Tafuta

Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu ni tunda la kwanza la kazi ya ukombozi. Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu ni tunda la kwanza la kazi ya ukombozi. 

Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Kristo Yesu: Upendo

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Tunda la wokovu.

Na Padre Benjamin Angelus Mwinuka, C.PP.S. – Roma.

Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika watoto wake wote waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia kuimarisha imani yao kwa nguvu ya upendo wa Mungu pamoja na kutambua kwamba, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba, tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.”

Mpango wa Mwenyezi Mungu wa kumkomboa mwanadamu umekuwa bayana tangu mwanzo wa nyakati. Mpango huu unatangazwa mwanzoni kabisa na Mungu mwenyewe mara tu baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza. Jambo la kusisimua ni ushiriki wa mwanamke katika mpango huo wa wokovu, mwanamke ambaye kwa kuto tii kwake dhambi ilipata kuingia, sasa mwanamke mwingine anatangazwa kuwa ndiye atakaye shiriki katika mpango huo wa wokovu. Mwenyezi Mungu katika tangazo hilo anasema; “nitaweka uadui kati yako wewe na huyo mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake, huyo atakuponda kichwa, nawe utamgonga kisigino” (Mw, 3:15). Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu yajulikana kama Injili ya kwanza kabisa ya Wokovu (Proto-evangelium).  Habari hii Njema ya Wokovu ambayo inatangazwa katika Agano la Kale, yabainisha kwamba ushindi huo utawezekana kwa ushenga wa mtoto wa kiume atakaezaliwa na mwanamke. Hapana shaka kabisa kuwa mwanamke huyu anayetangazwa katika Injili hii ya kwanza ya wokovu ndiye Mama Bikira Maria ambaye anabeba jukumu la kushirikiana kikamilifu na “mshenga” ambaye kwa Damu yake Azizi ‘atamgaragaza’ na kumfanya kibogoyo mshtaki wetu kama tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane,  “Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake, kwa maana ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, yeye awashtakiye mbele za Mungu wetu mchana na usiku, wameshinda kwa damu ya mwana kondo (Uf 12:10-11).”

Bikira Maria Mama wa Mungu. Mtaguso wa Efeso 431
Bikira Maria Mama wa Mungu. Mtaguso wa Efeso 431

UHUSIANO WA MAMA BIKIRA MARIA NA DAMU AZIZI YA BWANA WETU YESU KRISTO

Upo uhusiano wa ndani kabisa wa Damu ya Mama Bikira Maria na Mwanae Bwana wetu Yesu Kristu. Kiini cha mwunganiko huo thabiti na wapekee kuliko uhusiano mwingine wowote ule wa Mama Bikira Maria na Damu Takatifu ya Kristo unakuwa bayana katika FUMBO LA UMWILISHO. Mwinjili Yohane anashuhudia na kusisitiza ajabu hilo akisema “Neno akafanyika Mwili akakaa kwetu nasi tumeuona wokovu” (Yn 1:14). Ni katika msingi huo, kanuni ya Imani ya Kanisa Katoliki inathibitisha na kusisitiza: “Alishuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu, akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.” Maria akiwa kama Mama wa Yesu, alimpa kila kitu ambacho mama humpa mtoto wake awapo tumboni. Ndio kusema, alimpa maisha yake ya kibinadamu; ikiwa ni pamoja na Damu Yake ya thamani, kwa kuwa ilifanyika katika mwili wake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kumbe, Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo aliye tungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ndani ya tumbo la Mama Bikira Maria, vinapata uhusiano wa moja kwa moja, yaani uhusiano wa Mama na Mwana.

Mtakatifu Yohane Damascene anasema; “Kutoka katika Damu safi isiyo na doa ya Bikira Maria, Mwana wa Mungu alijitwalia Mwili na akaungana naye.” Maandiko ya mababa hawa wa kanisa yanaendelea kutilia mkazo wa uhusiano mkubwa wa Mama Bikira Maria na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo, Mama Bikira Maria kwa kukubali kutoa ushirikiano wake kwa uhuru kamili wa dhamiri yake katika malezi ya upendo wa kimama ya ubinadamu kwa Kristo ndani ya tumbo lake la uzazi na kutoka katika hali yake mwenyewe, Mariamu anaweza kuitwa kwa usahihi kabisa chanzo cha damu ya Kristo, na hivyo kanisa la weza na linapaswa kutangaza kwa nyakati zote kuwa, Damu ya Kristo, Damu ya Maria. Aidha uhusiano mwingine wa karibu kabisa wa Mama Bikira Maria na Damu ya Thamani ya Bwana wetu Yesu Kristo ni ule tunaoelezwa katika fundisho la Kukingiwa dhambi ya asili.  Bikira Maria katika tukio la kukingiwa dhambi ya asili, anathibitisha nguvu na ushindi wa “kale” wa Damu ya thamani ya mwana-kondoo asiye na doa. Maria anakuwa tunda la kwanza la ukombozi.

Kristo Yesu ni Kuhani wa Agano Jipya na la Milele.
Kristo Yesu ni Kuhani wa Agano Jipya na la Milele.

Padre G. Faber anasema, “Fadhila zote zimhusuzo Bikira Maria kama uzuri wa taji lake la Kimalkia, kuinuliwa na kushirikishwa utukufu wa mwanae, upendeleo wa neema nyingi na mafumbo yote ya umama wake yana sababu ya pekee katika damu ya thamani ya mwanae Yesu Kristo” Lakini pia uhusiano mwingine ni ule unaojidhihirisha bayana katika sadaka ya Kalvari. Katika Historia ya wokovu wa mwanadamu hakuna mwanadamu mwingine ambaye anatajwa kushiriki kikamili zaidi tena kwa kutoa sadaka ya pekee kama Mama Bikira Maria. Mama Bikira maria alikuwa tayari kushiriki matukio yote ya mwanae ikiwa ni pamoja na dhabihu ya umwagaji wa damu ya mwanae, angalau kwa wazi kwenye matamshi na kwa jinsi mpango wa Mungu ulivyo jidhihirisha, kama Mwinjili Luka anavyo twambia “na upanga utakupenya moyo ili mawazo ya mioyo mingi ya funuliwe (Lk 2: 35).” Ndio kusema, Maria si Mama wa Mwana ambaye alikuja kuwa kuhani pasipo yeye baada ya kuzaliwa kwake, kwa maana Krito Yesu alichukuliwa mimba kama kuhani katika tumbo lake. Kama kuhani alizaliwa na kulishwa na kuvikwa na kuhifadhiwa na Maria. 

Lakini Kuhani huyu, ukuhani wake ni tofauti na makuhani wengine, yeye mwenyewe anakuwa dhabihu ya kutolewa kwa ajili ya dhabihu ya wokovu. Ndio kusema, sadaka ya kristo ilikuwa ni kamilifu na inayo jitosheleza kwasababu alitoa damu (uhai) yake mwenyewe. Kwa hiyo, Maria alishiriki kumtayarisha kuhani ambaye ni dhabihu ya kuteketezwa kwa ajili ya sadaka ya Damu ya ukombozi. Pamoja naye pia alitoa dhabihu kwa kushiriki huzuni na mateso yake kwa kuungana kikamilifu na mwanae kutimiza mpango wa Mungu kwa wokovu wa wanadamu wote. Hivyo basi, Mama wa Yesu aliyesimama chini ya Msalaba ni Mama wa Damu Azizi na anajua vyema upendo mkuu uliomfanya Mwanawe wa Kimungu kumwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya wokovu wetu. Ni kwa njia ya Bikira Maria sote tunataka kuitukuza na kuiheshimu Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mama Bikira Maria chini ya Msalaba aliotundikwa Mwanae aliye tapakaa Damu alikuwa Mama yetu sote. Rejea mazungumzo ya Yesu na Yule mwanafunzi mpendwa. Mwanafunzi huyo hatajwi jina na msisitizo ukiwa “Mwanafunzi aliye mpenda” kumbe yawezekana kabisa mwanafunzi ni MIMI NA WEWE “Mama tazama mwanao” kisha akamgeukia mfuasi “Tazama mama Yako” (Yn 19:26-27).

Mt. Gaspari alianzisha Shirika lake, C.PP.S tarehe 15.8.1815
Mt. Gaspari alianzisha Shirika lake, C.PP.S tarehe 15.8.1815

MTAKATIFU GASPARI NA IBADA KWA BIKIRA MARIA MAMA WA DAMU AZIZI 

Mtakatifu Gaspar Del Bufalo, Mtume na mtangazaji hodari wa Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo alizaliwa Mjini Roma (1786-1837). Alianzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo, mnamo tarehe 15 Agosti 1815 katika nyumba ya Mtakatifu Felix huko Giano dell'Umbria, katika siku ya Sherehe ya Kupalizwa Mama Bikira Maria Mbinguni, Mwili na Roho. Haikuwa kwa bahati mbaya kwamba Mtakatifu Gaspari del Bufalo kuanzisha Shirika lake siku ya sherehe ya Maadhimisho ya Kupalizwa Mbinguni Mama Bikira Maria. Kama wamisionari wengine mashuhuri walio tolea maisha yao katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, Mtakatifu Gaspari naye alipokuwa anaenda kufanya kazi zake za utume wa hadhara daima alibeba Picha ya Mama Bikira Maria wa “Utume”, na pia aliamuru hata Wamisionari wa Shirika lake kufanya hivyo. Kwa kadili ya mapokeo ya shirika la wamisionari wa damu azizi ya Yesu, picha iliyo kuwa ikitumika ni ile ya Mama Bikira Maria akiwa amembeba Mtoto Yesu mkono wa kulia na mtoto akiwa ameshika kikombe, Kalisi. Picha hii imekuwa ikiitwa majina tofauti tofauti kama, “Madonna Auxilium Christianorum, yaani Bikira Maria Msaada wa Wakristo” “Madonna delle Missioni”, yaani “Bikira Maria wa Utume” “Madonna del Calice” yaani: Bikira Maria wa Kalisi Takatifu, “Madonna del Preziosissimo Sangue” yaani Bikira Maria wa Damu Azizi ya Kristo Yesu. Kwa tafsiri kwa lugha ya Kiswahili “BIKIRA MARIA MAMA WA DAMU AZIZI. Picha hii inahusishwa na mchoraji maarufu POMPEO BATONI kati ya miaka ya (1708-1787).

Kwa kadili ya maandiko yake mwenyewe Mtakatifu Gaspari anakiri wazi kwamba picha hii ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi aliipata kutoka kwa Wamisionari wengine ambao walisha kuwepo kabla yake, hivyo wazo la kuchora picha hii halikuwa la Mtakatifu Gaspari, yeye alicho kiongezea kwenye picha hiyo ni KALISI (kikombe) alicho shika Mtoto Yesu mkononi. Mtakatifu Gaspari anasisitiza hilo katika barua yake kwa PALMUCCI akisema “kwa hakika simjui mtu aliye chora picha ya Bikira Maria wa Damu Azizi. Lakini, aliye ongezea kikombe (Kalis)i katika picha hiyo ni Bwana Pozzi.”  Mtakatifu Gaspari katika barua zake na matini mengine aliyoandika hakuna mahali anapo elezea maana ya kiroho kuhusu picha hii, ila kinacho julikana ni kwamba aliibeba popote pale alipokuwa akienda kuhubiri ama kufanya utume. Pamoja na hayo, katika kanuni ya Wamisionari wa Shrika la Damu Azizi ya Kristo kifungu cha 6, iliyopitishwa mwaka 1841inaelezea maana ya kiroho ya picha hii ya Mama yetu wa Damu Azizi ya Bwana Yesu Kristo ikisema: …Pia ni desturi ya Shirika kwamba katika makanisa yetu kuna madhabahu ambayo sura ya Bikira Maria akiwa amembeba Mtoto Yesu mikononi mwake inaoneshwa kwa ajili ya Ibada ya waamini, ameshika mkono wake wa kulia kikombe cha Damu yake Azizi katika hali ya kumwonesha Mama.

Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Kristo Yesu ni Mama Yetu sote.
Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Kristo Yesu ni Mama Yetu sote.

Bikira Mwenye heri mwenyewe anawaalika wadhambi kuitumia dawa hiyo ya Kimungu, iliyotayarishwa kwa ajili ya watu kwa msukumo mkubwa wa upendo wa kufuta dhambi zao na kuwavika wema. Mwanzilishi wetu amethibitisha kwamba Papadre wetu na watumie picha zenye sura moja katika utume… Hivyo basi, kutokana na maelezo haya, Mtoto Yesu anamwonesha mama yake kikombe kilicho furika Damu Azizi, na Mama Bikira Maria anawaalika wakosefu “kuitumia dawa hiyo ya kimungu” siyo tu kwa sababu wametakaswa dhambi zao bali pia kwa sababu wamevishwa huruma na wema wa Mungu. Lakini pia macho ya Mtoto na Mama humtazama mtazamaji, ambapo Mtoto humpa kikombe mama, hakuna shaka kwamba maana ya msingi ni mwaliko kwa wanaomtazama, yaani, wanaomkazia macho ya imani, kana kwamba anawaambia maneno ya Karamu ya Mwisho: “Twaeni Mnywe wote. Hiki ni kikombe cha Damu yangu Damu ya Agano jipya na la milele itakayo mwagika kwa ajili ya wengi na kwa maondolea ya dhambi Mt (26:26-28).”

Mtoto Yesu anapo tuonesha kikombe anatutazama na wakati huo huo mama pia kwa macho yake ya upendo na kwa ishara ya kutuarika kwa mkono wake wa kulia anatutuzama. Hivi, ni nani angekataa zawadi nzuri kama hii iliyotolewa na Mtoto mpole na na mnyenyekevu? Mtoto mwenye uso mzuri na mwenye upole kama mama yake? Mama Maria kwa mkono wake wa kuume, anatusihi tupokee kwa ujasiri kikombe cha Damu Azizi ya Mwanae, kwa sababu alikuwa wa kwanza kupata mwaliko huo katika maamkio ya Malaika (Lk 139-56). Hiyo, anajionyesha kwetu kama kielelezo kamili cha mtu aliyekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo. Ulimwengu mamboleo kwa hakika umejaa chuki, visasi na maudhi mengi yenye kusababisha vilio vingi vya damu. Ni ulimwengu usio tambua na kuheshimu utu na thamani ya mtu. Ndio kusema ni ulimwengu ambao umejitenga na upendo wa Damu Azizi ya Yesu, Bikira Maria anapoona masaibu haya sauti yake iliyo sikika katika harusi ya kana inaendelea kusikika kwetu ikisema “hawana divai”. Daima anaendele kufanya kazi ya “ushenga” baina yetu na mwanae Bwana wetu yesu Kristu akituombea na kuuombea ulimwengu katika mabaya yote yanayo endelea kuhuzunisha uso wa Yesu.  Upendo wake wa kimama daima unatualika kushiriki na kunywea kikombe cha Damu Azizi ya mwanae rejea agizo analo toa katika Harusi ya ya Kana “Lolote atakalowaambia, fanyeni (Yn 2:5).” Ni katika kikombe cha mwanae Bwana wetu Yesu Kristu tunapata furaha ya Kweli na kuimba naye utenzi wa kumtukuza Mungu ambao yeye mwenyewe aliuimba akisema, “Moyo wangu wamtukuza Bwana, Na Roho yangu imeshangilia katika Mungu, Mwokozi wangu (Lk 1:46-47).”

Bikira Maria ni Tunda la Kwanza la Ukombozi.
Bikira Maria ni Tunda la Kwanza la Ukombozi.

Ni ukweli kwamba neema ya wokovu wetu ni kazi ya Mungu, lakini Mama Bikira Maria Mama wa Damu Azizi anabaki kuwa mshiriki wa pekee, kielelezo na mnufaika wa kwanza wa tunda la wokovu hivyo sisi kanisa linalo safari kwa mfano wa maisha bora ya fadhila wa mama yetu, tunaalikwa kuukumbilia ulinzi wake yeye ambaye anajua namna nzuri ya kuomba. Damu ya Kristo ni Damu ya Agano Jipya na la milele. Mama Bikira Maria ndiye Sanduku la Agano jipya na la milele. Kumbe, Mama huyu anatualika sote katika sherehe hii ya Agano jipya na la milele tujumuike katika karamu hii isiyo na ubaguzi, “Damu iliyo mwagika kwa ajili ya wengi kwa maondoleo ya dhambi” (Misale ya Kirumi katika sala ya Ekaristi). Damu inayotufanya tung’are Roho zetu na kuona maana halisi ya maisha. Wapendwa, tumkimbilie daima Mama Bikira Maria Mama wa Damu Azizi tukifahamu kwamba, alishirikiana kwa namna ya pekee sana na Mwanae katika kazi ya ukombozi, kiasi kwamba pale Kalvari alitangazwa na Yesu kuwa Mama wa Kanisa Kwa hiyo, Mariamu, ambaye tayari anafahamu kutokana na uzoefu wake manufaa makubwa yaliyomo katika Damu Azizi ya Mwanae, anamwalika kila mtu kunywea kutoka kikombe kimoja cha mkono wake wa kulia, ili wote waweze kufurahia matunda ya wokovu wake kwa ajili ya utakaso wao wenyewe, na kushirikiana na Yesu katika kazi ya ukombozi wa ulimwengu (taz.Kol 1:24).

B.M. Mama wa Damu Azizi
14 August 2022, 14:55