Tafuta

Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu watatu wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre na Bro. Francis Maganga anaadhimisha Miaka 25 ya kuwekwa wakfu kama mtawa wa C.PP.S. Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu watatu wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre na Bro. Francis Maganga anaadhimisha Miaka 25 ya kuwekwa wakfu kama mtawa wa C.PP.S. 

Bro Francis Maganga Jubilei ya Miaka 25 ya Utawa! Ndoa 8 Zafungwa Sanza, Singida!

Kilele cha Jubilei ya Bro. Francis Maganga, ndugu zake katika familia, wameamua kuachana kabisa na “uchumba sugu” uliokuwa unawapekenya kwa miaka kadhaa, sasa wanafunga ndoa na kushuhudiwa na Askofu Edward Mapunda, tayari kutangaza na kushuhudia maisha ya ndoa na familia katika: Ukuu, uzuri, na utakatifu wa Injili ya familia unaobubujika kutoka kwa Mungu Mkuu.

Na Angela Andrew Kibwana, Morogoro & Pd. Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, Jumatano tarehe 3 Agosti 2022, anaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu Bro. Francis Maganga wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., alipowekwa wakfu kuwa Mtawa. Hili ni tukio ambalo linaadhimishwa kwenye Parokia ya Sanza, Jimbo Katoliki la Singida kwa kuleta mvuto wa pekee katika maisha ya ndoa na familia. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Bro. Francis Maganga, ndugu zake katika familia, wameamua kuachana kabisa na “uchumba sugu” uliokuwa unawapekenya kwa miaka kadhaa, sasa wanafunga ndoa na kushuhudiwa na Askofu Edward Elias Mapunda, tayari kutangaza na kushuhudia maisha ya ndoa na familia katika: Ukuu, uzuri, utakatifu wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Wanatambua fika kwamba, ndani ya familia kuna matatizo, changamoto na fursa zake, lakini sasa wameamua kupiga moyo konde na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wanataka kujenga familia zao, ili ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia ili hatimaye, ziweze kuwa ni vitalu vya miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Jubilei ni Kipindi cha kuwasha moto wa imani, matuimaini na mapendo
Jubilei ni Kipindi cha kuwasha moto wa imani, matuimaini na mapendo

Itakumbukwa kwamba, tarehe 29 Julai 2022, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki la Morogoro, ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S., Padre Dennis Pantaleo Massawe, C.PP.S., Padre Gregory Simon Mkhotya, C.PP.S., walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Bro. Maganga kuwekwa wakfu kama mtawa. Maadhimisho ya Jubilei hii yalikwenda sanjari na kumbukumbu ya Miaka 20 tangu Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Kristo, Jimbo Katoliki la Mogoro lilipotabarukiwa. Na Mapadre wa kwanza kupewa Daraja Takatifu ya Upadre Kanisani hapo walipongezwa pia. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. Kutabarukiwa kwa Kanisa maana yake ni kwamba, Kanisa limewekwa wafu kwa ajili ya kumtolea Mungu: sifa, shukrani na sala, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na waamini kutakatifuzwa. Hivyo basi, Kanisa linakuwa ni nyumba ya Sala, Nyumba ya Mungu na Nyumba ya Ibada. Ni mahali ambapo waamini wanalishwa kwa Neno la Mungu na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Altare iliyotabarukiwa na hivyo kuwekwa wakfu, inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa sababu Altare ni kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ni mahali ambapo waamini wanatolea sala na sadaka zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Kanisa pawe ni mahali pa: amani, usalama na utulivu wa ndani.

Jubilei ya Bro. Maganga imekua ni chachu ya maisha mapya kwa ndugu na jamaa.
Jubilei ya Bro. Maganga imekua ni chachu ya maisha mapya kwa ndugu na jamaa.

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., katika mahubiri yake, amewapongeza Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., kwa kujenga Kanisa hili ambalo kwa sasa limekuwa ni Kanisa la hija. Ameelezea umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu katika huduma ya upendo kwa jirani zao. Askofu Msimbe, amefafanua maana ya Jubilei na umuhimu wake katika maisha ya waamini kama fursa ya kuomba toba, msamaha na upatanisho kwa Mungu na jirani ili kusomba mbele pasi na mawaa. Ni fursa ya kuomba tena baraka na neema katika maisha, wito na utume. Askofu Msimbe, amewashukuru na kuwapongeza Wamisionari wa Damu Azizi kwa ushiriki wao katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima: kiroho na kimwili. Amewataka waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Ujenzi wa Kanisa na hatimaye kutabarukiwa kwa Kanisa la Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Jimbo Katoliki Morogoro, ni wazo lililoanzishwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, ili kupata mahali pa Majandokasisi kufanyia mazoezi ya shughuli za kichungaji. Pili, Wamisionari walipania kusogeza huduma za maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu Kola A na B. Askofu Mstaafu Telesphor Richard Mkude, tarehe 29 Julai 2002 akatabaruku Kanisa la Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yes una kutangazwa kuwa ni Kituo cha Hija, Dekania ya Morogoro mjini. Miundo mbinu ya Kanisa imetengezwa kwa kusoma alama za nyakati. Parokiani hapo ni mahali ambapo, mwamini anaweza kupata fursa ya kufanya tafakari ya kina ya maisha ya kiroho mintarafu historia nzima ya wokovu. Huu ni ubunifu mkubwa uliofanywa na Padre Vincent Boselli, “Mjomba” kwa kusoma alama za nyakati. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre, amekumbukwa pia Padre Basil Ndeshingiyo, C.PP.S ambaye ametangulia mbele ya haki, akiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele!

Jubilei Tanzania
02 August 2022, 16:30