Tafuta

Kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2022 Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2022 Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. 

Jubilei ya Miaka 25 ya Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam: Umisionari na Huduma

Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam, nchini Tanzania kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2022 linaadhimisha Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, sherehe ambayo inaadhimishwa kwa kishindo na kilele chake ni tarehe 28 Desemba 202: Umisionari wa Watoto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa kawaida Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950 inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka tarehe 6 Januari sanjari na Sherehe ya Tokeo la Bwana. Papa Pius XII aliwataka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha na utume wa Kanisa unaanza na kusimikwa katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, zinazomwilishwa kila siku, hatua kwa hatua hasa katika malezi na makuzi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, watoto kuendelea kuinjilisha mintarafu hali na mazingira wanayokumbana nao kwa wakati huu. Ikumbukwe kwamba, watoto wanapaswa kujifunza na hatimaye, kujenga utamaduni wa: ushirika, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Hii ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimisionari tangu sasa, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na baa la umaskini linalosigina utu, heshima na haki zao msingi.

Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia! Huu ndio mshikamano wa watoto katika huduma ya Injili ya huruma na mapendo. Hata watoto kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, na hivyo, wanahamasishwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu katika maisha na mazingira yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hata Mtoto Yesu alikumbana na “mkono wa chuma na udhalimu wa Mfalme Herode” kiasi cha kuwafanya wazazi wake kukimbilia uhamishoni Misri. Hata leo hii, kuna watoto wanafariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo mkali; magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibika pamoja na ujinga! Watoto hawa ni mboni ya Jicho la Kristo! Kanisa litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa na kwamba, watoto wanapewa haki ya kufurahia utoto wao katika mazingira ya amani na utulivu na kwamba, watoto hawa wasipokwe furaha na matumaini yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Watoto ni wamisionari wazuri miongoni mwa watoto wenzao, watuwe shime.
Watoto ni wamisionari wazuri miongoni mwa watoto wenzao, watuwe shime.

Ni katikia muktadha huu, Ndugu Cletus Majani, Mwenyekiti wa Walezi wa Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam, nchini Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2022 linaadhimisha Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, sherehe ambayo ilipaswa kuadhimishwa mwaka 2021, lakini kutokana na changamoto mbalimbali inaadhimishwa kwa kishindo na kilele chake ni tarehe 28 Desemba 2022, watoto kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam watakapowazunguka Maaskofu wao, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya miaka 25 ya uwepo na utume wao kama wamisionari miongoni mwa watoto wenzao. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Miaka 25 ya Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar Es Salaam ilizinduliwa rasmi tarehe 28 Desemba 2021 kwa kuwasha Mshumaa wa Jubilei ambao unaendelea kutembezwa kwenye Parokia mbalimbali za Jimbo kuu la Dar es Salam kuchochea na kukoleza ari na mwamko wa umisionari miongoni mwa watoto wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Ndugu Cletus Majani, Mwenyekiti wa Walezi wa Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam anakaza kusema, hii pia ni fursa kwa wazazi na walezi kupata semina mbalimbali kuhusu: Historia ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa; Ulinzi na Utetezi wa Haki Msingi za Watoto dhidi ya nyanyaso na dhuluma za kijinsia. Katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2022, Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam umechanga jumla ya shilingi milioni tisa na thelathini saba elf una vitu vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni tatu kwa ajili ya kusaidia watoto wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hija ya Kimisionari Parokia ya Kimbiji, Jimbo kuu la Dar Es Salaam kuanzia tarehe 11 hadi 15 Agosti 2022 ni mahususi kwa ajili ya walezi na watoto 1920, kutoka Parokia za Jimbo kuu la Dar es Salaam, huku wakiwa wanasindikizwa na walezi wao 297, kati yao kuna watawa 13.

Watoto na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Watoto na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Hivi karibuni, Tanzania imekuwa ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA ulionogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ndiyo mada kuu iliyoongoza mkutano wa AMECEA kwa mwaka 2022. Kimsingi Waraka unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kumbe, Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam lina chambua tena mada hii kadiri ya mazingira ya Utoto Mtakatifu. Kuna mada ya Liturujia: Ibada na matendo katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa; Ulinzi na Utetezi wa Haki Msingi za Watoto dhidi ya nyanyaso na dhuluma za kijinsia. Hija ya Kimisionari Parokia ya Kimbiji, Jimbo kuu la Dar Es Salaam itahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu na Maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu kuzunguka viunga vya Parokia hii, kielelezo cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tangu mwaka 2005 alitoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa uinjilishaji kwenye Parokia ambazo zilikuwa pembezoni mwa Jimbo kuu la Dar es Salam na Parokia ya Mafia, ikawa na upendeleo wa pekee katika maisha na utume wake, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, yanayosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu Kisiwani Mafia, kwa njia ya huduma makini.

Jubilei ya Miaka 25 ya Utoto Mtakatifu, kilele chake ni tarehe 28 Desemba 2022
Jubilei ya Miaka 25 ya Utoto Mtakatifu, kilele chake ni tarehe 28 Desemba 2022

Mama Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba, kila mwaka anapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwamko wa ari na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani zao. Waamini wanakumbushwa kwamba, utakatifu ni wito na mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuchuchumilia na kuambata ukamilifu wa maisha kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kumwilisha Matunda ya Roho Mtakatifu katika uhalisia wa maisha yao. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mwezi Oktoba, uliotengwa maalum kwa ajili ya hamasa ya kimisionari, Watoto wa Utoto Mtakatifu, mwanzoni mwa Mwezi Desemba 2022 watafanya matendo ya huruma kwa watoto wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Utoto Mtakatifu
11 August 2022, 16:25