Mama Evaline Ntenga: Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: Wito na Mwaliko wa Utakatifu
Mama Evaline Malisa Ntenga, - Moshi, Kilimanjaro, Tanzania.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema, Kristo Yesu anawaalika watu wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Watakatifu ni watu wanaowatia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale; hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu.
Watakatifu ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako! Neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia Matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Wakristo watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani, kumbe, wanatumwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kadiri ya historia na changamoto za Kiinjili; daima kwa kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la maisha na utume wake, kielelezo makini cha ufunuo wa upendo na huruma ya Baba wa milele kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!
Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo Yesu unaowabidiisha katika maisha yao! Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA yananogeshwa na kauli mbiu "Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji” na kilele chake ni tarehe 11 Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam, WAWATA itakapowasha moto wa imani, matumaini na mapendo, tayari kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. WAWATA Wanalo Jambo lao muhimu sana siku hiyo!
Ni katika muktadha wa maadhimisho haya yanapoelekea kileleni, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, katika semina kwa WAWATA Kanda ya Kaskazini inayoundwa na Majimbo yote yaliyoko chini ya Jimbo kuu la Arusha, hivi karibuni, ameendesha semina maalum, akiwataka WAWATA kutambua kwamba, wao ni chumvi ya ulimwengu wanaitwa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yao. WAWATA wawe ni ni chumvi ya kuyakoleza malimwengu kwa utakatifu wa maisha, kwa kujikita katika ukarimu na ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kuganga na kuponya majeraha yanayomwandama mwanadamu; kwa kunogesha maisha kwa hekima ya Kimungu inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu, Sala, Sakramenti na Matendo adili, tayari kuyatakasa pia malimwengu. Ili kuyatakatifuza malimwengu wanapaswa kwanza kabisa kuwa na mawazo na moyo safi unaosheheni wingi wa huruma na mapendo, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya WAWATA wamepewa hadhi kubwa ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. WAWATA wajitakatifuze na kuyatakatifuza malimwengu kwa uwepo wao, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika historia ya ukombozi hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba.
WAWATA wajitahidi kuwepo: kimwili, kihisia, kisaikolojia na kiroho, ili kukoleza mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wanawake wajitahidi kuwepo katika maisha na utume wao wa Kifamilia, wakitambua kwamba, mara nyingi wao wamekuwa ni nguzo ya familia pale ambapo Mababa wanapokosekana katika familia. Hali ya Baba wa familia kutokuwepo katika familia inaweza kuwatumbukiza wanawake katika upweke hasi na hali ya kujikatia tamaa; na matokeo yake ndio mwanzo wa “michepuko”; malezi tenge pamoja na athari za maendeleo: kiuchumi, kijamii na kiroho. Kutokuwepo kwa baba katika familia kuna athari nyingi sana katika malezi na makuzi ya watoto kiasi cha kujenga tabia ya chuki kati ya watoto na baba yao; watoto kukosa mahitaji muhimu na upendo kwa familia kupungua siku hadi siku. Watoto kukengeuka na kutopea katika malimwengu na huo ndio mwanzo wa makundi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Kuna mambo yanayowafanya wazazi wa kiume kukosa muda wa kukaa nyumbani na “asali wa nyoyo zao” pamoja na familia zao ni pamoja na: migogoro inayofyekelea mbali ile furaha ya familia; tabia ya uasherati, ulevi, misiba na kufilisika: kiroho, kimwili na kiakili. Ili kuweza kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu, WAWATA wanawataka wenzi wao wa ndoa kuwepo kwenye familia, maisha na utume wao, ili hatimaye, waweze kutangaza na kushuhudia: Ukuu, uzuri, utakatifu wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu.
Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Maisha ya ndoa na familia wanasema WAWATA yakolezwe kwa sala za kifamilia, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; Kusamehe na kusahau; upendo na uaminifu unaosimikwa katika ukweli na uwazi. Wazazi wote wawili washirikiane na kushikamana katika malezi na makuzi bora ya watoto wao. Wazazi wawe ni washauri wema na watakatifu, watoto wawe ni chemchemi ya furaha, amani na utakatifu wa maisha. Wawasikilize watoto wao na kuwatekelezea yale mambo msingi, wazazi wajifunze kuwa ni watu wema, na mifano bora ya kuigwa na watoto pamoja na jirani zao. Katika shida, mahangaiko na patashika za maisha na utume wa familia, wazazi wawe wadadisi, tayari kusoma alama za maisha ya watoto wao. Watiane shime na kufarijiana katika maisha, ili hatimaye, kuuona mwanga wa Kristo Mfufuka anayetembea kati pamoja nao kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau aliyewafafanulia Maandiko Matakatifu, lakini wakamtambua tu wakati wa kuumega mkate.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, anasema, ulimwengu mamboleo unaendelea kushuhudia familia tenge, ambamo mwanamke anaishi peke yake na kuendelea kukabiliana na: fursa, changamoto na matatizo ya kifamilia. Jambo la msingi ni kuondoa hofu na wasi wasi katika maisha kwa sababu inawezekana kukosa mme kutokana na sababu mbalimbali katika maisha: changamoto za maisha ya ndoa na familia; mama “hakupata” mtu wa kumwoa; athari za utandawazi, nguvu ya pesa na tabia za usagaji na ushoga. Katika muktadha huu, mwanamke awe imara katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu. Ashirikiane na wanawake wenzake kupambana na umaskini wa hali na kipato. WAWATA wajitahidi kuboresha hali ya maisha yao ya kiroho, kiutu na kijamii kwa nguvu ya sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa kama kielelezo cha imani tendaji. WAWATA wanakumbushwa kwamba, watakapoitupa mkono dunia na kwenda kulala kwenye usingizi wa amani, wasitafutwe kwenye makaburi yaliyojengewa kwa marumaru, bali kwenye nyoyo za watu waliowahudumia kwa: imani, matumaini na mapendo! Kumbe Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA: isimikwe katika Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji.