Askofu Msonganzila: Umuhimu Sensa ya Watu na Makazi Nchini Tanzania 2022: Jitokezeni!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sensa ya watu na makazi ni zoefu linalofanyika kila baada ya miaka kumi. Lengo ni kupata idadi ya watu wote waliopo nchini Tanzania ambapo taarifa zai za kijamii na kiuchumi hukusanywa. Sensa pia hukusanya hali ya makazi ya watu hao. Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa tarehe 23 Agosti ambayo ni siku ya Sensa na Makazi ya Watu nchini Tanzania iwe ni siku ya mapumziko, ili Watanzania wawepo majumbani, waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo husika. Waziri mkuu ametoa tamko hilo, Jumatano tarehe 17 Agosti 2022 kwenye kikao cha saba cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amesema kutokana na uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais, anaamini zoezi la sensa ya watu na makazi litaenda vizuri kama lilivyopangwa. Mapema, Waziri Mkuu alipokea vishikwambi 600 kutoka kwa Balozi wa Korea Kusini, Mhe. Kim Sun Pyo vyenye thamani ya shilingi milioni 202. Pia alipokea fulana 1,759 zenye ujumbe wa kuhamasisha sensa zenye thamani ya sh. milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Serikali wa Benki ya NMB, Bw. William Makoresho ambaye alikabidhi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo. Wajumbe wa kikao hicho walijulishwa kwamba utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebainisha kuwa uelewa wa wananchi kuhusu zoezi zima la sensa umefikia asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 96 ya Juni, 2022.
Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anabainisha umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na jinsi ambavyo mchakato huu unavyoweza kusaidia maboresho ya huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na: Kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 kwa kupata taarifa za msingi za mwenendo wa idaidi ya watu, kijamii na kiuchumi; idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote; Kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi; Taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; na msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa ya Watu na Makazi zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa. Mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa; Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.