WAWATA Jimbo Kuu la Dar Es Salaam Jubilei ya Miaka 50 Ya Utume: Kilele 11 Septemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji” na kilele chake ni tarehe 11 Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin William Mkapa, Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. Ibada ya Misa Takatifu itaongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kama mwenyeji, ili kuwapokea na kuwakaribisha wanawake kutoka ndani na nje ya Tanzania. Msisitizo ni kwamba, hii ni Siku ya Wanawake Wakatoliki Tanzania kwa raha zao wenyewe! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi katika kumbukumbu ya Mtakatifu Monica, Mama yake Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, hapo tarehe 27 Agosti 2022, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hii pia ilikuwa ni Siku ya WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam, fursa ya kusali na watoto wao, kuwaombea Waseminari na kuwaunga mkono katika mchakato wa malezi na makuzi yao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Monica kwa Mtoto wake Augustino. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Ruwa’ichi amepembua kwa ufupi historia ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na changamoto za maisha alizokutana nazo wakati wa ujana wake.
Mtakatifu Monica, Mama yake Mtakatifu Augustino anayeadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Agosti ya kila mwaka, alibahatika kuzaliwa katika familia ya Kikristo, akarithishwa fadhila za Kikristo zinazosimikwa katika: imani, matumaini na mapendo thabiti; huruma pamoja na fadhila za kimama. Alimlilia, akamwombea na kumsindikiza kwa ushauri, usikivu mwanana, machozi na mahangaiko makubwa mwanaye mpendwa Augustino. Na kwa sala za Mtakatifu Monica, Augustino akatubu na akamwongokea Mwenyezi Mungu. Hatimaye, akabatizwa na kuanza maisha ya sala, adili na matakatifu na mwishoni akabahatika kutukuka katika maisha na utume wake kama Askofu wa mji wa Hippo, ulioko Kaskazini mwa Afrika. Alibahatika kuwa na kipaji cha akili, kilichomwezesha kufafanua imani ya Kikristo. Jimbo kuu la Dar es Salaam linawashukuru na kuwapongeza WAWATA kwa ukaribu na ujirani wao mwema; utayari wa kuwa karibu na watoto wao kwa kuwalea, kuwatunza na kuwasaidia ili wamjue, wampende, wamtumikie na kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha ya Kristo katika ulimwengu mamboleo, mwishoni waweze kufika mbinguni.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema, anaendelea kuenzi utamaduni wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wa kuwahusisha WAWATA katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee katika malezi na makuzi ya Seminari ya Bikira Maria, Visiga. WAWATA ni zawadi bora sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; ni zawadi kwa watoto, Taifa na kwa namna ya pekee Seminari Ndogo ya Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam. WAWATA wamechangia kiasi cha shilingi milioni 240 kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Seminari ya Visiga! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anawashukuru WAWATA kwa moyo wa ukarimu na upendo; majitoleo na sadaka; mshikamano na umoja wa udugu wa kibinadamu katika maisha na utume wao. Waamini watambue daima kwamba, wanalo jukumu la kulea watoto pamoja na miito yao. Kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kamwe Kanisa haliwezi kutosheka na miito, kumbe, malezi na makuzi ya miito ni dhamana endelevu na fungamani kwa watu wote wa Mungu. Amewataka WAWATA kutambua neema na baraka wanazokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha, wawe wepesi kutumia karama na mapaji mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.
WAWATA watumie muda wao kutafakari, kusali, kupembua na kupambanua; wajitambue na kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema: tunu, karama na mapaji yao. WAWATA waendelee kuwa ni wanawake kweli kwa ajili ya familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Hapa ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mtakatifu Monica awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya sala, malezi na makuzi ya watoto wao. Wachunguzi wa mambo wanasema, WAWATA, tarehe 27 Agosti 2022 wamewasha moto wa Injili, kuelekea kilele cha maisha na utume wa WAWATA, hapo tarehe 11 Septemba 2022. Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi akisaidiana na Maaskofu wasaidizi, Mapadre 40 na wanawake zaidi 25, 000 na zaidi ya asilimia 90% ya wote waliohudhuria walikuwa ni wanawake. Ushiriki wao katika sala, kwaya na majitoleo kwa hakika hakuna mfano. Kuna mwanamke aliyecharaza kinanda, hadi anasimamia, utadhani anaendesha baiskeli kilimani, zote hizi zilikuwa ni mbwembwe za WAWATA Miaka 50 ya maisha na utume wao Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Nitaonekana kuwa na “mtima nyongo” kama sitamtambua yule Mama, jina ninalihifadhi, aliyecharaza ngoma wakati wa Ibada, kama “Mzee Moris Nyunyusa enzi zake! Hapa watanielewa wahenga tu, vijana wa kizazi kipya watapita kapa! Kulikuwa na burudani ya ngoma aina ya “Mdundiko” kutoka Pwani, “Mdange” kutoka Tanga, waja leo waondoka leo, hatari kubwa pamoja na “Iringi” ya Wachaga, Wasukuma hawakubaki nyuma kama mkia wa Mbuzi nao walishiriki kuonesha tunu zao! Ila tu WAWATA kutoka Kanda maalum wamesema, watafanya vitu vyao kwa Mkapa, hapo tarehe 11 Septemba 2022. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania. Jumuiya hii ilianzishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kunako mwaka 1972 kwa lengo la kuwasaidia wanawake kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!