Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika XV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika XV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika XV ya Mwaka C: Injili ya Msamaria Mwema: Huruma

Huruma ni daraja inayomkutanisha Mungu na waja wake. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kupyaisha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni shuhuda na mhudumu wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu wa Mungu mintarafu Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu.

Na Padre Efrem Msigala, OSA., - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka C ya kipindi cha kawaida cha Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu inayopaswa kupenya katika sehemu mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Huruma ni daraja inayomkutanisha Mungu na waja wake, kiasi cha kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kupyaisha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni shuhuda na mhudumu wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu wa Mungu mintarafu Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Huruma ni msingi thabiti wa uhai na maisha ya Kanisa unaopaswa kujidhihirisha katika shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Kanisa linatumwa kumwilisha huruma na upendo katika maisha na vipaumbele vyake. Leo tunamwadhimisha Mwenyezi Mungu aliye karibu nasi katika: Sala, Neno lake, Sakramenti na jirani zetu. Kama sura ya Mungu asiyeonekana, na kama Msamaria Mwema, Kristo yuko karibu nasi katika hali zote za maisha. Kwa hiyo, kanisa linatuhimiza kukiri uwepo wa Mungu katika Neno lake, na kwa jirani zetu. Ndivyo alivyofanya yule msamiaria kumsaidia mtu aliye katika shida.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu

Somo la kwanza kutoka kitabu cha kumbukumbu la Torati 30;10-14 ni sehemu ya ujumbe wa kuaga, na maagizo ya mwisho ya Musa kwa watu wake siku zake za mwisho. Ujumbe huu unakazia umuhimu wa kudumu na Mungu kupitia Neno lake. Yaani kuishi sawasawa na amri zake katika maandiko matakatifu. Kupitia somo hili Musa anatukumbusha kwamba Mungu yu hai, na yuko karibu nasi kila wakati katika Maneno yake. Anasema: “… Kwa maana sheria hii si nje ya nguvu zenu wala nje ya uwezo wenu kuifikia…” Kwa hiyo, ni lazima tumtafute katika maandiko kwa kumwomba Roho Mtakatifu atie nuru macho ya akili zetu (Efe 1:18). Pia tumeitwa kutii na kuishi kwa Neno kwa sababu, ndilo chemchemi ya uzima. Mungu amejifunua kwetu kikamili katika Neno lake, na ni wale tu wanaofanya jitihada za haraka watampata. Pamoja na hayo, Zaburi ya leo inatuhimiza hivi: “Mtafuteni Bwana, na mioyo yenu itafufuka.” Njia rahisi zaidi ya kuwa karibu na Mungu ni kwa kuliishi Neno lake. Katika somo la pili kwa wakolosai 1:15-20, Paulo anatukumbusha pia jinsi Mungu alivyo karibu nasi. Kupitia Mwanawe Yesu Kristo, anasema: “mfano asiyeonekana wa Baba asiyeonekana”. Mungu alikuja kukaa kati yetu. Mungu alinena Neno lake, naye akawa halisi kati yetu. Kwa hiyo, Paulo anatukumbusha kwamba Mungu aliamua kukaa nasi kwa njia ya Yesu Kristo ili atupatanishe na yeye mwenyewe.

Katika injili ya Luka 10:25-37, Yesu alimwelekeza kijana huyo kwenye maandiko aliyetaka kujua ni mambo gani afanye ili kurithi uzima wa milele, kutokana na upendo kwa jirani hivyo alihitaji kujua jirani ni nasi hasa. Kwa kufanya hivyo, Yesu anajaribu kumfanya aelewe kwamba, Mungu angeweza kupatikana katika Neno lake ambalo liko karibu naye. Kwa hiyo kumpenda Mungu ni kupenda Neno lake. Alisisitiza zaidi hili kwa kusimulia hadithi ya Msamaria Mwema. Neno la Mungu limetajwa kama mtu katika Msamaria Mwema katika injili ya leo. Wasamaria walikuwa wazao wa Wayahudi kutoka sehemu ya Kaskazini ya nchi, ambao walikuwa wameoana na Wasio Wayahudi na hawakuabudu huko Yerusalemu. Na wakawa hawapendwi na wala kuchangamana na Wayahudi. Sasa Msamaria anamwendea yule mtu aliyejeruhiwa na anasafisha majeraha yake, anamweka juu ya mnyama wake mwenyewe. Anamhangaikia kwa namna yo yote ile ili huyu myahudi aliyevamiwa na majambazi apone. Anamuhudumia bila kujali kabila au taifa. Anatumia gharama zake zote. Kwa mfano huo  Yesu anabomoa matarajio yote ya mipaka. Kumtazama jirani kwa upana zaidi. Bila kujali matabaka ya kidini, kabila, rangi, jinsia na kadhalika. Yesu anapomuuliza mwanasheria ambaye alikuwa jirani katika hadithi hiyo, mwanasheria hawezi kutaja kuwa aliyekuwa karibu na yule aliyejeruhiwa ni Msamaria. Anachosema tu ni kwamba yule aliyemwonea huruma na kumtendea kwa rehema. Na Yesu anamwambia mwanasheria nawe nenda kafanye hivyo hivyo.

Jirani yangu ni yeyote yule aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu
Jirani yangu ni yeyote yule aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu

Neno la Mungu ni Yesu mwenyewe, ambaye anazungumza nasi, na Yesu ambaye yuko karibu nasi daima kama Msamaria Mwema. Injili ya leo pia inatuonesha njia nyingine ambayo Mungu yuko karibu nasi. Hiyo ni, kwa jirani yetu. Akiwa bwana mnyenyekevu, anapatikana kwetu siku zote kwa njia na vitu rahisi. Yuko karibu nasi katika maandiko, katika masikini, kwa wenye haki, kwa wacha Mungu, kwa waliotengwa, kwa wagonjwa, na kwa wanyonge. Kama Msamaria Mwema, tukimtafuta Mungu katika haya, tutampata. Msamaria mwema alimwona Mungu ndani ya mhathirika na hivyo akachochewa kumsaidia. Msamaria Mwema anawakilisha wale wanaomtafuta Kristo katika wanyonge, waliojeruhiwa, na maskini waliopondeka na kuvunjika moyo. Anawakilisha wale wanaojali majirani zao na waliojeruhiwa. Pia, anawakilisha Kristo ambaye ni mwepesi daima kuja kutusaidia tunapokuwa dhaifu, tunadharauliwa, na tumeachwa. Yeye yuko tayari kila wakati kutusaidia kupona kutokana na majeraha yetu, na yuko karibu sana kututunza, na kutuponya.

Dominika 15
06 July 2022, 15:21