Tafakari Dominika ya 22 Mwaka C wa Kanisa: Kiburi Ni Kaburi la Utu; Unyenyekevu Ni Fadhila.
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 22 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Dominika hii yanatukumbusha kuwa; Unyenyekevu ni fadhila ambayo kwayo mtu hujitambua kuwa hajitoshelezi na hivyo anamhitaji binadamu mwenzake ili amsaidie kujikamilisha na zaidi sana anamhitaji Mungu aliye ukamilifu wote kwa ajili ya uzima wa milele. Basi acheni kiburi na majivuno, jivikeni unyenyekevu ndiyo njia ya kutusaidia kumtumainia Mungu naye atatutegemeza daima katika maisha haya na yajayo. Somo la kwanza ni la kitabu cha Yoshua bini Sira (YbS 3:17-20, 28-29). Yoshua Bin Sira anatuasa akisema: “Mwanangu, katika kufanikiwa kwako uendelee kuwa mnyenyekevu…utapendwa kuliko mwenye ukarimu…utapata kibali machoni pa Bwana…kwani siri zake ni kwa wanyenyekevu” (YbS 3:17-20). Kumbe somo hili latufundisha kuwa unyenyekevu upo katika kujua kuwa Mungu peke yake ni mkubwa na mwenye nguvu na ndiye ukamilifu wote. Mtu mnyenyekevu hajikuzi mbele ya wengine bali yupo tayari kuwahudumia wote wanaohitaji msaada wake ndiyo maana anasema, mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarimu. Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu.
Yoshua Bin Sira anatuasa tuachane na kiburi maana kitatuangamiza; “Mateso ya mwenye kiburi hayana matibabu, maana uovu umeota na kutia mizizi ndani yake. Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, mche wa uovu umepandika ndani yake” (YbS 3:28). Moyo wa Busara utatambua mithali na sikio sikivu ni tamaa ya Mtaalamu” (YbS 3:29). Basi tujivike unyenyekevu, tumtumainie Mungu aliye ngao na nguvu yetu naye atatuokoa na kila ovu na zaidi kutustahilisha uzima wa milele. Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (Ebr 12:18-19, 22-24). Mapokeo yanatuambia kuwa waraka huu uliandikwa na mfuasi mwaminifu wa Paulo, baada ya kifo cha Paulo, kwa ajili ya kundi la Wayahudi walioongokea Ukristo, lakini baadae kwa matatizo na madhulumu walianza kuwa na wasi wasi na imani ya kikristo na hivyo wengine walianza kukata tamaa na kurudi katika dini yao ya asili. Sehemu tunayoisoma dominika hii ya 22 mwaka C, ulikuwa ni mwaliko kwao wa kutafakari juu ya lengo ambalo Kristo anawataka watu wote walifikie, wao wameshalifikia: “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu ya mbinguni” (Ebr 12:22). Kumbe, furaha ya maisha ya mbinguni isiyo na ukomo inaanza hapa hapa duniani kama tukiwa na muunganiko na Kristo Mkombozi wetu ambaye ndiye anayetufunulia uwepo wa Mungu katikati yetu kama alivyofanya wakati ule katika hema ya kukutania chini ya mlima Sayuni/Sinai alipofanya nao Agano na kuwapa Amri zake.
Yesu Kristo ni ukamilifu wa Agano la Mungu na watu watu. Ndiyo maana somo hili linalinganisha Ufunuo wa Agano Jipya na Agano la Kale. Agano Jipya halikufanyika kwa vitisho kama lile la Kale ambapo lilitisha kiasi kwamba Waisraeli walimwambia Musa: “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi Mungu asiongee nasi, tusije tukafa” (Kut 20:19). Agano jipya limefanyika katika utii na unyenyekevu wa Bwana wetu Yesu Kristo, utii na unyenyekevu hata mauti ya Msalaba. Agano hili halikufanyika hapa duniani bali lilifanyika patakatifu mbinguni, kati ya Mungu Baba na Yesu Kristo, Mkombozi wetu; na tena sisi wakristo tumekwisha kushiriki maisha ya Kimungu na heri ya Watakatifu kwa Agano hilo. Kumbe basi nasi tusirudi kamwe yuma na kuiacha imani yetu hata tukiwa katika mahangaiko kwani ndiyo ufunuo kamili wa Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, njia ya kwenda mbinguni kwa Mungu Baba.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 14:1, 7-14); imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatufundisha kwamba tukitaka kuufaidi ufalme wa Mungu lazima tuwe wanyofu, wanyenyekevu na tutegemee msaada wa Mungu. Kristo anatuasa tusijikweze ili tusijedhiliwa, bali tuwe wanyenyekevu ili katika unyenyekevu wetu tuweze kukwezwa. Na sehemu ya pili inatuambia kuwa mapendo ya kweli ni kuwasaidia wale ambao hawawezi kutulipa kitu chochote. Tukifanya wema kwa maskini, vilema, viwete na vipofu ambao hawana uwezo wa kutulipa tunakuwa na heri ya kulipwa katika ufufuo wa wenye haki, yaani kuuridhi ufalme wa mbinguni. Basi tujitahidi kukua katika fadhila ya udogo na unyenyekevu, ili itusaidie kutambua hali yetu ya dhambi, umaskini wetu wa kiroho, uhitaji wetu wa wengine, unyonge wetu, madhaifu na mapungufu yetu, kutokuwa na mastahili kwa kile tulicho na tunachopokea na kwamba hatustahili hata kushiriki Karamu ya Ufalme wa Mungu lakini Mungu kwa upendo na huruma yake kwa kuangalia unyenyekevu wetu anatustahilisha kuupoke uzima wa milele. Basi tujifunze fadhila hii ya unyenyekevu. Unyeyekevu ni fadhila na fadhila ni kuwa na mazoea na mwelekeo thabiti wa kufanya mema.
Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema; “Fadhila ni tabia ya kudumu ya akili, dhamira au vionjo ambayo kwayo mtu aweza kutenda analotakiwa kimaadili katika nafasi fulani, au kutenda kwa njia sahihi, yaani akiwa na msukuma wa kufaa”. Hivyo fadhila hutusaidia kutenda mema kwa wepesi, kwa urahisi, kwa kudumu na kwa furaha. Kuwa mwenye fadhila humaanisha kujisahau mwenyewe kwa ajili ya upendo wa Mungu unaojimimina kwetu. Ni kuiga upendo wa Kristo, kujikana nafsi kabisa na kuwa mwanga wa upendo kwa Mungu na jirani. Mtume Paulo anapowaandikia Wafilipi anasema; “Ndugu zangu jazeni fikira zenu kwa mambo mema na yanayostahili kusifiwa, mambo ya kweli, bora, haki, safi, ya kupendeza na ya heshima” (Wafil. 4:8). Ili kudumu kuwa mkristu mwema lazima kuamua kwa makusudi kujijengea mazoea yanayoendana na imani. Mazoea hujenga tabia, mazoea yanayotokana na kurudiarudia hali, mwenendo au matendo safi na maadilifu. Mazoea yanayoendana na Injili huitwa fadhila. Kama fadhila zingine zilivyo, unyenyekevu unajengwa kwa matendo mema madogo madogo ya kila siku pasipokutegemea sifa na mtu yuko tayari kukosolewa anapokosea na kujirekebisha, mtu huyu daima anajitafakari kila mara juu ya udhaifu wake, anajikosoa na kujirekebisha na pia yuko tayari kusifia mafanikio ya wengine wala hajikwezi daima. Kumbe unyenyekevu ni mama wa fadhila zote, humfanya mtu kuwaheshimu wengine na kumtegemea Mungu. Unyenyekevu unampatia mtu kibali cha kuonekana wa maana na wa muhimu na hivyo kupewa sifa na majukumu zaidi. Ni katika namna hii Yesu anasema; “kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Lk 14:11).
Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi. Kiburi ni kupenda makuu, kuwa na dharau, kujiona bora kuliko wengine, kupenda ufahari na mtu kutaka kujimwambafai. Mwenye kiburi hujikweza hata kwa sifa asizokuwa nazo na kuwadharau wengine, ana majivuno kuwa yeye ni bora kuliko wengine wote. Mwenye kiburi hayuko tayari kuwa chini ya Mungu au kuwa chini ya wenye mamlaka halali au wale wanaotawala na kuongoza kwa niaba ya Mungu katika mambo muhimu na halali (Rum 1:29-32). Yakobo anasema; “Mwenye kiburi humpinga Mungu na Mungu anampinga mwenye kiburi na ukipingana na Mungu lazima uumie tu” (Yak 4:6). Mwenye kiburi daima anajiona mkamilifu mbele za watu na mbele za Mungu kama Mfarisayo aliyeenda hekaluni kusali (Lk 18:11-12). Tukumbuke daima kuwa, kiburi ni mzizi mkuu wa dhambi, kwani mwenye kiburi ukaidi haumuachi salama. Mwenye kiburi hawathamini wengine, mwenye kiburi hamtegemei Mungu, mwenye kiburi hujiona anajua yote, yeye ndiye kipimo cha ukweli, hivyo hawezi kutii sheria yoyote. Jamii yenye kiburi, inajiona kuwa inajitosheleza katika yote, inamwondoa Mungu kuwa ndiye chanzo cha ukweli hasa kuhusu maadili, inajifanya yenyewe ndiyo chanzo na kipimo cha maadili, inamwondoa Mungu kuwa ndiye lengo la maisha.
Jamii yenye kiburi haitambui kwamba furaha tunayoihitaji kama binadamu itakamilishwa kwa kumwona Mungu, kwa kuwa watu wake daima wanaitafuta furaha ndani mwao, kwa ajili ya hiyo watu wake hawawezi kutenda mema kwa sababu jamii imeondoa chanzo cha mema. Jamii ya namna hii haiwezi kuwa na furaha watu wake daima wanaishi katika kilindi cha huzuni. Ndiyo maana Mtakatifu Augustino baada ya kuikosa furaha ya kweli katika viumbe alimwongokea Mungu na kusema; “Ee Mungu umetuumba kwa ajili yako na roho zetu hazitatulia kamwe mpaka pale zitakapotulia ndani mwako.” Daima tuzingatie ushauri huu wa Yoshua bin Sira: “Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, mche wa uovu umepandika ndani yake” (YbS 3:28). Kushindwa kwa wengi katika maisha na hata kile walicho kadiri ya wito na nafasi zao hutokana na kiburi. Mshahara wa kiburi ni anguko lako mwenyewe. Kumbe nisichoke kuiomba hekima ya Mungu kila siku ili iniongoze katika busara. Na “moyo wa busara utatambua mithali, na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu” (YbS 3:29). Unyenyekevu utatuinua pale tunapojishusha pasipo shuruti kwani Yesu anasema; “Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Lk 14:11). Basi tumwombe Mungu atajalie fadhila ya unyenyekevu ili kwayo tuweze kutambua ukuu wake na kumtegemea yeye.