Watu hawa tayari waliwakilisha aina mbili za watu katika jamii. Farisayo ni kundi la wale waliojiona watakatifu, wale wanaojua kila kitu kuhusu sala na kuhusu Mungu. Yeye alipofika hekaluni alianza kujisifu kuwa sio kama watu wengine wadhambi na yuko hivyo kwa sababu ya mambo mengi mazuri anayofanya. Mtoza ushuru yeye aliwakilisha kundi la wale walioonekana wadhambi na watu wasiojua chochote kuhusu dini. Yeye alipofika hakusogea hata mbele bali alibaki nyuma akijipigapiga kifua kuomba toba. Kati ya hawa watu wawili, Yesu anasema aliyesali vizuri ni yule mtoza ushuru. Alisali vizuri sio tu kwa sababu alikiri udhaifu wake mbele ya Mungu bali pia alijongea katika sala kwa unyenyekevu, unyenyekevu ulio ndani yake na uchaji na hofu ya Mungu. Katika mfano huu, Injili inatufundisha kuwa namna nzuri ya kumjongea Mungu katika sala ni ile ya  unyenyekevu. Kusali kwa kujiangalia mwenyewe na si kwa kujilinganisha na wengine wala kwa kujionesha. Mungu hahitaji yote hayo. Anachohitaji kuona ni moyo uliojiweka tayari kupokea mema yake.

Sala inafumbatwa katika unyenyekevu
Sala inafumbatwa katika unyenyekevu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tafakari yetu ya leo, katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, inajikita katika kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya kwa mwaka huu. Kauli mbiu hii ambayo tumeitaja mwanzoni mwa kipindi hiki inabeba maneno “nanyi mtakuwa mashahidi wangu (Mdo. 1:8). Katika maneno hayo ambayo Kristo aliwaambia Mitume kabla ya kupaa kwake mbinguni, Baba Mtakatifu Francisko anatualika tutafakari mambo matatu. Jambo la kwanza ni kuwa, kuwa shahidi wa Kristo ni wito wa kila mkristo. Jambo la pili ni kuwa hadi leo bado kuna hitaji la kwenda “mpaka miisho ya dunia” kupeleka Habari Njema ya wokovu. Jambo hili ambalo kwa kiasi kikubwa ndio limebeba taswira ya umisionari, inatugusa sote: wale wanaotoka na kwenda kufanya umisionari na wale ambao wanawawezesha wamisionari kwa hali na mali kutoka na kwenda kufanya umisionari. Jambo la tatu na la mwisho ni uhakika wa uwepo wa Roho Mtakatifu anayeimarisha na kuongoza wajibu wa umisionari wa Kanisa. Dhamira ya sala ambayo Maandiko Matakatifu yametupatia pamoja na dhamira ya umisionari wa Kanisa tunayoiadhimisha katika dominika hii havipingani. Si kwa bahati mbaya kwamba Mtakatifu Msimamizi wa Misioni ambaye ni Mt. Theresa wa Mtoto Yesu ni mtakatifu ambaye hakusafiri kwenda popote kuhubiri. Yeye alikuwa ni mtawa wa ndani na aliuishi utawa wake akisali kuliombea Kanisa na kuuombea utume wa Kanisa. Sala, kiini cha maisha ya mkristo ni kiini pia cha umisionari wa Kanisa.

Liturujia D30
21 October 2022, 17:30