Tafuta

Ujumbe wa masomo ya dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa ni kutuimarisha kiimani tunapoelekea kukata tamaa wakati wa taabu na mahangaiko. Ujumbe wa masomo ya dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa ni kutuimarisha kiimani tunapoelekea kukata tamaa wakati wa taabu na mahangaiko.  

Tafakari Dominika 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani Na Matumaini

Ujumbe wa masomo ya dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa ni kutuimarisha kiimani tunapoelekea kukata tamaa wakati wa taabu na mahangaiko. Hivyo yanatukumbusha kuwa imani ni msingi na chanzo cha matumaini ya kweli na mwanzo wa uzima wa milele kwani hutujalia kuonja furaha na mwanga wa heri ya mbinguni wakati tungali hapa duniani tukihangaika. Imani thabiti!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kutuimarisha kiimani tunapoelekea kukata tamaa wakati wa taabu na mahangaiko. Hivyo yanatukumbusha kuwa imani ni msingi na chanzo cha matumaini ya kweli na mwanzo wa uzima wa milele kwani hutujalia kuonja furaha na mwanga wa heri ya mbinguni wakati tungali hapa duniani tukihangaika na maisha. Somo la kwanza linatoka kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 18:6-9). Kitabu hiki kiliandikwa kwa ajili ya Wayahudi wa Diaspora –walioishi nje ya Palestina – waliokuwa wametawanyika katika himaya ya Kirumi. Lengo hasa la kuandikwa kwa kitabu hiki ni kuwakumbusha Wayahudi hususani vijana historia ya babu zao, na mambo makuu ya Mungu aliowatendea mababu zao hapo zamani ili kamwe wasimuaisi Mungu wao na kufuata imani ya miungu mingine. Kilichomsukuma mwandishi wa kitabu hiki ni mazingira walioishi ndugu zake Wayahudi nje ya Palestina wakichangamana na watu wa mataifa mengini wakiwa na dini na miungu yao na hivyo wengine walianza kuiiacha imani yao.  Kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha ya Kigiriki, ambayo ilikuwa ikizungumzwa wakati ule na Wayahudi wa Diaspora na sio lugha yao ya asili [Kiharamayo]. Kwa sababu hii Wayahudi wa Palestina na Waprotestanti walioibuka baadae, walikikataa kitabu hiki na kusema kuwa sio kitabu kitakatifu.

Hekima ya Mungu imetundikwa Msalabani.
Hekima ya Mungu imetundikwa Msalabani.

Somo la kwanza katika dominika ya 19 Mwaka C kutoka kitabu hiki cha Hekima, linawakumbusha uaminifu wa Mungu, jinsi alivyowatayarisha babu zao Waisraeli kwa safari ya ukombozi kutoka utumwani Misri, usiku ule alipowaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri na mwanzo wa Pasaka yao ya kwanza walipomla mwanakondoo waliyemchinja na Mungu kuwaweka huru kutoka utumwani. Hivyo anawaasa wasifuate na kuiga njia potofu za dhambi za watu wa mataifa. Anawakumbusha kuwa Hekima ya kweli ni kufuata Njia ya Mungu kwa uaminifu na kuzishika ahadi zake kwa maana maisha hayaishii hapa duniani kama wapagani – wadhambi wafikirivyo. Hivyo wasiionee aibu, historia yao ya zamani iliyokuwa imejaa utukufu kuliko historia ya mataifa mengine. Hekima ambayo Mungu anawapa watu wake, ni bora na kubwa kuliko hekima ya wanadamu wasomi wa duniani hii. Kumbe kama vile Waisraeli walivyokesha usiku ule kwa imani wakingoja ukombozi wao kutoka kwa Mungu, sisi nasi kwa imani tunapaswa daima kuwa tayari kwa saa ya kifo chetu na kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa utimilifu wa ukombozi wetu kama injili inavyotuambia tukeshe na tuwe tayari mda wote.

Somo la pili linatoka katika Waraka kwa Waebrania (Ebr 11:1-2,8-19). Waraka huu waliandikiwa Wayahudi walioongokea ukristo na wakalazimika kuiacha ardhi yao na kwenda kuishi kwingineko wakiwa wamezungukwa na Wayahudi wasio wakristo na Wapagani. Hawa nao waliteseka sana kwa sababu Wapagani na Wayahudi wenzao waliwatenga kwa kuwaona kuwa ni wasaliti wa imani ya kiyahudi – imani ya babu zao, kwa kuingia Ukristo. Hivyo waliukumbuka mji wao Yerusalemu na Hekalu sehemu muhimu kwa Ibada.   Kumbe somo hili linawaimarisha wakristo Waebrania waliovunjika moyo kwa sababu ya madhulumu na mateso kwa ajili ya imani yao kwa Kristo mfufuka likiwaasa wawe na imani kwa uzima wa milele kama aliyowaahidi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo wakifuata mfano wa babu zao Ibarahimu, Isaka na Yakobo. Kwa imani Ibrahimu alikaa ugenini katika nchi ya ahadi, katika hema pamoja na Isaka na Yakobo. Kwa imani Sara alipokea uwezo wa kuwa na mimba katika uzee wake akiwa na umri wa miaka 90, na Ibrahimu akiwa na miaka 100, (Mwa 17:17). Hivyo imani inatujalia uhakika wa mambo yajayo. Nasi tunakumbushwa kubaki waaminifu kwa Mungu wetu aliyetufunulia Yesu Kristo nasi tukaipokea kwa njia ya mitume. Imani hi indio hakika yetu ya maisha ya uzima wa milele mbinguni.

Waamini wajitahidi kukesha katika sala, Neno, Sakramenti na Matendo adili.
Waamini wajitahidi kukesha katika sala, Neno, Sakramenti na Matendo adili.

Injili kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 12:32-48), inasisitiza juu ya matunda ya kudumu katika imani tukiyavumilia mateso na mahangaiko yatokanayo na imani yetu kuwa ni kupokea tuzo ya maisha ya milele mbinguni yaani kuonana uso kwa uso na Mungu Baba. Itakumbukwa kuwa Wakristo wa kwanza mara baada ya Kristo kupaa mbinguni na ujio wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, waliamini ujio wa pili wa Yesu kuwa u-karibu sana, hivyo walimsubiri kwa shauku kubwa aje awachukue na kuwapeleka mbinguni. Mda ulizidi kupita na kwa sababu ya mateso na madhulumu, wengi walipoteza mali zao, wengine walifungwa magerezani na wengine kuuawa. Hali hii ilipelekea wengine kukata tamaa na kuona kuwa ujio wa pili wa Yesu ni fundisho la uongo la kiimani. Katika hali hii Luka anawaandikia injili yake kuwaelewesha kuhusu Mpango wa Mungu, kuimarisha imani yao kwa Kristo, na kuwatia moyo. Katika Injili tunayoisoma dominika ya 19 mwka C, Luka akiongozwa na Roho wa Mungu, anaweka pamoja misemo ya Yesu, aliyoisema sehemu mbalimbali wakati wa kuhubiri kwake ili kutoa mwongozo kwa Wakristo hawa waliokuwa na mashaka kuhusu kuchelewa kwa Yesu kuja mara ya pili. Luka anawatoa shaka akiwaambia; “Msiogope enyi kundi dogo” (Lk 12:32), licha ya madhulumu na mateso mnayopata sasa, furahini, simameni imara, msikate tamaa, maana wale wanaowatesa hawawezi kuichukua furaha yenu ya uzima wa milele kama wanavyowachukulia mali yenu kama mtasimama imara katika imani yenu.

Kumbe, masomo yote matatu yanasisitiza kusimama imara katika imani yetu. Lakini imani ni nini? Imani ni fadhila ya kimungu. Imani ni “Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1). Imani ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Imani ni ile hali ya akili ya mtu kupokea ukweli uliofunuliwa na Mungu. Imani ni mwambatano wa nafsi ya mtu kwa Mungu. Imani ni kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu ameufunua kwetu (KKK, 150). Imani ni neema ya Mungu ndani mwetu (KKK, 153). Imani ni zawadi ya Mungu, fadhila ya kimungu inayomiminwa naye mioyoni mwetu. Kumbe uhakika wa ukweli wa imani ya Kikristo ni Mungu mwenyewe anayejifunua kwetu ili tumjue, tumpende, tumtumikie, tuokolewe naye na mwisho wa yote ni kuonana naye uso kwa uso huko mbinguni aliko yeye pamoja na malaika na watakatifu wake wote. Hivyo imani haitegemei ufahamu wa akili ya kibinadamu, bali yamtegemea Mungu mwenyewe. Tuna amini ukweli wa mafumbo ya Kimungu, si kwa mamlaka ya akili zetu, bali kwa mamlaka ya Mungu anayejifunua na kutufunulia ukweli wa mafumbo hayo. Tunafahamu na kuamini kuwa yote yatokayo kwa Mungu ni kweli kwa sababu Mungu ni ukweli na uaminifu, hadanganyi, wala hadanganyiki.

Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu

Kwa kuwa Mungu ni Fumbo, na ukweli wa Kimungu ni Fumbo kama Mungu mwenyewe, fumbo hili linaeleweka na kuhakikishwa na Mungu mwenyewe, si kwa mamlaka ya akili ya kibinadamu. Lakini hata hivyo, uelewa wa kina zaidi unaleta imani kubwa zaidi. Neema ya imani inafungua “macho ya moyo” kwa ajili ya ufahamu hai wa yale yaliyo katika ufunuo. Hivi ndivyo asemavyo Mtakatifu Augustino: “Nasadiki ili kufahamu, na nafahamu ili kusadiki vizuri zaidi”. Kanisa Katoliki linaungama mafumbo makuu ya imani ambayo ni fumbo la Utatu Mtakatifu, fumbo la Ukombozi, fumbo la Yesu kujifanya Mtu (Umwilisho), fumbo la Ekaristi Takatifu, fumbo la Umama wa Bikira Maria, fumbo la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili pia fumbo la Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Haya yote yamefunuliwa na Mungu na imani tu yaelewa. Imani ina faida kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Imani inatupatia utambulisho wetu. Kubatizwa na kupokea Imani Katoliki kunatufanya watoto wa Mungu. Imani inatuunganisha na wengine na hivyo kutusaidia kujua namna ya kuhusiana na wengine na kunufaika na misaada ya sala na kijamii kutoka kwa wengine. Imani inatuweka na kutupatia njia ya uhakika ya kufika mbinguni. Imani ni namna ya maisha. Kwa hiyo, inatusaidia kujua jinsi tunavyopaswa kuishi maisha yetu, jinsi ya kuielewa na kuitika miito mbalimbali kama vile upadre, utawa, ndoa na namna ya kuendesha kazi zetu kama biashara, kilimo, kazi ya ajira hata jinsi ya kuipenda, kuitunza na kuiheshimu miili yetu inategemeana na imani tuliyonayo.

Imani inatusaidia kujua namna tunavyopaswa kusali. Tunasali kadiri ya imani na tunaamini kadiri tunavyosali. Sala ni chazo cha imani na sala inaonyesha imani ya mtu. Imani ni sababu ya matumaini yetu. Imani yatusaidia kujua malengo ya maisha yetu na hivyo kutupatia mwelekeo wa maisha yetu na jinsi tunavyopaswa kuishi kwa sasa na baadae. Imani inatupatia maelezo ya mambo ambayo hatuyaelewi kwa akili zetu za kibinadamu mfano uwepo wa matatizo, magonjwa, mateso hata uwepo wa kifo. Katika jamii zetu hata miongoni mwa waliopokea ufunuo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo bado tunashikilia dhana potofu ya imani za kishirikina. Ukatili wa kinyama wa watu wenye ulemavu wa ngozi, biashara ya viungo vya binadamu, mauaji ya vikongwe, imani katika tiba za masharti ya kishirikina kama vile kutoa kafara za watu, au kufanya tendo la ndoa kinyume na maumbile au na watoto au vikongwe hata wanyama, imani kwa mafuta ya upako, maji au chumvi ya upako, pete, medali au mikufu hata nguo na viatu vya upako  ni matokeo ya imani potofu kuwa kwa njia hiyo mtu atafanikiwa katika maisha mfano katika biashara, kupata ajira, kufaulu mitihani au kupata mchumba au watoto. Masharti kama hayo ni uvunjifu wa amri ya kwanza ya Mungu, ni kinyume na imani aliyotufunulia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, pia yanamuathiri mtu mzima kiroho na kimwii.

Imani iwasaidie waamini kujenga mahusiano mema na wengine
Imani iwasaidie waamini kujenga mahusiano mema na wengine

Injili ya mafanikio inayotegemea miujiza bila kufanya kazi, ahadi za kutajirika kimiujiza, maombezi ya kufuta nuksi, kuvunja mti wa ukoo na kumaliza matatizo ya kiroho au kimwili, hofu ya “freemasoni” na dini ya waabudu shetani (devil worship) ni dalili za ukosefu wa imani kwa Mungu mmoja katika nafsi tatu aliyejifunua kwetu kama Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Haya ni matokeo ya kukosekana kwa elimu-dini ya kweli juu ya imani ya kweli na elimu-dunia iliyo bora na yakutosha kutuwezesha kusimama imara na kutolea uamuzi fumbuzi na sahihi kwa changamoto za kimaisha. Tukumbuke daima mafanikio katika maisha yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa huku tukimtanguliza Mungu Roho Mtakatifu ili atujalie karama na vipawa vya kufanya kazi vyema. Basi ndugu nawasihi “simameni imara katika imani ya kweli” ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume ili mpate kulifikia tumaini letu la kweli yaani maisha ya milele Mbinguni.

Dominika 19 ya Mwaka C
04 August 2022, 17:20