Tafuta

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, limeadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 , Accra, Ghana. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, limeadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 , Accra, Ghana. 

Mkutano Mkuu wa 19 wa SECAM: Ujumbe Kwa Watu wa Mungu Barani Afrika: Haki na Amani

Ujumbe wa SECAM: Umiliki wa SECAM, Ukosefu wa usalama; Kanisa na hali ya wakimbizi, Kanisa katika Sinodi, Vyombo vya mawasiliano ya jamii na hatimaye ni shukrani kwa wadau mbalimbali. SECAM inasema, maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 19 imekuwa ni nafasi ya kukutana, kusali na kushirikishana uzoefu na mang'amuzi yashughuli za kichungaji kutoka Barani Afrika. SECAM

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, limeadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Accra, nchini Ghana kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani. Baada ya mkutano huo, Mababa wa SECAM wametoa ujumbe maalum kwa watu wa Mungu kwa kuonesha: Umiliki wa SECAM, Ukosefu wa usalama Barani Afrika; Kanisa na hali ya wakimbizi Barani Afrika, Kanisa katika Sinodi, Vyombo vya mawasiliano ya jamii na hatimaye ni shukrani kwa wadau mbalimbali. Mababa wa SECAM wanasema, katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 19 wamepata nafasi ya kukutana, kusali na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Afrika na Madagascar. Wamepembua kuhusu mchakato wa ukombozi wa mwanadamu unaogusa kweli za kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, kiikolojia, maadili na utu wema, kama unavyofafanua kwenye Waraka wa SECAM wa Kampala, Uganda wa Mwaka 2019. SECAM ni chombo cha ushirika na mshikamano wa Kanisa Barani Afrika, tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, wajumbe wa SECAM hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajitegemea kwa rasilimali fedha, mali na watu, ili kutekeza kikamilifu dhamana na utume wao wa uinjilishaji Barani Afrika, huku wakishuhudia ushirika wa watu wa Mungu Barani Afrika. Mmisionari wa kweli ni mtakatifu, mwaliko kwa watu wa familia ya Mungu Barani Afrika kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama ushuhuda wa Ukristo wao.

Mababa wa AMECEA katika Mkutano wao mkuu wa 19 mjini Accra, Ghana 2022
Mababa wa AMECEA katika Mkutano wao mkuu wa 19 mjini Accra, Ghana 2022

Sehemu mbalimbali Barani Afrika zinakabiliwa na vita, kinzani, umaskini, mipasuko ya kidini, kisiasa na kijamii, miundo mbinu hafifu ya afya, vitendo vya kigaidi, misigano ya kidini kwa malengo ya kisiasa, uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, mwaliko kwa watu wote wa Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, vitendo hivi vinafikia ukomo. Watunga sera na watekelezaji wake, watambue kwamba, wanayo dhamana na wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba, haki, amani, usalama na utulivu vinarejea tena Barani Afrika. Vyombo vya ulinzi na usalama Kimataifa, vinapaswa pia kushiriki kikamilifu Barani Afrika, ili kweli amani na utulivu viweze kutawala. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kinabii kwa kupinga na kulaani vitendo vyote vya uvunjifu wa misingi ya haki na amani Barani Afrika na kwamba, Kanisa linatakiwa kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani. Mababa wa SECAM wanabainisha kwamba, tangu mwanzo wa historia ya mwanadamu, kumekuwepo na matatizo, changamoto na fursa kwa wakimbizi na wahamiaji. Kuna sababu msingi zinazowafanya baadhi ya watu kuzikimbia nchi zao kutokana na majanga asilia, hali mbaya: kiuchumi, kisiasa na kiakili zinazowafanya baadhi ya watoto wa Afrika kuwa na haki ya kuzikimbia nchi zao kadiri ya Tamko la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki Msingi za Binadamu.

Wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi za kisiasa limepelekea watu hawa: kunyonywa na kudhalilishwa utu, heshima na haki zao msingi. Hawa wamekuwa ni watu ambao wananyimwa haki yao ya utambulisho kama wakimbizi na wahamiaji. Wanakumbana na ujinga wa hali ya juu kabisa kwa kuogopa umaskini wao “Aprophobia” yaani “hofu ya umaskini. Mababa wa SECAM wanawataka wanasiasa, watunga na watekelezaji wa sera mbalimbali Barani Afrika kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira bora na thabiti yatakayo saidia kudhibiti uhamiaji haramu kutoka Barani Afrika. Kati ya mambo msingi ni: utawala bora, fursa za ajira, uhakika wa usalama wa watu na mali zao; umoja na mafungamano ya kijamii sanjari na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa haki jamii. Kwa nchi zile zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa hazina budi kuhakikisha kwamba zinalinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa wale vijana wanaodhani kwamba, wanataka kutekeleza haki yao msingi ya kuhama na kuzikimbia nchi zao, watambue fika kwamba, mbele yao kuna changamoto kubwa sana kwa wakimbizi na wahamiaji. Jambo la msingi kwa vijana ni kuhakikisha kwamba, kamwe hawakati tamaa wala kuvunjika na kupondeka moyo, bali waendelee kumwamini na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa kujitahidi kuishi kitakatifu.

Wajumb wa SECAM wakishiriki katika mkutano wa 19  mjini Accra, Ghana.
Wajumb wa SECAM wakishiriki katika mkutano wa 19 mjini Accra, Ghana.

Mababa wa SECAM wanabainisha kwamba, Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi dhidi ya utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Mababa wa SECAM wanasikitika kuona makundi ya vijana kutoka Barani Afrika yakikimbilia ughaibuni kutafuta fursa, wakati wanatambua fika mateso na majanga wanayokwenda kukumbana nayo mbeleni. Wengi wao wamefariki dunia, jangwani na kuzikwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania, ambako hakuna hata alama ya makaburi yao. Haki msingi kwa vijana Barani Afrika ni kubaki nchini mwao, ili waweze kushiriki katika ujenzi wa nchi zao.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023, tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Alikazia: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa unaotekelezwa na kila mbatizwa, kama kielelezo cha imani tendaji! Ni wakati wa kuondokana na nadharia, mtazamo mgando, ili kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja, daima likiwa karibu zaidi na watu! Kanisa linapaswa kutenda kadiri ya ukaribu, upole na huruma ya Mungu, kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu; na kuendeleza majadiliano ya: kiekumene, kidini na kitamaduni na watu wa Mungu popote pale walipo! Hiki ni kipindi cha kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu ndani na nje ya Kanisa. Sinodi ya XVI ya Maaskofu ilizinduliwa rasmi Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Viongozi wapya wa SECAM
Viongozi wapya wa SECAM

Mchakato wa Awamu ya Kwanza umeyahusu Makanisa Mahalia na Taasisi zote za Kanisa na ulianza Mwezi Oktoba 2021 hadi tarehe 15 Agosti 2022. Awamu ya Pili ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Lengo kuu ni kuhamasisha majadiliano katika ngazi ya Mabara, ili hatimaye, kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum Laboris.” Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023 na itahudhuriwa na wajumbe watakaokuwa wameteuliwa kutoka kwenye Mabara na maadhimisho haya yatakuwa ni chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Kanisa linataka kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mababa wa SECAM wanawaalika watu wa Mungu Barani Afrika kuyasindikiza maadhimisho haya kwa sala na mtindo wao wa maisha.

Nyaraka Muhimu katika Maisha na Utume wa Kanisa Barani Afrika: Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Pili ni Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote vita na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Waraka huu unajikita zaidi katika masuala msingi ya kijamii katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa SECAM wanasema, kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi Barani Afrika, familia ya Mungu Barani Afrika inaitwa na kuhamasishwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ikolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ikolojia kwa njia ya na ushirikishwaji wa jumuiya! Mababa wa SECAM katika Waraka wa Kampala wa Mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu: “Wapate Kumjua Kristo na Kuwa na Uzima tele” (Yn 17:3; 10:10. Waraka huu pamoja na mambo mengine unakazia umuhimu wa mawasiliano Barani Afrika.

Mkutano wa SECAM muda wa kusali, kutafakari na kupanga mikakati ya kichungaji.
Mkutano wa SECAM muda wa kusali, kutafakari na kupanga mikakati ya kichungaji.

Wataalam wa sayansi ya mawasiliano ya jamii wa Kikatoliki wanahimizwa kutekeleza dhamana na utume wao kwa kuzingatia usawa; kwa kutafuta na kuanzisha mahusiano na mafungamano ya Kikanisa na ya Mashirika ya Kimataifa. Mababa wa SECAM waliahidi kuboresha na kuimarisha kitengo cha mawasiliano ya jamii, kwa kutumia rasilimali zake ili kuboresha mawasiliano kwa Kanisa Barani Afrika. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwekeza katika malezi ya kitaaluma, kiufundi, kimaadili na kiutu kwa mihimili yote ya uinjilishaji, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Malezi na majiundo makini ya wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii Barani Afrika ni muhimu sana kwa wakati huu, pengine hata kuliko nyakati za nyuma. Mababa wa SECAM wanakaza kusema, Kanisa Barani Afrika litaendelea kujielekeza zaidi katika kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali. SECAM itaendeleza mchakato wa maboresho ya njia mbalimbali za mawasiliano sanjari na kuwafunda wadau wa tasnia ya mawasiliano, ili Kanisa Barani Afrika liendelee kujikita katika mchakato wa: Ushirika, Upatanisho na Amani. Mwishoni, Mababa wa SECAM wanatoa shukrani zao za dhati kwa wadau wote walioshiriki na kufanikisha maadhimisho ya Mkutano wa 19 wa SECAM huko Accra, Ghana kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022.

SECAM Ujumbe
06 August 2022, 16:14