Tafakari Dominika ya 21 ya Kipindi Cha Mwaka C: Ufalme wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa Sakramenti ya ubatizo ni mlango wa Sakramenti zote na ni ya kwanza kati ya sakramenti tatu za kutuingiza katika ukristo – ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Ubatizo zaidi ya kutuingiza katika ukristo, unatufanya washiriki katika taifa teule la Mungu. Lakini kule kuwa mkristo au taifa teule la Mungu sio kibali cha kuingia mbinguni na kuurithi uzima wa milele. Tusipouishi ukristo wetu vizuri, tusipozishika amri na maagizo ya Mungu hatutaingia kamwe katika ufalme wake hata kama tumebatizwa na kuwa Taifa lake teule. Ushuhuda wa imani kwa maneno na matendo yetu ndiyo yatakayotustahilisha kuingia katika ufalme wa milele mbinguni. Katika somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 66:18-21); Mungu kupitia kinywa cha Nabii anawafariji na kuwatuliza Waisraeli waliorudi toka utumwani Babeli akiwaambia kuwa siku za mbele utukufu wake utahubiriwa kwa mataifa yote. Ilikuwa ni katika kipindi hiki manabii wa taifa la Israeli walianza kutambua kuwa Mungu ni Mungu wa watu na mataifa yote. Kule wao kuteuliwa kuwa taifa teule la Mungu sio kwa sababu ya ubora wao bali ni upendeleo tu aliowapa Mungu.
Utabiri huo umetimia katika Agano Jipya kwa njia ya Yesu Kristo kama maandiko yasemavyo; “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana” (Gal 4:4-5). Yohane anasisitiza akisema; “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo” (Yn 1:17). Naye Yesu anathibilisha akisema; “Mimi ndimi njia, ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yn 14:6). Kumbe tukiishi kadiri ya mafundisho yake Yesu tunastahilishwa kushiriki uzima wa milele. Somo la pili kutoka Waraka kwa Waebrania (Ebr 12:5-7, 11-13); linatukumbusha kuwa kuishi daima katika imani, kama anavyotaka Mungu, ni wajibu wa kila mkristo. Hata tukipata mateso, tusikate tamaa kwani madhulumu na mateso ni malezi ya Mungu Baba kwetu sisi wanae. Tukumbuke wosia huu; “Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye; maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi. Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa si kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani”. Basi na tuyavumilie mateso na mahangaiko ya kimaisha katika kuishuhudia imani yetu ili tupate kibali machoni pa Mungu na kushirikishwa uzima wa milele.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 13:22-30); inatufundisha kuwa si juu yetu kujua ni wangapi watakaokoka, bali ni juu yetu kufanya juhudi ili tuokoke. Sisi tuliohubiriwa Injili baada ya Wayahudi kuikataa, tusipookoka ni kosa letu kwa kutojitayarisha vema hapa duniani kupata ukamilifu wa wokovu mbinguni. Kumbe kusikiliza mahubiri na mafundisho ya Kanisa, kushiriki sadaka ya Misa Takatifu na kupokea Ekaristi Takatifu yaani kula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake Kristo hakutoshi kwa ajili ya kuurithi ufalme wa mbinguni. Watakaoingia mbinguni ni wale walioishi amri ya mapendo, waliofanya yale aliyoamuru Yesu Kristo. Nasi tujitahidi kufanya hivyo ili tupate kustahilishwa kuingia katika uzima wa milele. Kumbe tunakumbushwa kuwa kule kubatizwa na kuwa wana wa Mungu, wateule wa Taifa lake sio tiketi ya kuingia mbingu bali kule kujibidisha kuishi karidi ya ame ina maagizo yake. Itakumbukwa kuwa katika upendo wake, Mwenyezi Mungu alilichagua taifa la Israeli, kama maandalizi ya kumpokea Masiha na kuyaongoza mataifa mengine yapate kumpokea. Lakini kwa majivuno na kiburi, Wayahudi walifikiri kuwa kule Mungu kuwachagua ni kwa sababu wao ni bora zaidi ndio maana Mungu amewachagua na wengine wote wasio Wayahudi, wamelaanifu na hivyo wataangamizwa milele.
Lakini waliamini na kufundisha kuwa wasiokuwa Wayahudi walikuwa na nafasi ya kuokolewa kwa kuongokea dini ya Uyahudi. Mafarisayo, walienda mbali zaidi hata kusema kuwa; ni Wayahudi Mafarisayo ndio waliokuwa na uhakika wa kuokolewa, wengine walikuwa ni bahati tu kuokoka, kwani walikuwa hawazishiki sheria za Musa kama wao ndio maana waliweza kusema; “Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa” (Yn 7:49). Kumbe ni katika uelewa huu, katika Injili ya dominika hii ya 21 mwaka C mtu mmoja anamwuliza Yesu: “Hivi ni kweli kwamba ni watu wachache tu watakao-okolewa?” Yesu akatoa jibu kuwa kule kuwa Farisayo, au Mwisraeli, siyo kigezo cha kuokoka. Kule kubatizwa, kuwa kiongozi wa Kanisa; Papa, Askofu, Padre au Mtawa au Katekista au Baba – Mama katika siyo tiketi ya mbinguni. Kinachompeleka mtu mbinguni ni kutambua Mapenzi ya Mungu maishani, kuyatekeleza na kufanya toba ya kweli kwa dhambi zetu. Maneno ya Kristo kuwa; “watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu” ni mwangwi wa utabiri wa Nabii Isaya katika somo la kwanza aliposema; “wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu, nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, wauhubiri utukufu wangu”.
Utabiri huu unaweka wazi kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, sote tunaitwa kuwa watakatifu, sote tunaitwa kushiriki furaha ya uzima wa milele lakini ni lazima kuzishika na kuziishi amri na maagizo ya Mungu. Bila kuishi Maisha ya kumtukuza na kumsifu Mungu, bila kuwa na muunganiko na Mungu wetu aliyemtakatifu hatuwezi kuuona utukufu wake katika Maisha yajayo. Na huku ndiko kuingia katika mlango ulio mwembamba kuishi kadiri ya amri na maagizo ya Mungu. Kumbe, katika kuurithi ufalme wa mbinguni haitoshi kuwa mingoni mwa Taifa teule la Israeli, kama walivyoamini wayahudi. Hata kwetu sisi kubatizwa na kuitwa wakristo haitoshi kuuridhi ufalme wa mbinguni yatupasa kuiishi Imani yetu, kuwa kweli mashahidi wa Kristo kwa watu wote. Ushuhuda wa kiimani sio jambo rahisi yahitaji kujitoa sadaka kuvumilia mateso ndiyo maana Yesu anasema; “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze”. Kuna uwezekano kuwa tumebatizwa, tunaitwa wakristo lakini hatuuishi ukristo wetu, hivyo tusije kushangaa siku ya mwisho wa Maisha yetu Bwana atakapomtuma mjumbe wake kutuita kila mmoja kwa mda na nafasi yake yakasikika maneno haya; “siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno”.
Ni wazi Ubatizo ni mlango wa Sakramenti zingine zote, ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika sakramenti hii. Lakini licha ya haya yote, bado tuna wajibu wa kuishi kweli kama Watoto wa Mungu, tuna wajibu wa kuishi kama watoto wa Kanisa. Na wakati mwingine tunapaswa kwenye kinyume na fikra za kiulimwengu huu, kuishi kinyume na mtazamo wa wana wa ulimwengu huu, kujinyima kwa ajili ya wengine, kuachana na tamaa za kidunia na kuyakaza macho yetu kuelekea mbinguni. Huu ni mlango mwembamba. Basi tumwombe Mungu atujalie neema na baraka zake tuwe kweli Watoto wake, tuuishi kweli ukristo wetu, ili mwisho wa siku ukifika tuweze kuokolewa na kuingia katika ufalme wa uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.