Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukuu wa Fumbo la Msalaba: Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukuu wa Fumbo la Msalaba: Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. 

Tafakari Dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukuu wa Fumbo la Msalaba, Ufunuo wa Mungu

Tafakari: Jambo la kwanza ni udogo wa uwezo wa akili ya mwanadamu usivyoweza kumjua Mungu na kufahamu mipango yake bila Mungu mwenyewe kumfunulia kwa hekima yake. Na jambo la pili ni kuwa gharama ya imani yetu ya Kikristo ni Msalaba ndiyo kuachana na yote yaliyo kikwazo cha kumfuata Kristo ikiwa ni pamoja familia zetu, mali na hata nafsi zetu. Hapa yataka moyo!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 23 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatufundisha mambo makuu mawili: Jambo la kwanza ni udogo wa uwezo wa akili ya mwanadamu usivyoweza kumjua Mungu na kufahamu mipango yake bila Mungu mwenyewe kumfunulia kwa hekima yake. Na jambo la pili ni kuwa gharama ya imani yetu ya Kikristo ni Msalaba ndiyo kuachana na yote yaliyo kikwazo cha kumfuata Kristo ikiwa ni pamoja familia zetu, mali na hata nafsi zetu. Kwa mtazamo wa kibinadamu jambo hili si rahisi, lakini kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu inawezekana. Basi tumruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani mwetu na afanye kazi yake ya kutukumbusha daima aliyotufundisha Yesu na atuwezeshe kuyaishi kwani kwa nguvu zetu hatuwezi. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 9:13-18); ni sehemu ya sala ya Mfalme Sulemani ya kumwomba Mungu hekima ili aweze kutambua mema na mabaya na aweze kuwaongoza watu wake katika haki na kweli. Sulemani aliomba hekima kwa kuwa alitambua kuwa uwezo wa mwandamu haujakamilika. Hivyo hakuna anayeweza kufahamu mipango na mawazo ya Mungu kwa uwezo wake mwenyewe ndiyo maana anasema; “Ni mtu yupi anayeweza kulijua shauri la Mungu? Au ni nani anayeweza kuelewa mapenzi yake? …Kwa shida tu, twayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni shida kuyaona…” (Hek 9:13, 16). Tumaini letu liko kwa Mwenyezi Mungu, ambaye kwa njia ya Roho wake ndani mwetu, hutuwezesha kufahamu mipango yake. Kumbe somo hili latufundisha kumtegemea Mungu katika shughuli zetu za kila siku, hasa katika magumu na katika uamuzi wa jambo lolote kubwa. Hii ni kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa; na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Tumwombe Roho Mtakatifu ili atuongoze vyema katika kuyatumbua mapenzi ya Mungu na kuyatimiza.

Waamini wamtegemee Mungu katika maisha na utume wao
Waamini wamtegemee Mungu katika maisha na utume wao

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Filemoni (Fil. 1: 9-11,12-17). Filemoni alikuwa kijana tajiri kutoka Kolosai. Mtume Paulo alimlea katika Imani kwa Kristo akawa Mkristo mwema na Jumuiya ya Kikristo ya Kolosai ikawa inakusanyika katika nyumba yake kusali. Katika barua hii Paulo anamsihi na kumshauri Filemoni ampokee Onesmo mtumwa wake aliyemtoroka, si kama mtumwa tena, bali kama ndugu halisi katika Kristo maana kwa ubatizo sisi sote ni ndugu. Katika barua hii tunaona moyo wa upendo wa Paulo. Itakumbukwa kuwa Paulo anaandika barua hii katika uzee wake na akiwa mfungwa huko Roma. Katika Milki ya Kirumi kulikwa na “Watu huru” na “Watumwa”. Kila mtu huru alikuwa na watumwa wake. Hali ya kuwa mtumwa ina taabu nyingi maana haki ya maisha ya mtumwa iko mikoni mwa Bwana wake. Kama ilivyo hata, sasa nyakati hizo mtumwa aliweza kununuliwa, kuuzwa na hata kuuawa ikiwa Bwana aliona mtumwa husika amekuwa mgonjwa, mzee, au kilema na kwamba hana faida tena kwake. Filemoni alikuwa mtu huru na tajiri. Hivyo alikuwa na watumwa wake mmoja wao akiwa Onesmo. Mapokeo yanasema kuwa Onesmo aliiba fedha kwa Filemoni na kutoroka kutoka Kolosai. Katika kukimbia kwake alijikuta mjini Roma. Baada ya fedha alizoiba kumwishia alienda kujisalimisha kwa Mtume Paulo akiwa katika kifungo huru katika nyumba binafsi, lakini chini ya uangalizi wa maaskari (Mdo 28:30).

Mtume Paulo alimpatia Onesmo hifadhi kwa muda, akimfundisha imani ya Kikrito na kumfanya atambue makosa yake ya kuiba, hivyo afanye toba, arudi kwa Bwana wake na kuomba msamaha. Baada ya kumfundisha, alimbatiza. Onesmo alionja upendo wa Paulo na hivyo alijitoa kikamilifu kumtumikia. Paulo akampenda sana. Baadae Paulo aliamua kumrudisha Onesmo kwa Bwana wake – Filemoni kwa sababu Onesmo alikuwa bado na chapa ya utumwa na kisheria alipaswa kumrudisha. Na kwa kuwa Onesmo alitoroka na zaidi sana aliiba, adhabu yoyote ilikuwa halali kwake hata ya kifo. Ndiyo maana Paulo anapomrudisha Onesmo kwa Filemoni hamuachi aende peke yake bali anamtuma Tikito Mkolosai amsindikize akiwa na barua ya mbili moja kwa Filemoni na nyingine kwa jumuiya yote ya Kikristo ya Kolosai (Kol. 4: 7-9). Mtume Paulo daima aliandika barua zake kwa njia ya imla, ambapo katibu wake aliaandika kile anachomwambia yeye. Lakini barua kwa Filimoni aliiandika kwa mkono wake mwenyewe (Film 1:19), ili kuonesha msisitizo na umuhimu wa ujumbe wake wa upendo kwa Filemoni. Katika barua binafsi kwa Filemoni Paulo, anamsihi na kumwomba ampokee Onesimo kama ndugu katika Kristo na aweze kumpiga chapa ya kumfanya mtu huru (Film. 1:16). Maana kadiri ya sheria ya Kirumi, Bwana wa watumwa alikuwa na uwezo wa kumtangaza mtumwa wake kuwa mtu huru, akimpatia hati ya uhuru.

Toba na wongofu wa ndani ujenge na kuboresha mahusiano na Mungu na jirani
Toba na wongofu wa ndani ujenge na kuboresha mahusiano na Mungu na jirani

Mtume Paulo anamkumbusha Filemoni misingi ya imani yake kuwa; mbele ya Mungu hakuna mtu huru na mtumwa, kwa kuwa Kristo amewaweka watu wote huru kutoka utumwa wa dhambi, na kutufanya sote kuwa ni wana wa Mungu kwa sakramenti ya ubatizo. Jina Onesmo, asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha “Anayefaa”. Paulo anacheza na Jina hili na kumwambia Filemoni kwamba mtumwa wake alikuwa hafai kwa chochote, lakini sasa, amfaa sana, kama mtumwa na ndugu katika Bwana (Film. 1:11). Paulo anamhakikishia Filemoni kwamba yuko tayari kumlipa chcochote anachowiwa Onesmo (Film. 1:18). Katika Waraka kwa Jumuiya ya kikristo ya Kolosai, Paulo anawataka Wakristo wanaomiliki watumwa akiwaambia: “Ninyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kuwa nanyi pia mnaye Bwana mbinguni” (Kol 4:1). Kumbe tunaona kuwa barua za Mtume Paulo kwa Filemoni zikawa kichocheo cha kupinga biashara ya utumwa, ambayo ni aibu kubwa kabisa kwa mwanadamu. Nasi tuone ubaya wa biashara haramu ya binadamu na tuweke nia thabiti ya kupambana nayo na kuikomesha kwani sote tulikuwa watumwa katika dhambi nasi tumekombolewa kwa thamani ya Damu Azizi ya Yesu Kristo iliyomwagika Msalabani.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 14:25-33); inatoa fundisho gumu sana kulielewa na kulifuata katika hali ya kawaida ya kibinadamu. Fundisho hili ni kuwa katika kuitika mwito wa kumfuata Yesu; mali, ndugu na familia wanachukua mahali pa pili. Kumfuata Yesu ni kujitoa sadaka na kunahitaji udumivu. Tukirejea katika Maandiko Matakatifu tunakutana na sheria kuu ya zamani isemayo: “Waheshimu Baba na Mama yako” (Kut 20:12). Yesu katika Injili ya Yohane anatuagiza; “Amri mpya nawapa; pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi” (Yn 13:34-35). Lakini katika Injili tunayoisoma dominika hii ya 23 Mwaka C Yesu anatuambia: “Mtu yeyote, akija kwangu, asipomchukia baba yake, mama yake, mke wake, watoto, ndugu, na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Lk 14:26). “Vivyo hivyo, basi hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu, kama asipoachilia kila kitu alicho nacho” (Lk 14:33). Ni kana kwamba agizo hili la Yesu linapingana na Amri mpya ya mapendo na mafundisho ya Kale ya kuwawaheshimu Baba na Mama. Ujumbe wa Yesu hapa ni huu; kama wazazi, watoto, marafiki, jamaa zetu, mali na hata nafsi zetu, zinakuwa kikwazo katika kuitikia wito wa Mungu wa kuwa watakatifu, tunapaswa kuyaacha na kuyatupilia mbali kuliko kwenda kinyume na mapenzi Mungu. Uhusiano wetu na wanafamilia au marafiki haupaswi kupingana na uhusiano wetu na Kristo.

Gharama ya kumfuasa Kristo inadau sadaka na majitoleo binafsi
Gharama ya kumfuasa Kristo inadau sadaka na majitoleo binafsi

Hii ndiyo gharama na amana ya kumfuasa Kristo. Hii ndiyo gharama ya imani yetu. Ndiyo gharama ya ufuasi wetu kwa Kristo na ndiyo gharama ya ukristo wetu. Ndiyo maana katika mafundisho na maagizo mengine Yesu anasema; “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake…waache wafu wawazike wafu wao” (Lk 9:57-62); “Na kama mkono wako ukikukosesha ukate, jicho lako likikukosesha ling’oe” (Mt 18:8-9). Mafundisho haya si rahisi kuyapokea. Hii ni kwa sababu mapendeleo ya mwili mara nyingi yanapingana na mapenzi ya Mungu kwani mwili wenye uharibifu, huigandamiza roho. Mtazamo wa kidunia ni tofauti na mtazamo wa Kimungu, kama Paulo anavyotuambia kuwa; “Ujumbe wa msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu, maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu (1Kor 1:18, 25). Jambo hili nalo ni ngumu kulielewe kwa akili zetu za kibinadamu kama anavyosema nabii Isaya; “Mawazo ya Mungu si mawazo yetu, na njia zake si njia zetu kama mbingu zilivyo mbali na dunia ndivyo yalivyo mawazo ya Mungu na yetu”. Lakini tukiwa na moyo wa unyenyekevu na imani Mungu atatufunulia ukweli huu.

Hii ni kwa sababu, matatizo ya maisha yanaleta changamoto kubwa sana kwa Imani yetu kwa maana kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko nazo zinashindwa kubaini mambo ya Mungu katika uzuri wake. Na utamu wa mambo ya dunia huzifumba akili zetu, kwa shida tu, twayapambanua yaliyoko duniani. Hivyo ni Roho Mtakatifu ndiye anatuwezesha kuyaelewa mambo ya Mungu, kwani mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye isipokuwa Roho wa Mungu” (1Kor 1:11). Mtume Paulo aliwaasa Wagalatia akisema; “Basi nasema hivi, mwenendo wenu na uongozwe na roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Matokeo ya kuongozwa na roho ni Mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (Gal 5:16,22 – 25). Daima tuombe kuyapata hayo matokeo na kuyafanya yatawale maisha yetu. Tuwe wanyeyekevu na kukubali kufundishwa na Roho Mtakatifu tuwe na sikio sikivu kama anavyosema Nabii Isaya “Huniamsha sikio langu lipate kusikia kama wafundishwao” (Isa 50:4) tumwombe ayafungue macho yetu ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.

Dominika 23 Mwaka C

 

01 September 2022, 15:30