Tafuta

Papa Francisko anasema: “Anayetaka kuwa Mfuasi wa Yesu hana budi kutembea kwenye njia ya utakatifu, kwanza atabadilishwa kwa hiari na nguvu ya upendo wa Mungu." Papa Francisko anasema: “Anayetaka kuwa Mfuasi wa Yesu hana budi kutembea kwenye njia ya utakatifu, kwanza atabadilishwa kwa hiari na nguvu ya upendo wa Mungu."  

Sherehe ya Kung'ara Kristo Yesu: Ufunuo wa Utukufu Wake: Msalaba

Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati, toba na wongofu wa ndani katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo.

Na Padre Kelvin Mkama, - Pozzuoli, Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana wetu Yesu Kristo kwa mwaka 2022 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema akisema, “Discipuli esse Iesu et super viam sanctitatis incedere vult imprimis Dei caritatis virtute libenter transfigurari.” Yaani “Anayetaka kuwa Mfuasi wa Yesu hana budi kutembea kwenye njia ya utakatifu, kwanza atabadilishwa kwa hiari na nguvu ya upendo wa Mungu." Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo Yesu; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji.  Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo.

Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa juu ya Msalaba
Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa juu ya Msalaba

Katika somo letu la Injili “Yesu anaufunua umungu wake ili kuimarisha imani ya wanafunzi wake watakapomwona akiteswa Msalabani.” Yesu anapanda mlimani kwenda kuomba. Akiwa mlimani anageuka sura. Tukio la Yesu kwenda mlimani na kugeuka sura linatokea Yesu akiwa safari kwenda Yerusalem ambako atakamatwa, atateswa, atasulibishwa na kisha kuuawa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Hivyo Yesu anapanda mlimani kuomba/kusali ili kuchota nguvu ya kukabiliana na tukio hilo- mateso na kifo chake. Yesu anapanda na wanafunzi wake watatu: Petro, Yohane na Yakobo. Wanafunzi hawa watatu wamekuwa na nafasi ya pekee katika matukio mengi yaliyotendwa na Yesu. Swali la msingi ni hili: kwa nini hawa watatu tu? Yesu anapowapa Mitume hawa watatu nafasi ya pekee hafanyi hivyo kwa bahati mbaya, kuna sababu za Yesu kufanya hivyo: Petro ndiye mtume aliyempenda zaidi Yesu kuliko Mitume wengine na hivyo anaandaliwa kuwa kiongozi wa Kanisa/Mitume (rejea Yn. 21:15-17); Yohane ni mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu, hasa kwa sababu ya useja wake (ndiye Mtume pekee ambaye hakuwa ameoa) aliacha kuoa ili amtumikie Yesu bila kujibakiza; Yakobo wa Zebedayo anaambatana na Yesu kwenye matukio makubwa ili kuimarishwa zaidi kiimani kwani ndiye atakuwa Mtume wa kwanza kuuawa (kumwaga damu yake) kwa ajili ya kumshuhudia Kristo (rejea Mdo. 12:2). Hivyo, nasi tukitaka Mungu ajifunue kwetu ni lazima kuwa na sifa kama za akina Petro, Yohane na Yakobo: kumpenda sana Kristo kama Petro alivyompenda sana Kristo; kujitahidi kupendwa sana na Kristo kama Yohane alivyopendwa sana na Kristo, hasa kwa kutumikia pasipo kujibakiza; kuwa tayari kufa kwa ajili ya Kristo kama Yakobo alivyokuwa wa kwanza kufa kwa ajili ya Kristo.

Tukio la Yesu kugeuka sura linatufunulia mambo mengi makubwa: (1) Yesu Kristo ni Mungu kweli. Mitume walizoea kumwona Yesu katika mwonekano wake wa kibinadamu na hivyo walizoea kumwona katika asili ya kibinadamu. Leo Yesu anageuka sura kuonesha upande wa pili wa asili yake- asili ya kimungu. Kwa tukio hili Yesu anaonesha kuwa Yeye ni Mungu na ni Mwana wa Mungu: “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu…” Lengo kubwa la kufunua umungu wake ni nini? Yesu alifunua umungu wake ili kuwafanya wanafunzi wake wasibaki kumtazama katika ubinadamu wake tu pindi atakapoteswa na kufa msalabani, bali wamwone pia katika umungu wake, yaani Yeye ni Mungu na hivyo atashinda dhambi na mauti na kushiriki utukufu wa Mungu kama vile Musa na Eliya wanavyoshiriki utukufu wa Mungu. (2) Yesu Kristo ni utimilifu wa Torati na Manabii. Biblia ya Kiyahudi iligawanyika katika makundi matatu: vitabu vya Torati, vitabu vya Manabii na vitabu ya Maandiko. Waisraeli walivipa umuhimu wa kwanza vitabu vya Torati (ambavyo waliamini vimeandikwa na Musa), nafasi ya pili vilipewa vitabu vya Manabii (ambavyo Nabii mkubwa kabisa kwa Waisraeli ni Eliya) na nafasi ya tatu ni vitabu vya Maandiko. Katika Injili yetu wanaonekana Musa na Eliya wakizungumza na Yesu juu ya habari ya kifo chake. Musa anawakilisha Torati na Eliya anawakilisha Manabii. Hivyo Yesu ni utimilifu wa Torati na Manabii. Yote waliyofundishwa Wayahudi katika Torati na Manabii yanapata ukamilifu wake katika Kristo Yesu. (3) Kuna maisha baada ya maisha ya hapa duniani.

Kristo Yesu aliwaandaa wanafunzi wake kulipokea Fumbo la Kifo katika maisha yao.
Kristo Yesu aliwaandaa wanafunzi wake kulipokea Fumbo la Kifo katika maisha yao.

Katika tukio hili la Yesu kugeuka sura tayari Musa na Eliya walikuwa “wameondoka katika maisha ya hapa duniani” Musa aliondoka kwa njia ya kifo na Eliya aliondoka kwa njia ya kupandishwa mbinguni katika gari la moto kwa upepo wa kisulisuli. Hata hivyo, licha ya kuondoka katika maisha haya, Musa na Eliya wanaonekana wakiwa hai na kuzungumza na Yesu. Hapa kuna fundisho kubwa: kuna maisha ya kiroho baada ya maisha ya kimwili hapa duniani. Hata hivyo, Musa na Eliya ambao wanaonekana katika utukufu hawakuwa watu wa hovyo ovyo, bali walikuwa watu wacha-Mungu na wema. Hivyo ‘wataonekana katika utukufu” wale tu ambao ni wacha-Mungu na wema. Je, wewe na mimi kwa matendo yetu ya hapa duniani tutastahilishwa kuishi na kushiriki utukufu wa Mungu baada ya kuondoka hapa duniani? (4) Ni lazima kuamka kutoka usingizi wa kiroho ili tuone utukufu wa Mungu/Kristo. Injili inatuambia kuwa wanafunzi walikuwa wamelemewa na usingizi lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wa Yesu. Hapa pia kuna fundisho: ni lazima tuamke/tutoke katika usingizi wa imani ili tuweze kuona utukufu wa Mungu. Kwa bahati mbaya wengi wetu tu usingizini na hivyo hatuoni utukufu wa Mungu: tu katika usingizi wa mila na imani potofu, tu katika usingizi wa anasa za dunia, tu katika usingizi wa ujinga wa kiimani (hatujui imani yetu), tu katika usingizi wa dhambi. Ni lazima tuamke kutoka katika aina hii ya usingizi ili tuone utukufu wa Mungu.

Njia ya kuamka kutoka katika usingizi wa kiroho ni kupenda kujifunza katekesi, kupenda kusoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu, kupenda kusoma vitabu vya kiroho, kupenda kusali, kupenda kushiriki semina na makongamano ya kiroho, kupokea Sakramenti na mengineyo. (5) Mungu yu pamoja na wateule wake, hasa nyakati za mahangaiko, shida na mateso. Yesu anapanda mlimani kusali akijua wazi kuwa muda si mrefu atauawa. Yesu tayari ameishaanza kuteseka sana moyoni kwa kuwa anajua wazi aina ya kifo anachokwenda kuuawa. Hivyo, anasali kumwomba Mungu. Mungu anashuka katika wingu (wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu, rejea Kut. 13:21) na kuonesha kuwa yupo pamoja na Yesu katika safari yake ya mateso. Hata sisi tunapaswa kutambua kuwa Mungu hakai kimya katika mateso yetu wala hatuachi bali yupo pamoja nasi kututia nguvu. Wengi wetu huwa tuna desturi ya kukata tamaa nyakati za shida na kufikiri Mungu hayuko nasi na hivyo kuanza kukimbilia miungu mingine: waganga wa kupiga ramli, wahubiri wanaotenda miujiza, mizimu, n.k. Hata hivyo, Mungu yupo pamoja na wote wanaosali wakati wa shida, mahangaiko na mateso. (6) Tupende kukaa na Mungu na watakatifu wake. Uwepo wa Mungu katika maisha yetu unagusa undani wetu na hata kutawala akili zetu.

Waamini watafute fursa za kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao.
Waamini watafute fursa za kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao.

Uwepo wa Mungu na Watakatifu wake katika maisha yetu unapaswa kuwa tamanio letu la kwanza. Petro, baada ya kuona utukufu wa ajabu wa Yesu, anashauri kujenga vibanda vitatu (cha Yesu, cha Musa na cha Eliya) ili azidi kuona utukufu wa Mungu. Je, mimi na wewe tunatamani kuona utukufu wa Mungu? Je, tunatamani kukaa na Mungu/Yesu? Wengi wetu tunatamani kuona na kujiambatanisha na mambo ya kishetani: kutazama picha za ngono, wivu, chuki, uzinzi, ubinafsi, mauaji, dhuluma, nk. Tuondoe haya ili tuweke mambo yanayoonesha utukufu wa Mungu: amani, upendo, uvumilivu, ukarimu, wema, imani, n.k. (7) Tunapaswa kuwa watii kwa Kristo. Yesu alipogeuka sura, sauti ya Mungu Baba ilisikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikilizeni yeye.” Huu ni mwaliko kwetu sisi sote kumsikiliza Kristo. Je, sisi tunamsikiliza Kristo? Kristo anazungumza nasi katika mahubiri ya makasisi wetu, anazungumza nasi katika tafakari ya Neno la Mungu, anazungumza nasi katika sala, anazungumza nasi katika Sakramenti kama vile Kitubio, anazungumza nasi katika dhamiri zetu adili na anazungumza nasi katika matukio ya maisha. Je, tunamsikiliza? Kwa bahati mbaya wengi wetu badala ya kumsikiliza Kristo tunausikiliza ulimwengu na kelele zake: tunasikiliza porojo za waitwao wafadhili wanaotutaka kutoa mimba ati wakiita afya ya uzazi; tunasikiliza nyimbo za matusi ati tukiziita muziki wa kisasa, tunawatii wanasiasa uchwara badala ya kutii sauti ya Mungu. Tafakari na chukua hatua. Tukio zima la Yesu kugeuka sura lina maana sana katika maisha yetu ya kiroho. Tukio la Yesu kugeuka sura ni mwaliko kwetu tugeuka kutoka maisha yetu ya dhambi na kuwa viumbe vipya, vyenye mwonekano mpya wa maisha ya kiroho na kiutu!

06 August 2022, 08:19