Askofu Lazarus Msimbe Afafanua Sifa za Kiongozi wa Maisha ya Kiroho: Mashemasi Wapya 23!
Na Angela Kibwana, Morogoro na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican
Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu; Kwa kusimamia na kubariki ndoa; Kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa niaba ya Mama Kanisa! Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” ni sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia. Mwongozo unatoa kwa muhtasari wa sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja.
Mwongozo unapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Seminari na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo. Malezi endelevu ni nyenzo msingi zinazomwezesha Padre kupyaisha maisha na utume wake, kwa kuwa na wongofu endelevu, kwa kusoma alama za nyakati katika mwanga wa imani, upendo wa kichungaji na sadaka binafsi.
Malezi haya ni wakati wa masomo ya falsafa ili kujenga dhana ya Ufuasi wa Kristo na masomo ya taalimungu ni kumwezesha jandokasisi kujifananisha zaidi na Kristo Yesu mtumishi na mchungaji mwema na hatima ya safari hii ya malezi ni Daraja ya Ushemasi na hatimaye Daraja takatifu ya Upadre. Majiundo endelevu kimsingi yanajikita katika upendo wa shughuli za kichungaji unaofumbatwa katika maisha na utakatifu wa Wakleri. Ni wajibu wa Maaskofu kuwa makini kwa maisha na wito wa Mapadre wao vijana, ili wasijikute wanaingia katika mazingira magumu na hatarishi katika maisha na wito wao wa Kipadre. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na kwamba, wao ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa na wala si wafanyakazi wa mshahara. Wawe makini katika kupambana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kukuza umoja na udugu katika maisha ya Kipadre sanjari na Mashauri ya Kiinjili. Ni katika muktadha huu, Mashemasi wapya wanakumbushwa kwamba, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo, wameandaliwa vyema: kiutu, kiakili, kiroho na kichungaji ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika maisha ya watu wanaowazunguka. Mashemasi wapya watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!
Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS., wa Jimbo Katoliki la Morogoro, hivi karibuni ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 23 kutoka katika Mashirika manne yanayotekeleza dhamana na utume wao nchini Tanzania. Katika mahubiri yake, amekazia sifa kuu za mhudumu wa maisha ya kiroho kuwa ni hekima, juhudi na maarifa. Awe ni mtu wenye sifa njema, imani thabiti, na anayejitahidi kuongozwa na Roho Mtakatifu katika maisha yake. Kumbe, baada ya malezi na majiundo makini, Kanisa linawatarajia Mashemasi wapya kuwa ni wahudumu bora wa Mafumbo ya Kanisa. Kristo Yesu alikwenda mjini Galilaya akihubiri Habari Njema ya Wokovu kwa kusema, “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili”. Mk. 1:15. Askofu Msimbe amefafanua kuhusu tamko hili la Kristo Yesu kama msingi wa mafundisho yake, kwa kukazia toba, wongofu wa ndani; imani, upendo na wajibu wa mwaamini katika maisha yake ya Kikristo. Mashemasi wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika ukweli, amani, matumaini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wanatumaini kwa namna ya pekee kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na: magonjwa, matatizo na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii.