Tafuta

Mateso tuyapatayo kwa kuwa tuko upande wa Mungu yanatupatia wokovu wa uzima wa milele kwani ni sawa na Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao wokovu wetu umetundikwa juu yake. Mateso tuyapatayo kwa kuwa tuko upande wa Mungu yanatupatia wokovu wa uzima wa milele kwani ni sawa na Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao wokovu wetu umetundikwa juu yake.  

Mateso Ni Shule ya Uadilifu na Utakatifu wa Maisha: Ukuu wa Fumbo la Msalaba!

Masoma ya dominika hii yanatukumbusha kuwa upande wa Mungu lazima tuwe tayari kuteseka lakini mateso tuyapatayo kwa kuwa tuko upande wa Mungu yanatupatia wokovu wa uzima wa milele kwani ni sawa na Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao wokovu wetu umetundikwa juu yake. Mateso ni shule ya uadilifu na utakatifu; ni mtihani wa imani, matumaini na mapendo thabiti.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Litrujia ya Neno la Mungu, dominika ya 20 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masoma ya dominika hii yanatukumbusha kuwa upande wa Mungu lazima tuwe tayari kuteseka lakini mateso tuyapatayo kwa kuwa tuko upande wa Mungu yanatupatia wokovu wa uzima wa milele kwani ni sawa na Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao wokovu wetu umetundikwa juu yake. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 38:4-6,8-10); linatupa simulizi la mateso aliyopata Yeremia baada ya kutumwa na Mungu kuwaeleza Wayahudi kwamba mji wa Yerusalemu utatekwa na jeshi la mfalme wa Babeli enzi za mfalme Sedekia baada ya wao kumuasi Mungu. Utabiri wa Yeremia haukupokelewa na wakuu wa Yuda. Wao walichukizwa na ukweli huo wakaamua Yeremia auawe wakimwambia mfalme, twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri bali shari. Yeremia alitupwa katika shimo la matope, akiyavumilia mateso na njaa kali, lakini Mungu alimwokoa kwa mkono wa Ebedmeleki. Na utabiri wake ulitimia kwa mji wa Yerusalemu kuangamizwa na watu wake kuchukuliwa mateka.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha

 

Ni ujumbe kwetu pia tuwe wasikivu kwa maonyo yanayotolewa na viongozi wetu wa kiimani kwani wao wanapata maono kutoka kwa Mungu na hivyo kutuonya kwa matatizo yanayoweza kutukumba sababu ya mienendo yetu mibaya. Somo la pili kutoka Waraka kwa Waebrania (Ebr 12:1-4); linatusimulia namna watakatifu walivyovumilia taabu na mateso mengi hata wakapata tuzo mbinguni na namna Yesu alivyostahimili mateso na kuvikwa taji ya ufalme na utukufu mbinguni. Uvumilivu wa watakatifu, ni mfano wa himizo katika kuzichukua taabu zetu za kila siku, tukiyatafakari mateso ya Yesu Kristo mioyoni mwetu bila kuchoka, tukipigana vita dhidi ya dhambi hata kumwagika damu yetu, ili kuufikia utukufu wa uzima wa milele. Kumbe tunakumbushwa kuwa maisha yawe ya kiroho au kimwili ni mapambano. Mafanikio yoyote katika maisha yanahitaji juhudi na bidii katika kufanya kazi na kusali ili kupata maelekezo na miongozo kutoka kwa Mungu aliye asili ya mema yote. Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 12:49-53); yatufundisha kwamba, kuwa wafuasi wa Yesu Kristo haima maana ya kuishi kwa amani na raha tu, bali ni pamoja na kuvumilia taabu na mateso ya kila siku kwa ajili ya imani iletayo wokovu. Kumbe hatuwezi kutenganisha maisha ya kikristo na msalaba, maisha ya imani na mateso. Kwa vile mateso yatokanayo na imani kwa Yesu ni kama msalaba basi yana thamani ya ukombozi katika maisha ya mkristo.

Hivyo mateso ni baraka, mateso ni furaha, mateso ni zawadi ya Kimungu na ni shule ya Utakatifu. Tukiyatafakari maisha ya watakatifu tunaonja na kutambua jinsi na namna mateso na mahangaiko katika maisha yanavyomweka binadamu karibu zaidi na Mungu muumba wake. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema; furaha ya kweli hupatikana katika mateso, kwani katika mateso mna msalaba nao msalaba ndio daraja letu la kumwona Mungu kama tukiyatambua, tukayapokea kikristo kwa moyo wa Imani na kuyabeba pamoja na Kristo na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke katika kuteseka kwetu kwani Kristo mwenyewe anasema; “mtu yeyote asiyechukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, huyo hafai kuwa mwanafunzi wangu” (Lk. 14:27). Mtakatifu Ignasi wa Antiokia anasema; “Mkristo anafananishwa zaidi na Yesu na kushiriki kikamilifu kazi yake ya ukombozi hasa anapovumilia mateso ya maisha yake kwa imani. Mateso na kifo kwa vyenyewe havina uzuri wala faida yoyote. Lakini vikipokelewa kwa imani na mkristo, vinapata kuwa visakramenti kwani vinakuwa alama ya mateso na kifo cha Yesu Kristo; na hivyo vinapata thamani tele mbele za Mungu."

Mateso ni shule maadili na utakatifu wa maisha.
Mateso ni shule maadili na utakatifu wa maisha.

Mtakatifu Ignasi alitambua kuwa kadiri mateso yanavyozidi ndivyo anavyozidi kuwa karibu na Mungu akisema; “nilipo karibu na upanga, ndipo nilipo karibu na Mungu, nilipo pamoja na wanyama wakali, ndipo nilipo pamoja na Mungu”. Ndiyo maana pale wakristo walipojaribu kumzuia asiende kuteswa, aliwafokea, akaona kama wanamzibia njia ya mbinguni. Akiwa katika minyororo alisema; “mniombee ili minyororo hii inisaidie kumpata Mungu”. Akasisitiza akisema; “kama vile kito kisivyoweza kung’arishwa bila msuguano, vivyo hivyo hakuna mtu anayeweza kufanywa mkamilifu bila kutoa machozi na hapatakuwepo na utakatifu ambao hauna alama ya muhuri wa mateso ya Yesu”. Mtakatifu Birgita wa Sweden aliyapokea mateso kwa moyo mkunjufu. Yeye daima alisali, akiwaombea watesi wake na kuwaita kuwa ni wafadhili wa mbingu. Yeye anatufundisha kuwa tunawashukuru wafadhili wa duniani wanaotupatia mali na vitu mbalimbali. Lakini tunasahau kuwashukuru wale wanaotutesa kwani kwa kututesa, tunaipata mbingu. Naye Mtakatifu Bakhita alipoambiwa anataka kuwa mtawa kwasababu ya hofu ya kuendelea kuwa mtumwa alisema: “nikikutana na wale walioniuza pamoja na aliyeninunua na kunifanya mtumwa nitapiga magoti kwa furaha na kuibusu miguu yao kwani ni kwa mateso yao nimemtambua Kristo, ni kwa msaada wao nimekuwa mkristo.”

Mtakatifu Vinsenti wa Paulo naye anasema; “inampendeza Mungu kumpatia mateso yule aliye imara katika upendo wake, hivyo kuchukua mateso na kunyamaa ni njia bora ya kujipatia fadhila na kumtukuza Mungu. Mateso ni mtihani wa Imani, ambayo kwayo twajifunza pia kutambua thamani ya wengine. Tena, ukiingizwa mwenyewe katika udhaifu wa majaribio, utawafahamu wengine vizuri zaidi”. Kumbe katika maisha ya Kikristo, Msalaba ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha na matumaini. Ni kwa sababu hii tunaona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mtakatifu Katarina wa Siena anasema: “hakuna mapendo yasiyo na mateso. Msalaba japo ni ishara ya mateso, vivyo hivyo ni ishara ya matumaini na mapendo kwetu. Linalobaki ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu msalaba kwa matumaini na mapendo ya kina kwa kuwa ndio wokovu wetu. Msalaba kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu (1Kor 1:18). Msalaba unatufunulia na kutufundisha juu ya Hekima kuu ya Mungu. Msalaba unatufundisha siri ya Mungu. Msalaba unatufunulia na unatufundisha juu ya upeo wa upendo wa Mungu kwetu. Lengo kuu la msalaba ni kutuinua sisi “juu.” Yesu anasema; “Nami nikiinuliwa juu ya nchi nitawavuta wote kwangu (Yoh 12:32). Msalaba una nguvu ya pekee ya kuwavuta watu kwa Yesu. Msalaba una nguvu ya kuwafanya watu waone ubaya wa dhambi na kifo na hivyo kuwafanya watubu. Msalaba ni mwamba salama na unafungua milango ya mbingu. Msalaba unawavuta watu kufanya toba, kutafakari, kukiri, kuungama, kufanya malipizi na kuacha dhambi (Lk 23:48).

Msalaba ni ishara na chanzo cha maisha mapya.
Msalaba ni ishara na chanzo cha maisha mapya.

Mtakatifu Andrea wa Crete anasema: “Msalaba ni utukufu wa Kristo na ushindi. Msalaba ni hazina ya uzima wa milele. Kwa jina la msalaba, juu ya msalaba, kwa njia ya msalaba na kwa sababu ya msalaba, utajiri wa ukombozi tulioupoteza tumerudishiwa. Msalaba ni mti wa uhai (Mwa 2:9; Ufu 2:7). Msalaba ni kama nyundo ivunjayo miamba (Yer 23;29). Msalaba ukikutana na moyo wa mtu ambao ni mgumu kama jiwe, unavunja vunja. Ni kama nyundo na moto. Msalaba ni upanga wa adhabu ambao unachoma adui wa Adamu na kufungua mlango ambao ulikuwa umefungwa kwa dhambi ya Adamu (Mwa 3:24). Msalaba ni gongo la kufariji (Zab 23:4). Ni fimbo ya Musa ambayo ilibadilisha maji kuwa damu na kuharibu nyoka wenye sumu (Kut 7:17; 4:2 – 4). Msalaba ni winchi la kuvutia jiwe la msingi la kujenga Kanisa. Msalaba ni daraja linalounganisha mbingu na dunia. Msalaba ni ishara ya sala (Kut 17:11). Kumbe basi, msalaba au mateso ni sehemu ya maisha ya Kikristo, hatuna budi kuupokea na kuubeba pamoja na Kristo. Tujiepushe na manabii wa uongo wanaotangaza injili ya mafanikio, injili ya kututoa katika mahangaiko kwa njia ya maombezi na miujiza ya kimafanikio bila kufanya kazi. Tukumbuke daima kuwa ujumbe ulio katika Msalaba ni ujumbe wa uhai, ukombozi, upatanisho na amani. Tutafute amani hiyo katika msalaba wa Yesu katika mioyo yetu, familia zetu, jumuiya zetu, Parokia zetu, majimbo yetu, nchi yetu na dunia kwa ujumla. Kila mtu abebe msalaba pamoja na Kristo kwani tukiubeba msalaba pamoja naye lazima tutapata ushindi. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 20 Mwaka C
12 August 2022, 10:54