Kituo cha Vijana Nala-Dodoma:Vijana na waamini kuchangia kituo ili kuimarisha malezi na makuzi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kongamano la Tano la Kitaifa la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, (VIWAWA), lilihitimishwa hivi karibuni mnamo tarehe 8 Agosti 2022 ambalo lilifanyika katika Jimbo Kuu katoliki la Tabora Tanzania huku likiongozwa na kauli mbiu: “Simama nimekuteua uwe shahidi wa yale uliyoyaona.” (Mdo 26: 16). Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ikizungumza na Padre Adolf Minga, Mratibu wa Vijana, Baraza la Maaskofu Tanzania TEC, mara baada ya Mkutano huo, alisema kwamba mkutano huo ulikuwa awali ya yote ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na Utume aliowapatia Mungu. Kuona wapi wamefaulu na wapi wameshindwa. Ni vema kuwasaidia vijana wengi kwa kila njia katika kujikwamua na maisha yao kiroho na kimwili hasa katika kukutana kwa pamoja. Na ni muhimu kuwa na kituo cha vijana katika maelezi na makuzi. Padre Minga alisema “Hii ni kama asemavyo Papa Francisko kwamba “haijalishi uzoefu wa kibinadamu, maisha ya kiroho, hali ya uchumi na kijamii, utamaduni na shughuli zinazompatia kijana mahitaji yake msingi, kwani vijana wote wanakaribishwa ili kupyaisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mwaliko kwa vijana wote ni kuchuchumilia utakatifu na maisha adili”.
Akiendelea na ufafanuzi zaidi Padre Minga alieleza jinsi ambavyo kwa neema ya Mungu, maudhurio hata kwa mwaka huu yalikuwa mazuri na muhimu kwani vijana wapatao 2500 kutoka majimbo yote 34 katoliki Tanzania waliweza kufika. Mada zilizotelewa zilikuwa ni kama zifuatavyo: Kijana ni shahidi wa Yesu; Uzalendo na siasa; kilimo cha kisasa; Athari za Ushirikina kwa vijana; Vijana na Utandawazi; Vijana na Ujasiliamali; Vijana na maisha yangu; na hatimaye vijana na maamuzi stahiki. Wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Misa iliongozwa na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), wakati huo huo Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, akisaidiana na Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda walifunga tukio hilo, na mgeni rasimi alikuwa ni Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Waziri wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), na kuudhuriwa na waamini Watu wa Mungu, Walezi wa vijana wa kutosha, viongozi mbali mbali wa dini na serikali na waalikwa kutoka nchi za nje kama vile: Burundi, Rwanda, Ivory Coast, Ethiopia, Malawi, Kenya, Uganda pamoja na Italia. Mkutano ujao wa VIWAWA unatarajiwa kufanyika mnamo mwaka 2025. Katika mkutano wao kwa mujibu wa Padre Minga amethibitisha kuwa wamejiwekea malengo ya kufikia hasa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha vijana NALA–Dodoma katika Mji Mkuu wa Tanzania.
Kuhusiana na kituo hicho Padre Minga amewasilisha kwa vyombo vya habari Vatican, (Idhaa ya Kiswahili) Barua iliyoandikwa na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC. Kwa mujibu wa barua hiyo iliyoelekezwa kwa :wakurugenzi na Walezi wa vijana Jimbo(VIWAWA;TYCS; TMCS na SKAUTI KATOLIKI); Mkurugenzi wa Walei Jimbo, Mwenyekiti wa Walei Jimbo; vijana wote na waamini wote wa Mungu, kuhusu kuomba mchango kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Askofu Mapunda katika barua iliyoandikwa mwanzoni mwa mwaka huu 2022 inabainisha kwamba: “Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kijana katika Kanisa, limeona yafaa kuwa na huduma ya vijana inayojitosheleza ambapo vijana wataimarishwa zaidi kiroho, kiimani na kupata majibu ya maswali mbali mbali katika maisha yao ya kutumikia Mungu”.
Hata hivyo Askofu Mpunda katika barua hiyo pia alibainisha jinsi ambavyo- “vijana hao kwa juhudi zao wenyewe waliweza kununua ekari 8 za kiwanja huko Nala Dodoma na kuwa na Hati miliki ili kujibu kiu ya vijana”. Kwa maana hiyo “Katika mkutano wa 77 wa Maaskofu kwa sauti moja walikubaliana kuazimia kupitia Idara ya vijana kwamba kila kijana waweze kuchangia kiasi cha kima cha chini kabisa cha shilingi elfu moja kabla ya mwezi Septemba mwaka huu 2022”. Kutokana na hilo, Mratibu wa Vijana Kitaifa amehimiza tena kwamba “Mwezi Septemba unakaribia, na kwa yule ambaye bado hajafanya hivyo, basi ni wakati hajachelewa, anakumbushwa kufanya hivyo”. Katika barua hiyo pia inaelezea jinsi ambvyo mchango huo utakavyotumika kwamba: “Kwa mchango utakaopatikana ni kwa ajili ya kujenga Holi la Mikutano, kujenga Hostel, jengo la Utawala, kujenga fensi ya eneo, ujenzi wa Kanisa na kutengeneza viwanja vya mpira na mengineyo muhimu kwa ajili ya vijana”.
Makadirio ya ujenzi huo yalikuwa ni bilioni tano, hivyo Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania, waliweza kuteuwa hata Dominika moja ambayo iweze kutumika katika kutoa mchango kwa ajili ya idara ya vijana Kitaifa na ambayo walionelea ifanyike kitaifa katika “Sherehe za Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme”, itakayofanyika mnamo tarehe 20 Novemba 2022. Kwa njia hiyo kila mmoja anaalikwa kuchangia kwa ukarimu wake na kwamba sadaka yote kwa siku hiyo iweze kuchangia kituo hicho cha vijana na utume wa vijana. Katika barua hiyo aidha inaweka maelekezo muhimu ya uwasilishaji wa fedha kwa kila jimbo.
Katika mahojiano hayo na Padre Adolf anakumbusha tena na tena kwa dhati juu ya uchangiaji huo wa kwanza wa vijana wote shilingi elfu moja na kwa kila mwaamini mwenye mapenzi mema ili kufikia Mwezi unaoanza Septemba 2022 uwe umekamilisha, na wakati huo huo kujiandalia na uchangiaji kitaifa kwa siku iliyopangwa na maaskofu, “ili kuweza kufikisha lengo hili muhimu na ufanisi wa vijana wetu wa Kanisa letu, la leo na kesho na kwa Taifa zima, ili kuwa na kituo chao muhimu cha makutano”. Kwa kuongezea Padre Minga alisema: “Shukrani kuu kwa Mgeni rasmi wa kufungua Mkutano huo, Mh. David Mwakiposa Kihenzile, Rais wa Msalaba Mwekundu,Tanzania na Mbunge wa Mufindi ambaye alichangia milioni mbili kwa ajili ya kituo na Waziri Bashungwa ambaye kwa siku ya kufunga mkutano huo alitoa shilingi milioni tano kwa ajili ya kituo hicho. Padre Minga kwa kuhitimisha alisema: “ili kituo kikamilike milioni 21 zinahitajika kwa awamu ya kwanza, mwanzoni mwa mwaka huu 2022, ambapo tunahitaji milioni tano ambazo ni kuanzia kazi”.