Tafakari Dominika 21 Mwaka C wa Kanisa: Wokovu Ni Roho ya Mtu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa, Neno la Mungu linazungumza juu ya wokovu. Neno hili linatuonesha kuwa wokovu ni mwaliko Mungu anaoutoa kwa watu wote na hapo hapo ni mwaliko unaomhusu mtu mmoja mmoja. Mungu haokoi kundi, anaokoa nafsi moja moja. UFAFANUZI WA MASOMO: Katika somo la kwanza (Is 66:18b-21), Mungu analitangazia taifa la Israeli mpango wake wa wokovu kwa watu wote. Kwa kinywa cha Nabii Isaya Mungu anasema “wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu.” Isaya anatoa unabii huu katika kipindi ambacho Israeli imerudi nchini kwake kutoka utumwa wa Babeli na kazi inayoiona mbele yake ni kulijenga upya taifa. Ni kipindi ambacho Israeli inazidi kujitambua kama taifa teule la Mungu. Kitendo chenyewe cha Mungu kuwatoa utumwani walikitafsiri kama ndio wokovu wenyewe. Sasa kilichotokea ni kwamba Israeli ilizidi kujifungia, haikuruhusu mchanganyiko wala mwingiliano na watu wengine. Ni wao tu ndio walijiona watu wa Mungu mataifa mengine wakiwa wapagani.
Mungu anapotangaza mpango wake wa kuwakomboa watu wa mataifa yote, anawakumbusha mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza ni kuwa wao kama taifa teule waliitwa ili wawe mlango wa mataifa yote kumjua Mungu na kuupata wokovu. Na jambo la pili ni kuwa wao hawataokolewa kwa sababu tu ni waisraeli bali wao pamoja na mataifa mengine, wataokolewa kama wataifungua mioyo yao kulipokea Neno la Mungu. Tukiingia katika somo la pili tunakutana na lugha ya kinyumbani. Ni lugha ya kinyumbani kwa maana inazungumzia malezi ambayo baba humpa mwanae wa kuzaa. Waraka kwa Waebrania (Ebr 12:5-7, 11-13) unachukua mfano huo, mfano wa baba ambaye ili kumlea vizuri mwanae kuna wakati humkemea na hata humuadhibu. Sasa katika muktadha wa dhamira yetu ya leo, dhamira ya wokovu, somo hili linakuja kutuonesha kwamba ni Mungu anayeongoza watu wake katika njia ya wokovu kama vile baba anavyomwongoza mwanae katika njia ya malezi. Mungu hutuonya kwa Neno lake na kwa kupitia makosa yetu hutuadhibu. Yeye anayetilia maanani maonyo na kupokea fundisho la adhabu yu katika njia salama.
Katika somo la Injili (Lk 13:22-30) tunasikia mtu mmoja anamuuliza Yesu: “Je watu watakaookolewa ni wachache”? Ni swali kuhusu takwimu, swali linalotaka kupima wokovu kwa asilimia ili kama mwanadamu alivyozoea kupima uhalisia wa jambo kwa kuangalia takwimu basi aweze kuona uhalisia wa wokovu uko namna gani. Jibu la Yesu linakuja kumhamisha kutoka katika namna hii ya kufikiri. Ni kama Yesu anamwambia, “wokovu hauendewi kwa takwimu” bali “wewe jitahidi kuingia katika mlango ulio mwembamba”. Ni hapa Yesu anasisitiza kwamba wokovu ni suala binafsi na kwamba Mungu anaokoa nafsi moja moja, haokoi kundi. Tunaishi katika jamii, tunaishuhudia na kuiadhimisha imani katika jumuiya pamoja na waamini wenzetu. Hayo yote yana lengo la kumsaidia mtu mwenyewe binafsi kuupokea wokovu yeye kama yeye. Tunaporudi katika swali hilo kwamba watakaookolewa ni wengi au ni wachache, Yesu anavyojibu anamwonesha muuliza swali kuwa wanaookolewa wawe ni wengi au wawe ni wachache, kama wewe haumo kati yao, idadi yao haitakusaidia chochote. Wewe jitahidi, fanya bidii uupokee mwaliko wa wokovu kwani mlango wake ni mwembamba kuruhusu kuingia mtu mmoja mmoja.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika masomo haya ambayo Kanisa limetupatia kwa dominika hii ya 21 ya mwaka C, ninaona kuna msisitizo mkubwa sana juu ya umuhimu wa kuzingatia wajibu binafsi katika kuifuata njia ya wokovu. Ninaona hivyo kwa sababu kuwa kuna wakati ambapo maisha yetu ya imani yanamezwa mno na kundi: kundi la marafiki, kundi la wafanyakazi wenzangu, kundi la wafanyabiashara wenzangu, wanasiasa, majirani n.k. Hao wakienda na mimi naenda; wasipoenda na mimi siendi. Sasa kama kundi hili linamsaidia mtu kuikuza imani na kuishika njia ya wokovu ni bahati nzuri. Vinginevyo ipo hatari kubwa ya kupotea. Ni muhimu kutambua kuwa imani inatusaidia kuona uhusiano binafsi ambao Mungu anao kwa kila mmoja wetu. Imani inakuonesha kuwa Mungu anakutambua wewe kama wewe na anakuita kwa jina lako (rejea Isaya 45:4). Sasa ni muhimu kuukuza huo uhusiano binafsi na Mungu ili kuufikia wokovu ambao Mungu amekuandalia. Msemo wa lugha ya Kiswahili unaosema “kukaa ndani ya maji sio kutakata” unaweza kutusaidia kuupokea ujumbe wa dominika ya leo na kutambua umuhimu wa juhudi binafsi katika kuiendea njia ya wokovu.