Sudan Kusini:Ukabila ni adui mkubwa wa amani na kuishi kwa pamoja
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Ukabila ni adui mkubwa sana katika nchi, hivyo haiwezekani kujenga taifa au Kanisa katika msingi wa ukabila. Ikiwa wanaujenga juu ya ukabila watasema kwamba hawana Ubatizo, Komunio Takatifu, Kipaimara na watanguka kwa sababu kuna jambo ambalo linawagawanya. Ni mahubiri ya Askofu Mkuu Stephen Ameyu Martin Mulla, wa Jimbo Kuu katoliki la Juba na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Torit, aliyotoa hivi karibuni mnamo tarehe 25 Septemba 2022 katika Misa kwenye Parokia ya Mama Yetu wa Mateso huko Torit nchini Sudan Kusini.
Askofu Mkuu Ameyu alisema, kwamba ukabila hauwezi kusalisaidia Kanisa na taifa kuendelea badala yake utaweza kuwapelekea baadhi ya wakristo kuwa na mashaka ya sakramenti. Kwa maana hiyo aliwatia moyo waamini na makuhani ili kupambana na ukabila nchini Sudan kusini kwa sababu huyo ndiyo adui mkubwa ambaye anahitaji jitihada zao za pamoja ili kufikia mwisho kwa kutumia hata zana zote.
Katika kukumbusha kuwa Sudan Kusini ni taifa jipya ambalo lilipata uhuru wake kutoka Sudan mnamo Julai 2011, hivyo kuwa na mizizi ya ukabila zaidi kuliko utaifa, Askofu Mkuu Ameyu aliomba nguvu ya Mungu kwa ajili ya kupambana dhidi ya ukabila huo kwa sababu alisema: ni ukabila tu ambao unawagawanya. Katika taarifa iliyotolewa na Shirika la habari za Kimisionari Fides, lilibainisha kwamba Askofu Mkuu Ameyu alisema wokovu utawezekana kwa wote hao, wawe matajiri au maskini walivyo, kadiri ya watakavyo shirikiana ili kufanya kazi pamoja kwa sababu ni kweli tu kupitia ushirikano wao wanaweza kujiokoa.
Katika mahubiri hayo alisisitiza ulazima wa kushirikiana kati ya wajumbe wa kanisa yaani Makleri na walei kwamba ikiwa kuna ushirikiano mdogo kati ya makleri na walei inapelekea kushindwa kwa sehemu kubwa ya shughuli za kiparokia au za kijimbo. Katika fursa nyingi, maaskofu wa Sudan Kusini wamekuwa wakikumbusha waamini kwamba ukabila hauendani na imani ya kikristo na kwamba binadamu wote ambao wameumbwa na ni mfano na sura ya Mungu, hakuna kabila lililo bora zaidi ya kabila jingine. ( Askofu Barani Edwardo Hiiboro Kussala, wa Tombura-Yambio, katika Ujumbe wa ajili ya amani 2020).
Nchini Sudan Kusini, kuna makabila 64. Makundi ya kwanza ya kikabila ni Wadinka wanafuatia Wanuer. Kwa maana hiyo si mara chache kusikia mtu au makundu yanatelekezwa au kupata hali fulani ya kudhalauliwa kwa sababu ya utofauti wa kikabila kati yao na wenzao wa Taifa la Sudan Kusini, wakati huo huo mafunzo msingi ya sera za kisiasa Sudan Kusini zinagawanyika kwa misingi ya makabia ya wakuu na wanajeshi. Vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyoibuka mnamo Desemba 2013 viliona walio mstari wa mbele makabila ya Nchi wakipigana dhidi ya makabila mwengine.