Tafuta

Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. Mambo msingi ya kuzingatia na kuendelezwa katika maadhimisho haya. Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. Mambo msingi ya kuzingatia na kuendelezwa katika maadhimisho haya. 

Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, 11 Septemba 2022: Mambo Msingi ya Kuzingatia

Mama Evaline Malisa Ntenga katika makala hii, anaelezea historia ya WAWATA, dhamana na wajibu wa WAWATA katika malezi na makuzi ya watoto na vijana ndani ya familia. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa WAWATA: Sera na mikakati ya kuwajenga wanawake kiuchumi, kwa kuanzisha Benki ya WAWATA. Kilele cha Jubilei ni tarehe 11 Septemba 2022. Usikose

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar es Salaam, Tanzania.

Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kuomba na kukimbilia: huruma, msamaha, neema na baraka ya kusonga mbele tena kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe ya Miaka 50 ya WAWATA ulifanywa na Askofu Edward Elias Mapunda, Mwenyekiti wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa Ibada ya Misa Takatifu, Kurasini, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika kipindi hiki kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA, wamekuwa wakiongozwa na Nyaraka zifuatazo: Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ambao kimsingi ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Ni wosia unaotoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni wosia unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha.

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe na wote.
Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe na wote.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao ya sasa yale ya baadaye! Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Mtakatifu Yosefu ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Hii ni changamoto kwa WAWATA kushirikiana kwa karibu sana na Umoja wa Wanaume Wakatoliki, UWAKA katika malezi na makuzi ya watoto wao kwa ajili ys ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Pili, ni Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa na Kitaifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo na changamoto zinazoikumba Jumuiya ya Kimataifa na Kitaifa. Huu ni msaada mkubwa katika mchakato wa kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbalimbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Udugu wa kibinadamu unakita mizizi yake katika umoja na ushirikiano. Kwa njia ya utamaduni wa udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia dhana ya upendo kwa watu wote, ili kujenga mahusiano, sheria, kanuni na taratibu zinazopania kudumisha amani na kuboresha maisha ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao. (Rej. Hotuba ya Kardinali Pietro Parolin, Uzinduzi wa Waraka wa “Fratelli tutti, tarehe 4 Oktoba 2020.)

Udugu na urafiki wa kijamii: fratelli tutti
Udugu na urafiki wa kijamii: fratelli tutti

Tatu, ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ambayo ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ambao WAWATA wanaalikwa kuutafakari kwa kina na kuchukua hatua muhimu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Nyaraka zote hizi, zikiwekwa kwa pamoja zinaunda kauli mbiu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya WAWATA yaani “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji”. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu Lk. 1:39: Mapendo kwa jirani: “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda…” Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa, katika makala hii, anaelezea historia ya WAWATA, dhamana na wajibu wa WAWATA katika malezi na makuzi ya watoto na vijana ndani ya familia. Malengo makuu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa WAWATA: Sera na mikakati ya kuwajenga wanawake kiuchumi, kwa kuanzisha Benki ya WAWATA. Kilele cha Jubilei ni tarehe 11 Septemba 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu, maonesho na uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya WAWATA, mahali walipotoka, walipo na matarajio yao mbeleni. Hili ni tukio la Kimataifa, Kitaifa, Kiekumene na Kidini.

Leo hii tumekutana nanyi ili kuelezea juu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) hapo Septemba 11 mwaka huu wa 2022. Hiki ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu ikijishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili kuwawezesha kutoa mchango wao kikamilifu kuliendeleza na kulistawisha Kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma na kiuchumi likiongozwa na Dhamira yake Kuu: Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika. Licha ya WAWATA kuanzishwa rasmi mwaka huo wa 1972 baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuridhia katiba yake, lakini pia chombo hiki ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu Paris, nchini Ufaransa. Tukio la Maadhimisho ya Jubilei hii ya Miaka 50 ya WAWATA, lilizinduliwa rasmi Uzinduzi wa Jubilei ulifanyika tarehe 25 Julai 2021 katika eneo la TEC, Kurasini, Dar es Salaam kwa kuongozwa na Kaulimbiu ya Jubilei isemayo "Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji, ambayo ndani yake imemeba ujumbe wa kaulimbiu tatu ambazo ni pamoja na ile ya WAWATA yenyewe (Upendo…), kaulimbiu ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.”

WAWATA: Tutumikie na Kuwajibika
WAWATA: Tutumikie na Kuwajibika

Baada ya uzinduzi huo wa kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Jubilei tuliazimia kufanya mambo kadhaa ambayo ni pamoja na: Kufanya uzinduzi ngazi za kanda, majimbo, parokia mpaka kwenye jumuiya. Kuendelea kutoe elimu ya kina juu ya utume wa mwanamke Mkatoliki na wajibu wake katika malezi ya familia. Kampeni ya kusafisha mazingira na kupanda miti isiyopungua 34,000 ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Baba Mtakatifu wa Laudato si. Lengo ni kuwafikia wahitaji na wale waliosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamjii (yaani kuwa sauti ya wasio na sauti) bila kujali imani zao tukitambua kuwa sote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu. Kutoa elimu kwa vijana wa kike ama WAWATA chipukizi kwa mpango wa Mafunzo ya Wakufunzi (TOT - Training of Trainers) bila kuwasahau VIWAWA (Vijana wa Kiume) na tumefanya hivyo ili kuyaishi kwa matendo Maandiko Matakatifu (Mithali 31 Maneno Ya Mfalme Lemueli juu ya mafundo aliyopewa na mama yake na 1Timotheo 1:5 tunapata Habari za Eunike na Lois waliomfundisha Timotheo imani. Kuendeleza na kufufua miradi mbalimbali iliyopo majimboni ili kutoa ajira kwa mama aweze kuchangia pato la familia na kutegemeza Kanisa mahalia na kuchangia pato la Taifa ambapo hadi sasa tuna vikundi mbalimbali vikiwemo vya vya “SILC” na “SACCOS.” Kutoa Elimu kwa Watoto wetu juu ya tunu Msingi za Maisha ili kuwezesha watoto kutambua kuwa wanategemeana na watambue upendo binafsi (wajipende), upendo kwa Mungu – Upendo kwa Mama Dunia na Maskini, Laudato si.

Baada ya kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya Jubilee ngazi za Parokia, Majimbo na Kanda sasa tunaingia hatua ya kilele cha kuhitimisha Jubilei hii Kitaifa (WAWATA Taifa) tukio linalotarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 11 Septemba 2022 katika viwanja vya Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. Tukio hili pia linatarajiwa kuhudhuriwa takribani watu 60,000 wakiwemo Maaskofu, Raisi Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO), Pamoja na wajumbe wa Bodi kutoka nchi za Afrika, Umoja wa Makanisa ya Kikristo (UWAMAKDA), Mtandao wa Wanawake wa Imani Tanzania, TWIN (Tanzania Women, Interfaith Network), Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mama Anne Makinda, Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki Mama Gertrude Mongella, Wakuu wa mikoa na wilaya na WAWATA kuanzia ngazi zote yaani  Jumuiya Ndogondogo za Kikiristu, Vigango, Parokia, Dekania, Jimbo hadi Taifa kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuzingatia kwamba  kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA kwa ubatizo wake.

Rais Samia Suluhu Hassan, Mgeni Rasmi Kilele cha Jubilei ya WAWATA
Rais Samia Suluhu Hassan, Mgeni Rasmi Kilele cha Jubilei ya WAWATA

Napenda kutumia fursa hii kuwaalika waamini wote tujongee Uwanja wa Benjamin Mkapa hapo 11/09/2022 katika Misa Takatifu itakayoanza majira ya 4:00 asubuhi (saa nne kamili asubuhi ikiongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi O.F.M. Cap., wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mbali na waamini, pia tunawaalika watu wenye mapenzi mema kujumuika nasi pia kwenye matukio mengine yatakayofanyika baadaya ya Misa ambapo pia kitazinduliwa Kitabu cha historia ya WAWATA, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha WAWATA kutokana na miradi yao, burudani mbalimbali, na kuzindua kitabu cha historia yetu. Karibuni sana mjumuike nasi wana WAWATA ili kumshukuru Mungu kwa kuwezesha haya yote kufanyika. Kufanya toba kwa yale ambayo hatukufanya sawa sawa. Kuomba neema ya kusonga mbele kwa kasi zaidi

Kwa Upendo wa Kristo – Tutumikie na kuwajibika.

Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti, WAWATA Taifa.

Jubilei WAWATA
08 September 2022, 15:05