Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Udumifu katika maisha ya sala, changamoto ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na upendo Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Udumifu katika maisha ya sala, changamoto ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na upendo 

Tafakari Dominika 29 Mwaka C wa Kanisa: Udumifu Katika Sala na Uaminifu Katika Kutenda Haki

Udumifu katika haki na sala ni mchakato unaokita mizizi yake katika sala ya moyo inayomkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuomba huruma na msamaha kwa kutambua kwamba, binadamu ni mdhambi, daima anahitaji msamaha na huruma ya Mungu. Hii ni sala inayopamba siku ya mwamini, kwa sababu sala hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwamini.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama!Kusali sio kumshawishi Mungu atende kadiri ya matakwa yetu, bali kumuomba neema zake za msaada ili tuweze kupokea mapenzi yake katika maisha yetu. Kusali ni kuinua mioyo yetu kwa Mungu kama anavyotufundisha Mtakatifu Yohane wa Damasko, ndio kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa na Mungu. Kama ndivyo kwa nini basi leo tunaalikwa kusali daima bila kukoma? Nini hasa maana ya sala? Sehemu ya Injili ya leo, Yesu anatuonesha nini maana ya sala kwa kutumia mfano wa hakimu au kadhi dhalimu pamoja na mjane aliyekuwa analilia haki yake. Wakati wahusika wakuu katika Injili ya Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa, Lk 18:1-8 ni wawili, kwanza ni kadhi au hakimu dhalimu, asiyekuwa na hofu ya Mungu, mtu mwenye moyo mgumu na labda kwa lugha ya siku hizi mmoja anayejimwambafai kwa kila hali, na upande wa pili ni mjane mnyonge, asiyekuwa na mtetezi. Katika Maandiko Matakatifu tunaona yatima na wajane kuwa ni ishara ya watu wanyonge na wasio na watetezi isipokuwa Mungu pekee. Huyu mjane leo hakujali unyonge wake au kukosa kwake fedha za kuweka wakili, bali aliona silaha pekee ni kutokukoma kudai na kuomba haki yake dhidi ya maadui na maasimu wake mbele ya kadhi yule dhalimu. Baada ya kuona wahusika hawa wakuu wawili tunaona Injili inaendelea kwa mazungumzo ya moyoni kwa yule kadhi dhalimu. Hakimu dhalimu anakiri kuwa yeye ni mtu asiye na hofu ya Mungu wala kujali watu, bali anaona ni heri ampatie haki mjane yule kwani alikuwa hakomi kumfuata na kumsumbua ili apate haki yake. Kadhi anachoshwa na hali ile, na hivyo kwa vile hakutaka tena usumbufu ule anaona ni heri amtendee haki mjane yule.

Waamini wanapaswa kuwa ni wadumifu katika sala kwa kujiaminisha kwa Mungu
Waamini wanapaswa kuwa ni wadumifu katika sala kwa kujiaminisha kwa Mungu

Ili kupata ujumbe wa sehemu ya Injili ya Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa tunajiuliza pia, ni nani anamwakilisha hakimu dhalimu? Hata kama tumeona tabia za kadhi dhalimu si nzuri kwani hakuwa na hofu ya Mungu bali kwa hakika anamwakilisha Mungu. Si nia wala shabaha ya Yesu kumuonesha Mungu aliye mgumu na mkatili, na asiyeguswa na shida na kilio cha wanyonge wanaomlilia, bali ni kutualika kuwa na matumaini bila kukoma kama yule mjane aliyekuwa anasaka haki yake kwa hakimu dhalimu. Si kwamba Mungu hasikii sala zetu, bali tunaalikwa kusali daima na kubaki wenye imani na matumaini. Sala ya kweli inaambatana na imani ya kweli. Ni shabaha ya Yesu leo kutualika kuwa watu wa sala daima bila kukoma na tukiwa wenye imani ya kweli kwa Mungu. Kusali ni kuingia katika mahusiano ya daima na siku zote na Mungu, ni kuwa na hakika ya kuwa naye katika nyakati zote za maisha yetu. Kama ilivyokuwa katika nyakati za Yesu hata nyakati zetu pia tunaona ukosefu wa haki katika maeneo mbali mbali, iwe kati ya uwanda wa siasa na serikali zetu, uwanda wa kimahakama, kijamii na hata kidini. Sisi kama waamini tunaalikwa daima kuwa watu wa haki na kumwomba Mungu ili haki iweze kutawala duniani. Mwinjili Luka anaandika wakati ambapo Wakristo wa Kanisa la mwanzo walikuwa wakipitia madhulumu na mateso mengi, na hivyo kuwaalika kubaki katika sala na imani. Ni mwaliko hata kwetu leo tunaposhuhudia ukosefu wa haki katika jamii zetu hatuna budi kubaki katika sala yenye matumaini na imani kubwa.

Kila mwamini Mkristo anaalikwa kuwa mjumbe wa haki, yaani kuwatendekea wengine kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu, kuwatakia na kuwatendea kwa wema wengine wanaotuzunguka. Kama nilivyotangulia kusema kuwa kusali sio kumshawishi Mungu atende kadiri ya matwaka yetu, bali kuweza kupokea mpango na mapenzi yake katika maisha yetu. Ni kuinua mioyo yetu mbele yake, ni njia pekee inayodumisha mahusiano yetu ya upendo na Mungu wetu. Hatusali kwa kuwa tuna shida na mahangaiko tu, hivyo tunataka Mungu asikie kilio na shida zetu bali ni kuonesha upendo na imani yetu kwake. Ni Yeye aliye kweli Mungu na Bwana wetu, ni Yeye aliye kimbilio letu katika kila hali za maisha yetu. Iwe ni nyakati nzuri au zile ngumu daima tunaalikwa kubaki katika mahusiano naye bila kukata tamaa au kupoteza imani. Kusali ni kuingia katika mahusiano ya upendo na Mungu aliye Baba yetu. Tunaporejea katika Maandiko Matakatifu tunaona kusali daima ni kubaki katika mahusiano na Mungu bila kujali nyakati na hali zetu. Ni njia ya kuonesha imani yetu kwake bila kujali magumu au mepesi tunayopitia. Mtume Paulo katika waraka wake kwa (Warumi 15:30) anatualika kupambana katika sala. Kusali ni kupambana kadiri ya Mtume Paulo. Yakobo alikesha katika kupambana na Mungu ndio kusema alikesha katika sala. (Mwanzo 32:23-33).

Waamini wawe ni wajumbe na vyombo vya haki na amani.
Waamini wawe ni wajumbe na vyombo vya haki na amani.

Mwinjili Luka anatuhakikishia leo kuwa hakika sala zetu zinamfikia Mwenyezi Mungu aliye asili na chanzo cha wema wote. Kama hakimu dhalimu aliweza kumpatia haki mjane yule, je, si zaidi Mungu Baba yetu aliye mwema na mwenye huruma. (Luka 11:13) Kama sisi tulio waovu tunaweza kuwapatia mambo mema watoto wetu; Je, si zaidi kwa Mungu Baba yetu mwema wa mbinguni? Hivyo msingi wa sala ni imani kwa Mungu. Tunabaki katika sala daima kwani tuna imani katika wema na huruma na upendo wa Mungu kwetu. Kusali ni kukua katika imani kwa Mungu, hivyo tunaalikwa kusali tukiwa wenye imani na matumaini kwa Mungu, hatuna sababu ya kuwa na mashaka kwani Mungu wetu ni wema wenyewe na mapenzi yake kwetu daima ni mema. Kanisa lile la mwanzo linawakilishwa na huyu mjane, kwani halikuwa na mtetezi bali silaha pekee ni kudumu katika sala. Hata nasi leo kama Kanisa au kama muumini mmoja mmoja tunaalikwa kubaki na silaha moja tu nayo ni sala na kusali kwa imani. Kubaki usiku na mchana yaani bila kukoma katika sala. Mungu wetu ni mwaminifu, hivyo mwinjili Luka anatuonesha kuwa Mungu ataleta haki duniani. Katika unyonge na udogo wetu tunahakikishiwa kuwa ni Mungu pekee aliye mtetezi wetu na ni Baba yetu Mwema.

Mungu daima ni mwaminifu na ndio Injili ya leo inahitimishwa na swali; Je, Mwana wa Adamu atakapokuja duniani ataikuta imani? Imani ndio nguzo yetu pekee tunapobaki katika sala. Hatuwezi kusema tunasali kweli kama tunakosa imani. Imani kama tulivyotafakari Dominika chache nyuma tuliona kuwa ni zawadi, hivyo hatuna budi kama mitume kusali bila kukoma ili tukue katika imani na hapo tunaweza kubaki bila kukoma katika sala. Imani ni tukio la kukutana na Mungu katika maisha yetu, kumruhusu Mungu aongoze maisha yetu, ni kuivaa mantiki ya Mungu katika kila hali za maisha yetu. Imani ni hitaji la lazima katika maisha ya sala, kusali ni kuonesha imani yetu katika wema, ukuu na uweza wa Mungu kwani hatuwezi lolote bila neema zake za msaada katika safari ya maisha yetu ya hapa duniani. Injili ya leo inatualika nasi kutafakari kuwa Mwenyezi Mungu anasikiliza sala zetu na ni mwaminifu daima kwani kwa muda wa kufaa au saa ile ya neema anajibu kila sala yetu. Kuna nyakati tunashawishika kuona kuwa Mwenyezi Mungu hasikii maombi na sala zetu, bali leo mwinjili anatuonesha kuwa Mungu daima ni mwaminifu na mwema kwetu sote. Mwenyezi Mungu daima anajibu sala na maombi yetu. Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta katika kuonesha nguvu ya sala aliwahi kusema; “Ningekuwa sisali nisingeweza kufanya lolote”. Ni mama anayetambua bila Mungu asingeweza kutimiza mapenzi ya Mungu ya kuwaonesha upendo maskini na wahitaji aliowahudumia. Mama yule aliweza kufanya kile ambacho wengi wetu leo tunakistaajabia kwa kuwa alipata nguvu katika kusali. Ni kwa njia ya sala aliweza kuchota nguvu ya kuwapenda na kuwatendea wengine kwa upendo na huruma. Ni kutoka kwa Mungu aliye asili ya wema wote nasi tunaweza kuwa wema kwa wengine.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa sala
Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa sala

Mtakatifu Yohane Paulo II anatukumbusha kwa maneno haya; “Siku bila sala ni siku iliyopotea. Tunashindwa mapambano mengi kwa kuwa tunasali kidogo”. Maisha ya Kikristo ni mapambano dhidi ya yule muovu na uovu, ni vita ya kiroho, hivyo kamwe hatuwezi kushinda vita hiyo kama sisi sio watu wa sala, sio watu tunaosaka na kuchota nguvu ya kiroho kwa njia ya sala. Kusali ni kuwa na hakika ya kukutana na Mungu, kukutana na neema zake ambazo kwazo tunaweza nasi kupambana na adui yetu. Ni katika sala tunapata nguvu ya kuendelea na mapambano ya kiroho katika maisha yetu. Mama yetu Bikira Maria ndiye katekista na mwalimu wetu wa maisha ya sala. Kusali ni kukubali mpango wa Mungu katika maisha yetu, na sio matakwa yangu, ni kuruhusu mantiki ya Mungu ituongoze, ni kusema ndio kwa Mungu, ni fiat! Ni kama Mama yetu Bikira Maria anayetambua kuwa ni mtumishi wa Bwana, na hivyo Bwana atende kadiri ya mapenzi yake. Ni kuwa na hakika katika wema na uweza wa Mungu kama harusini Kana, ambapo Maria anaona uduni wa kutindikiwa divai, na hapo kwa imani akimuomba Yesu kuwa hawana divai. Ni sala inayosukumwa na imani daima.

Mama yetu Bikira Maria ni kidole kinachotuonesha wapi twende wakati wa kutindikiwa katika maisha yetu, nyakati za mahangaiko na hata za furaha daima hatuna budi kusali kwa imani. Kusali ni kuwa na hakika katika wema wa Mungu na ndio kusali kwa imani, na hivyo tunaalikwa kusali daima. Kusali ni kuingia katika mahusiano na Mungu mwenyewe, ni kujikabidhi wazimawazima mikononi mwa Mungu. Ni kuinyanyua mioyo yetu ili ipate kutulia mikononi mwa Mungu. Mara nyingi tunashawishika kudhani kuwa Mungu hasikii sala zetu, ingawa katika uhalisia ni sisi tunaoshindwa kumsikiliza Mungu anayejibu kila sala tunayoitolea mbele zake. Hatuna budi kuzidi kumwomba Mungu Roho Mtakatifu atuongoze na atufundishe namna nzuri ya kusali na zaidi sana jinsi ya kuitambua na kuisikiliza sauti ya Mungu katika maisha yetu. Tumwombe Mungu atujalie jicho na sikio la imani ili tuweze kuwa watu kweli watu wa sala, ili tudumu katika mahusiano ya ndani kabisa naye. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

12 October 2022, 14:33