Tafuta

Moto ni kiashiria cha mateso, utakaso na wokovu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Moto ni kiashiria cha mateso, utakaso na wokovu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika Ya 20 ya Mwaka C: Moto: Kiashiria Cha Mateso na Utakaso wa Dhambi Kwa Waamini

Tafakari inaonesha wazi kuwa utayari wa kuishi imani na kumfuasa Kristo ni utayari wa kupokea “moto” katika maisha ya mfuasi. Moto ni ishara ya mateso na utakaso kwa wote wanaoishi imani ya kweli. Ujumbe wa Papa Pio XII ni wa faraja kwa wanaoteseka “Jumuiya aliyoianzisha Kristo (yaani Kanisa) haiwezi kushindwa, kwani inachota nguvu zake kutoka kwa Mungu, si kutoka kwa watu.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli, Napoli, Italia

Baba Mtakatifu Pio XII katika Waraka wake wa Kitume “Meminisse Iuvat” (yaani “Inasaidia kukumbuka”) inayohusu “Sala kwa Kanisa Linaloteswa” ya Julai 14, 1958 anasema, “Jumuiya ambayo Kristo aliianzisha inaweza kusambuliwa, lakini haiwezi kushindwa, kwani inachota nguvu zake kutoka kwa Mungu, si kutoka kwa mwanadamu. Hata hivyo, hakuna shaka kwamba itadhihakiwa kwa karne na karne kwa njia ya madhulumu, migongano na minong’ono kama ilivyokuwa zamani hatima ya Mwanzilishi wake- kwa kuwa alisema, “Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi.’ Lakini ni hakika vile vile kwamba, kama vile Kristo Mkombozi wetu alivyoinuka kwa ushindi, vivyo hivyo Kanisa siku moja litapata ushindi wa amani juu ya adui zake wote” (namba 24). Sehemu hii ya maneno ya Papa Pio XII inakazia uhalisia na utimilifu wa kile ambacho kinaelezwa katika masomo yetu ya Dominika ya 20 ya Mwaka C wa Kanisa ambayo yanaonesha wazi kuwa utayari wa kuishi imani na kumfuasa Kristo ni utayari wa kupokea “moto” katika maisha ya mfuasi. Moto ni ishara ya mateso na utakaso kwa wote wanaoishi imani ya kweli. Hata hivyo ujumbe wa Papa Pio XII ni ujumbe wa faraja kwa waamini wanaoteseka kwa sababu ya imani kwani anasema wazi kuwa “Jumuiya aliyoianzisha Kristo (yaani Kanisa) haiwezi kushindwa, kwani inachota nguvu zake kutoka kwa Mungu, si kutoka kwa mwanadamu.”  Tuanze kutazama ufafanuzi wa masomo yetu.

Yesu amekuja kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo.
Yesu amekuja kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo.

SOMO LA KWANZA: Yer. 38:4-6, 8-10: Somo letu la kwanza linatufundisha kuwa “kuwa nabii kuna gharama zake- ndiko kupokea moto anaouzungumzia Kristo katika Injili.” Nabii Yeremia alifanya utume wake kipindi ambacho Waisraeli walikuwa hawajachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Maisha ya Waisraeli kabla ya kupelekwa uhamishoni Babeli yalitawaliwa na maovu mengi: walimwacha Mungu wa kweli na kuigeukia miungu mingine, wanyonge walinyimwa haki zao, rushwa ilitawala katika mahakama zao, walitegemea nguvu za kijeshi toka mataifa mengine badala ya kujiaminisha kwa Mungu na mengineyo kama hayo. Kutokana na maovu haya nabii Yeremia anatoa unabii kuwa taifa la Israeli lazima liadhibiwe na Mungu. Adhabu kwa taifa la Israeli ni kuvamiwa na taifa la kigeni (Babeli), kisha mji wao wa Yerusalemu kutekwa na watu wake kuchukuliwa uhamishoni Babeli. Yeremia anasema wazi kuwa uvamizi huo hauepukiki na ya kwamba Waisraeli watashindwa watakapojaribu kuzuia uvamizi huo, hivyo ni bora wasalimu amri. Habari hii ya Yeremia haipendezi masikioni mwa wakuu wa taifa la Israeli ambao wanautazama utabiri huu wa Yeremia kama “kuwakatisha tamaa Waisraeli katika mipango yao ya kuzuia uvamizi wa taifa la Babeli.” Unabii huo unasababisha wakuu wa taifa la Israeli kutaka kumwangamiza nabii Yeremia kwa kumtupa kwenye shimo lenye matope ili afie humo kwa njaa kali- Yeremia anapokea “moto”. Haya yote yanampata kwa sababu tu anasema ukweli kuwa taifa la Israeli litashindwa katika vita dhidi ya taifa la Babeli kwa sababu ni njia ambayo Mungu analiadhibu taifa la Israeli kutokana na dhambi zake. Mateso anayopata Yeremia yanadhihirisha kuwa “kuwa nabii kuna gharama zake.”

Somo letu la kwanza linatufundisha kuwa “kusimamia/kusema ukweli kuna gharama.” Yeremia anapatwa na masaibu yote haya kwa kuwa tu amesema ukweli kuwa taifa la Israeli litashindwa katika vita kama adhabu ya Mungu kutokana na maovu wanayotenda. Katika jamii yetu watu wengi wanapenda kusikia tu habari zinazowafurahisha wao- hawataki kusikia/kuambiwa ukweli. Wengi wetu wanapenda kusikia tu habari za mafanikio katika maisha (Injili ya mafanikio): hawataki kuambiwa mapungufu/maovu yao. Kwa bahati mbaya hata wale wanaosimamia ukweli wanapata taabu sana na kutazamwa kuwa ni maadui kama nabii Yeremia katika somo letu la leo. Daima wasema ukweli hupata taaba sana: kunafanyika majaribio ya kuwaua (na hata kuwaua kabisa), wanapokea vitisho, wanachukiwa, wanazushiwa skendo za uzushi na mengineyo. Kwa kweli wanatupiwa moto mkali. Hata hivyo tunapaswa kutambua kuwa sisi sote ni manabii kama Yeremia na hivyo hatuna budi kupitia magumu katika jukumu letu la kusema, kutetea na kuishi ukweli/imani yetu. Tutambue kuwa siyo kila mtu atafurahishwa na ukweli tunaosema na kuutetea. Hivi ni mara ngapi tumechukiwa hata na ndugu zetu kwa sababu ya kusema ukweli? Ni mara ngapi watu wanauawa kwa sababu ya kusema na kusimamia ukweli? Mara ngapi watu wanafungwa jela na kunyimwa uhuru wao kwa sababu ya kusema ukweli? Ni Mapadre/Watawa/Walei wanapitia magumu katika kuishi utume wao wa kinabii? Je, hao wanaopatwa na masaibu hayo si akina Yeremia wa zama zetu? Tuwe tayari kusema ukweli hata kama tutachukiwa, tutadhulumiwa au kuuawa kwani mwisho tutapata ushindi.

Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa haki, amani na mapendo
Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa haki, amani na mapendo

SOMO LA PILI: Ebr. 12:1-4 Somo letu la pili linatufunulia kuwa “imani ni pamoja na kuvumilia mateso ambayo kwayo tunapata utukufu.” Wakristo wa kwanza waliteseka sana kwa sababu ya imani yao kwa Kristo- walishushiwa moto kweli kweli (moyo alioutabiri Kristo) kwa sababu ya imani hao. Hivyo mwandishi wa Waraka kwa Waebrania analenga kuwahimiza Wakristo kuvumilia mateso ili mwishoni wapate utukufu. Anawahimiza kuvumilia mateso kama Kristo alivyovumilia mateso msalabani. Mwandishi anawataka Wakristo wamwige Kristo ambaye ni chimbuko na ukamilifu wa imani yetu. Lakini pia mwandishi anawafunulia Wakristo kuwa kuna mashahidi wengi sana wanaowazunguka. Mashahidi hawa ni akina nani? Hawa ni wale waliokuwa tayari kuteseka na kufa kwa ajili ya imani yao kwa Kristo ambao kwa sasa wako mbinguni. Hawa wanaendelea kuwatia moyo Wakristo walio hai ili waweze kuvumilia mateso kwa ajili ya utukufu ujao. Hawa waliopo mbinguni walitakaswa kwa moto wa mateso ya hapa duniani.

Kupitia somo letu la pili tunajifunza kuwa “uvumilivu katika mateso hutuwezesha kupata utukufu.” Kristo ni kielelezo cha ukweli huu: Kristo alivumilia mateso ya msalaba na mwisho akapata tuzo la kuketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu (kuketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu kunamaanisha kutawala pamoja na Mungu). Tuzo hili kwa Kristo halikuja kirahisi wala bure bure bali kwa utayari wake wa kuvumilia mateso. Hivyo Kristo ni mfano kwetu wa namna ya kupata utukufu. Hata sisi tukitaka kupata utukufu ni lazima tuwe tayari kupokea na kuvumilia mateso huku tukichota nguvu kwa Kristo Mwenyewe ambaye naye aliteseka na kudharauliwa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa bahati mbaya tunapoteseka (kwa magonjwa, hofu za maisha, usaliti, kuonewa, changamoto za maisha, ndoa na familia) huwa hatubaki imara katika imani: daima tunatetereka katika imani kiasi cha kutafuta kila mbinu kuondoa mateso- kukimbilia maombezi kwa wahubiri bandia, kukimbilia kwa waganga kuondoa nuksi na mikosi, kufanya matambiko na mengineyo. Namna hii ya maisha haidhihirishi imani yetu, hasa tuwapo katika mahangaiko ya dunia. Mashahidi wa imani walioko mbinguni wawe chachu kwetu katika kuishi imani kwani daima wanatuombea. Moto wa mateso ya hapa duniani ututakase.

Moto ni alama pia ya mateso, mahangaiko na msalaba katika maisha
Moto ni alama pia ya mateso, mahangaiko na msalaba katika maisha

SOMO LA INJILI: Lk. 12:49-53: Somo letu la Injili linatufundisha kuwa “kuishi Ukristo (imani yetu) kunaambatana na mateso.” Tumesikia katika Injili Yesu akisema kuwa hakuja kuleta amani duniani bali amekuja “kutupa moto duniani.” Je, Yesu ana maana gani? Moto katika Biblia unaashiria mambo mengi. Kwanza, moto unamaanisha mateso makali  (rejea Ufu. 20:10-14). Hivyo, kwa maneno mengine Yesu anasema, “Nimekuja kuleta mateso duniani” akiwa na maana kwamba Injili anayoihubiri itakuwa ni chanzo cha wafuasi wake kuteseka, yaani wale watakaoamua kumfuata Kristo na kuishi yale anayofundisha watakumbana na mateso/taabu/changamoto hapa duniani. Hivyo Yesu analenga kusema kuwa ufuasi unaambatana na mateso na hivyo wafuasi wa Kristo wasitegemee maisha rahisi yasiyo na bughuza/karaha katika kumfuata Kristo- maisha ya amani yasiyo na mahangaiko. Wafuasi wa Kristo wanapaswa kuelewa kuwa kuna nyakati za mateso (nyakati za moto) katika ufuasi wao: kuna nyakati za kutengwa na kukataliwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo, kuna nyakati za kufarakana na ndugu/jamaa/marafiki kwa sababu ya imani yao kwa Kristo, kuna nyakati za maumivu yanayotokana na uamuzi wa kuishi ukristo. Pili, neno moto linamaanisha pia nyenzo inayotumiwa kuharibu na kutakasia vitu (moto unachoma vile visivyohitajika na pia unatumika kutakasia dhahabu). Hivyo, Yesu anaposema amekuja “kutupa moto duniani” anamaanisha pia kwamba amekuja kuharibu nguvu za uovu hapa duniani ili kutakasa maisha ya wafuasi wake. Tatu, moto kwenye Biblia ni ishara ya uwepo wa Mungu, hivyo Yesu amekuja duniani kuonesha uwepo na utendaji wa Mungu ambao kamwe hakuna wa kuuzima.

Moto ni alama ya utakaso na mwanzo wa maisha mapya
Moto ni alama ya utakaso na mwanzo wa maisha mapya

Kutokana na somo letu na Injili tunafundishwa kuwa (i) Ukristo wetu utaambatana na mateso kwa ajili ya Kristo. Kuishi ukristo siyo jambo la lelemama. Ukristo una changamoto na magumu yake- ukristo ni msalaba. Tumepitia, tunapitia na tutapitia mengi katika kuishi ukristo wetu: Ni wangapi wamesalitiwa na hata kuuawa na ndugu zao wenyewe kwa sababu tu wameamua kuwa Wakristo? Ni wangapi tunateseka katika maisha kwa sababu tunalazimika kushika mafundisho msingi ya ukristo? Ni watu wangapi wanabaguliwa na kunyima uhuru kwa sababu tu ya imani yao kwa Kristo? Haya yote ni “moto” katika ufuasi wetu. Moto huu chanzo chake ni uamuzi wetu wa kumfuata Kristo. (ii) Kristo amekuja kuharibu uovu na kututakasa. Nimedokeza hapo awali kuwa kazi ya moto ni kuharibu/kuteketeza yale yasiyohitajika na kutakasa vitu. Yesu amekuja kuharibu nguvu za uovu (dhambi) na kututakasa ili tuwe safi mbele za Mungu. Moto wa Kristo unaharibu dhambi zetu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio; moto wa Kristo unatakasa maisha yetu kwa njia ya neema tunazozipata tunapokuwa na muunganiko na Kristo (neema tunapopokea Sakramenti, tunapoishi maisha ya sala, tunapokuwa na uchaji, n.k). Je, mimi na wewe tunaruhusu moto wa Kristo uharibu vilema vyetu na kututakasa? Tumwombe Mungu atujalie neema ya kupokea “moto” wa utakaso na neema ili tuzidi kuwa imara katika maisha ya ufuasi, huku tukisindikizwa na sala na maombezi ya Bikira Maria, Mama Mpendelevu sana.

11 August 2022, 17:35