Nigeria:Watawa wanne wametekwa nyara kusini-mashariki mwa Nigeria
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Watawa wanne wa wa Shirika la Yesu Mwokozi walitekwa nyara nchini Nigeria. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la habari za Kimisionari Fides, watawa hao wanne, Johannes Nwodo, Christabel Echemazu, Liberata Mbamalu na Benita Agu, walizuiwa na watekaji nyara walipokuwa wakienda kwenye misa ya shukrani ya Sisita mmoja Dominika asubuhi, tarehe 21 Agosti kando ya mji wa Okigwe. -Humulol katika eneo la Serikali ya Mtaa ya Okigwe katika Jimbo la Imo, Kusini-mashariki mwa Nigeria.
Maeneo ya Okigwe na Leru yaliyo kati ya majimbo ya Imo na Abia yameathiriwa na kuongezeka kwa matukio ya kuteka nyara. Tukio hilo lilitokea takriban siku tisa baada ya watu wenye silaha kumteka nyara kuhani mwingine wa Kikatoliki na mseminari kando ya barabara ya Obigwe-Umunneochi kati ya majimbo hayo mawili. Wanaume hao wawili waliachiliwa muda mfupi baadaye.
Masista wa Yesu Mwokozi (pia wanajulikana kama Saviorites Sisters SJS) ni shirika la Kitawa lililoanzishwa mnamo mwaka 1985 katika Jimbo la Port Harcourt, Rivers State, kusini mwa Nigeria. Karama ya Shirika hilo inajumuisha kuwajali kwa huruma wagonjwa na watu wa Mungu wanaoteseka, hasa walemavu, maskini, wazee na waliotelekezwa kabisa na jamii, kiuchumi, kiroho, kielimu, kisaikolojia na kiakili.
Shirika la Habari za Kimisionari Fides, lilizungumza na Askofu Luka Sylvester Gopep, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Minna,na kutoa maoni yake juu ya habari ya kutekwa nyara kwa watawa hao wanne kwamba “Kwa bahati mbaya, hali katika nchi yetu tunayoipenda, Nigeria, haiko sawa lakini tunabaki na imani kwa Mungu kwa ajili ya siku zijazo”.