Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fadhila ya unyenyejevu isaidie kuboresha mahusiano kati ya mwamini na Mungu pamoja na jirani. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Fadhila ya unyenyejevu isaidie kuboresha mahusiano kati ya mwamini na Mungu pamoja na jirani. 

Tafakari Dominika 22 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu Ujenge Mahusiano na Mungu na Jirani

Neno la Mungu katika dominika hii linaita tuwe wanyenyekevu. Unyenyekevu ni fadhila inayotufanya tuishi vema katika jamii, unyenyekevu ni fadhila inayotufanya tukubalike mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwekeza katika fadhila ya unyenyekevu hasa pale wanapofanikiwa kimaisha na kamwe wasithubutu kumweka Mungu pembeni.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Juma hili tunaadhimisha dominika ya 22 ya mwaka C wa Kanisa.  Neno la Mungu katika dominika hii linaita tuwe wanyenyekevu. Unyenyekevu ni fadhila inayotufanya tuishi vema katika jamii, unyenyekevu ni fadhila inayotufanya tukubalike mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu. UFAFANUZI WA MASOMO: Fadhila hii ya unyenyekevu inapata msisitizo wa pekee na wa moja kwa moja katika somo la kwanza na somo la Injili. Katika somo la kwanza (Ybs 3:17-20, 28-29), tunayasikia maneno ya hekima kutoka kwa Yoshua bin Sira. Yeye anasema “mwanangu, endelea kuwa mnyenyekevu hata unapofanikiwa kimaisha.” Na anaongeza “kadiri unavyopanda juu – kielimu, cheo, madaraka n.k., zidi kujinyenyekesha.” Hekima hii ambayo tunaweza kusema ni ya kawaida kabisa inagusa kipengele muhimu sana kuhusu unyenyekevu. Kwamba anaweza mtu kuwa mnyenyekevu wakati wa kutafuta, wakati hana kitu na akishapata kile alichokuwa anakitafuta, waswahili wanasema “anavimba kichwa” au “anapandisha mabega.” Hasikii cha mtu wala hamwoni yeyote isipokuwa yeye tu. Sasa huo ndio wakati dhaifu kwa mtu kuanguka, wakati wa mafanikio. Na huo ndio wakati ambapo hekima ya Yoshua bin Sira inatutaka kuichuchumalia fadhila ya unyenyekevu ili kudumisha mahusiano mazuri na watu katika jamii.

Unyenyekevu uboreshe mahusiano na: Mungu pamoja na jirani.
Unyenyekevu uboreshe mahusiano na: Mungu pamoja na jirani.

Somo la Injili (Lk 14:1,7-14), lenyewe linaenda mbele kidogo na kutuonesha unyenyekevu si tu katika mahusiano ya mtu na mtu bali pia katika mahusiano ya mtu na Mungu. Yesu  kupitia katika mfano wa wageni na mwenye sherehe, anatoa fundisho juu ya namna mgeni anavyopaswa kuchagua nafasi ya kuketi na namna mwenye sherehe anavypaswa kuchagua watu wa kuwaalika. Kwa mgeni Yesu anasema asijichagulie viti vya mbele na kwa mwenye sherehe anasema asialike watu anaojua na wao wakifanya sherehe watamwalika. Kuuelewa mfano huu wa Yesu inabidi tukumbuke kuwa katika Uyahudi, sherehe na chakula cha pamoja halikuwa tukio la kijamii pekee, tukio la kula, kunywa na kufurahi. Lilikuwa pia ni ibada. Kupitia mlo wa pamoja urafiki na undugu viliimarishwa na pia watu walimtukuza Mungu kwa maana katika sherehe kama hizo haukukosekana wakati wa kusali, kumtolea Mungu shukrani, sifa, utukufu n.k. Sasa katika tukio hilo ambalo linamuunganisha Mungu na mwanadamu, mtu anayekwenda kuchagua nafasi ya mbele ni mtu ambaye anajihesabia haki mbele ya Mungu na ni mtu anayejiona bora kuliko wengine. Kumbe, Yesu anaposema ukialikwa chukua kwanza nafasi ya nyuma anamaanisha kusema kuwa mwache Mungu ndiye akuhesabie haki na waache watu wakupe sifa unayostahili kati yao, usijitwalie wewe wala kujipa nafasi isiyo yako. Hayo ni majivuno. Kwa yule anayefanya sherehe, yule anayealika wageni, fundisho ni lile lile. Asijitafutie faida yake mwenyewe katika tukio ambalo mhusika mkuu ni Mungu mwenyewe.

Kiburi ni kaburi la utu na heshima ya binadamu; unyenyekevu ni fadhila.
Kiburi ni kaburi la utu na heshima ya binadamu; unyenyekevu ni fadhila.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kuzungumza juu ya unyenyekevu na hasa zaidi kuupokea kama fadhila katika dunia ya leo ni changamoto kubwa. Ni changamoto kubwa kwa sababu karibu kila kona kanuni inayoonekana kuongoza maisha ni ile ya kupambana, vijana wangesema “kukomaa”, kanuni ya “ukilemaa hupati kitu”. Sasa vitu hivi vyote ambavyo kimsingi vinafundisha ukakamavu, bidii na maarifa kwa baadhi vinautafsiri unyenyekevu kama udhaifu. Neno la Mungu leo linakuja kutukumbusha kuwa unyenyekevu si udhaifu; sio udhaifu bali ni kinyume chake. Ni kinyume cha udhaifu kwa sababu aliye dhaifu hawezi kuwa mnyenyekevu. Unyenyekevu ni fadhila. Kuna haja ya kuwa mkakamavu, kuna haja ya kutetea haki, kuna haja ya kupaza sauti n.k lakini yote hayo kama hayafanyiki kwa unyenyekevu kuna hatari ya kuleta matokeo kinyume na yale yanayotarajiwa. Ninakualika ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kuingia katika tafakari hii kuhusu unyenyekevu na kuona namna unavyoweza kuboresha mahusiano yako na watu pamoja na kuboresha mahusiano yako na Mungu kwa kuikumbatia fadhila hii ya unyenyekevu. Yesu mwenyewe amejitambulisha kwetu kuwa ni “Mpole na mnyenyekevu wa moyo.” Yeye mwenyewe atuongoze na atusaidie kuifanya mioyo yetu ifanane na Moyo wake Mtakatifu, moyo mpole na mnyenyekevu.

Liturujia D22
26 August 2022, 09:01