Afrika/Kati,Kard.Nzapalainga:amani itafutwe kwa gharama zozote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Dieudonné Nzapalainga, Askofu Mkuu wa Bangui, katika fursa ya kuanza mchakato wa marekebisho ya Katiba ya nchi ulioanzishwa na Rais Faustin-Archange Touadéra wa nchi hiyo amesema kuwa “Ikiwa nina ujumbe fulani, ni kulinda amani kwa gharama yoyote. Wakati hatujawahi kupata uzoefu wa vita, huwezi kupima umuhimu wa kuhifadhi amani. Lakini tulipoishi kwenye vita, tulilala kwenye nyasi, tulikunywa maji machafu na hatukuwa na chochote cha kula, hatukuweza kwenda shule, hatukuweza kutibiwa na tuliogopa kufa kama wanyama yote hayo yanapelekea kusema ni wakati wa kulinda amani”. Kwa maana hiyo, Kardinali ameendelea kusema kuwa mashauriano mapana yanaweza kuonesha bila shaka yoyote ule mwelekeo wa watu juu ya hitaji la marekebisho hayo.
Kwa hivyo, katika kuundwa kwa Kamati ya kuandaa rasimu (ya Mkataba) amesema kungehesabiwa haki ya kufuatia mchakato huo wa kura ya maoni. Kutokana na hayo, ameongeza “tunamshukuru Rais wa Jamhuri kwa imani anayoendelea kuiweka katika Kanisa Katoliki, lakini Baraza la Maaskofu wa Afrika ya Kati linakataa mwaliko wa kuwa sehemu ya Kamati yenye dhamana ya kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati”. Tarehe 14 Septemba 2022, Kamati iliyopewa dhamana ya kuandaa Mkataba mpya wa Katiba nchini huko ilichukua madaraka. Ingawa walioalikwa, yaani Baraza la Maaskofu wa Afrika ya Kati liliamua kutoshiriki katika Kamati hiyo. Katika barua iliyotumwa kwa rais wa Jamhuri hiyo, Maaskofu walieleza hata sababu ya kutoshiriki kwao.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowafikia Shirika la Habari za Kimisionari Fides linasema kwamba wanathibitisha kuwa: “Katika awamu ya sasa ya mjadala, Baraza la Maaskofu wa Afrika ya Kati (ECSC) linashangaa juu ya usahihi wa mbinu ya kutunga Katiba mpya. Baraza linaamini moyoni mwao kwamba neno hilo lilipaswa kutolewa kwanza kwa watu wa Afrika ya Kati”. Hata hivyo kamati hiyo iliundwa kwa amri ya Rais Faustin-Arcangelo Touadéra mnamo Agosti 29. Kamati hiyo ina watu 55, wanaoshtakiwa kwa kufanyia kazi sheria mpya ya msingi katika muda wa miezi mitatu ijayo. Lakini upinzani umepinga agizo la rais mbele ya Mahakama ya Katiba. Mahakama bado haijatoa uamuzi.
Kuhusiana na suala hili, Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na mapinduzi matano tangu uhuru wake mnamo mwaka 1960, na mabadiliko kadhaa katika muundo wa serikali. Sasa Baraza la maaskofu Nchini Afrika ya Kati linasema kwamba wako “katika Jamhuri ya Sita kwa Katiba nane. Kwa zaidi ya miaka 25 nchi haijajua amani. Idadi kubwa ya watu ni chini ya umri wa miaka 18. Hii ina maana kwamba zaidi ya nusu ya watu hawajawahi kujua amani”.