Tafakari Dominika 17 Mwaka C wa Kanisa: Baba Yetu Ni Sala Ya Kikristo!
Na Padre Nikas Kiuko, - Mahenge, Tanzania
Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi zake kuhusu Fumbo la Maisha ya Sala anasema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwahimiza wafuasi wake kukuza na kudumisha ari na moyo wa sala dumifu, kwa kuwakumbuka na kuwaombea ndugu zao hasa wale wanaoishi katika mahusiano magumu na Mwenyezi Mungu! Wafuasi wa Kristo wajifunze kusamehe na kusahau kama wanavyosamehewa dhambi zao na Baba yao wa mbinguni. Sala ya Baba Yetu ni mfano bora wa Sala ya Kikristo! Mtakatifu Paulo hazungumzii sana kuhusu Sala ya Baba Yetu, lakini, muhtasari wa Sala hii unafumbatwa katika neno moja tu “Aba” yaani “Baba”. (Rej. Rm. 8: 15 na Gal.4:6). Katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka, Kristo Yesu, anazima kiu ya Mitume wake kwa kuwafundisha Sala ya “Baba Yetu” inayojulikana pia kama “Sala ya Wakristo” (Lk. 11:1). Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa Sala ya Kikristo. Waamini hawawezi kamwe kusali vyema pasi na nguvu ya Roho Mtakatifu anayesali pamoja nao. Roho Mtakatifu anawawezesha kusali kama wafuasi wa Kristo na waana wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini “kuchota” utajiri wa chemchemi ya maisha ya sala ambao umeandaliwa na Kristo Yesu, kiasi cha kuanzisha majadiliano ya upendo na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu alikuwa na mitindo mbali mbali ya kusali, kwa mfano aliweza kusali kwa kusema: “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha."
Kwa nini tusali? Mwinjili Luka tofauti na wengine amejikita zaidi kueleza Maisha ya Yesu yalikuwa ya sala (Luka 3:21, 5:16, 6:12 na Luka 11:1 ameianza kwa kusema Yesu alikuwa akisali. Alipo maliza kusali, mmoja ya wanafunzi wake akamwendea akimuomba amfundishe kusali kama Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Yohane Mbatizaji alikuwa mtangulizi ya Yesu, hivyo kuna mambo mengi yanamfanano hata katika utume wao. Yohane aliwafundisha wafusi wake sala na Yesu leo anawafundisha wafuasi wake namna yak usali. Yohane aliwafundisha sala gani? Maandiko Matakatifu hayaweki wazi sala ya Yohane kwa wanafunzi wake. Lakini aliwaalika wafuasi wake watubu na kuiamini Injili, wadumu katika msamaha na wapendane. Wanafunzi wa Yohane wengine waliomfuata Yesu walipo ambiwa tazama Mwanakondoo wa Mungu na wakamuuliza unakaa wapi? Yesu akawaambia njooni nanyi mtaona. Katika kukaa na Yesu wanamwomba wafundishwe kusali. Sala ya Yesu imejikita katika kumtukuza Mungu Baba, na kumwomba msamaha katika makosa yetu. Katika sala hiyo, Yesu anawaalika wafuasi wake wawe na mahusiano mazuri na Mungu Baba yetu aliye mbinguni. Anawaalika watu wamwite Mungu “Baba” kama yeye anavyomwita. Baba kama mzazi mwenye upendo kwa wanae. Tunaposema jina lako litukuzwe na ufalme wake ufike, ina maana kuna mkate wa kila siku na msamaha unakuwa kwa vitendo. Na Mungu anatutoa katika majaribu makubwa
Kwa nini tusali? Mbona wanaosali wengi wanamahangaiko makubwa kuliko wasiosali? Tangu Agano la Kale wazee wetu walisali. Walisali walipo kuwa na furaha, walipo kuwa na huzuni, walisali walipo kuwa na shida walisali walipo kuwa katika amani, walisali kuombea taifa lao na walisali kuyaombea mataifa mengine walipopotea amani. Sala zilitumika kuomba nguvu za kimungu, uponyaji na huruma ya Mungu. Mfano Ibrahimu aliombea Sodoma na Gomora ambako watu wake walikuwa wana maisha ya anasa, rushwa, ndoa za jinsia moja, mauji ya vikongwe, ushirikina na kutoshika amri za Mungu. Ibrahimu alisali Mwanzo 18:16-33. Ibrahimu alisali kuomba huruma ya Mungu. Ni mwaliko hata sisi tunasali kuombea mataifa ambayo watu watu wake wamemsahau Mungu. Sala inatumika katika kutupatanisha wanafamilia (Mwanzo 32:9-12). Yakobo alichukua baraka ya Esau kisha akakimbia mbali na akakaa huko miaka mingi akiogopa kuuwa. Yakobo aliko huko akasali niokoe ee Mungu katika mkono wa Esau namuogopa atakuja na kutendea uovu. Wanafamilia tukimbilie nguvu ya sala, tuziombee famila zetu, tuwaombee wapenzi wetu wanapo tusaliti, tuombeane ili kukaribisha nguvu ya Mungu. Mungu akawakutanisha n Yakobo na Esau wakakumbatiana, akamkaribisha kwa furaha na amani na Maisha yanaendelea.
Mara nyingi tunaapizana, tunakasirikiana mtu na mzazi wake mtu na mke wake mtu na rafiki yake tukumbuke kusali. Tunasali ili kuwaombea watu watubu na kumwongokea Mungu. Musa alivyo panda mlimani Wanawaisraeli wakajitengenezea mungu wa dhahabu na kusema Musa kachelewa mlimani sasa huyu ndiye Mungu wetu. Hasira ya Mungu ikawaka kwa wanaisraeli na alitaka kuliangamiza taifa zima. Kutoka 32 Musa alipiga magoti na kusali kuombea taifa, kwa dhambi waliyo tenda dhambi. Ee Mungu nakuomba uwasamehe dhambi zao. Kutoka 32: 32. Tunasali ili Mungu abariki familia zetu 1Samweli 1: 11. Sala ya Hana. Alikuwa mke wa Elikana, alipendwa sana lakini hakubaitika kupata mtoto. Mke wapili wa Elikana alikuwa Penina alikuwa na uzao wa haraka. Akaanza kunyanyapaa Hana, naye hana hakuwa na furaha, amani na upendo. Hivyo akapiga magoti na kumuomba Mungu. Ee Mungu wa Majeshi ukinipatia mtoto wa kiume nitamtoa awe mtumishi Maisha yake yote (1samweli 1:11). Naye akapata mtoto na Mungu akaibariki familia ikawa ya amani. Tusali kumuomba Mungu katika shida zetu. Tunapo kuwa katika mahangaiko tumkumbuke Mungu kwa sala.
Tunasali ili kurudisha mahusiano na Mungu. Yona 2. Sala ya Yona “Nilimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu niliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. Mungu yko kila mahali. Tukimkimbilia yeye hatatuacha, tukimkimbia atatutafika mbali. Mtakatifu Augustino anasema kadiri unavyo jikabidhi kwa Mungu ndivyo utakavyojifunza upendo wake, wema wake na ndivyo utakavyoweka matumaini kwake. Katika maisha yake alikiri kuwa najikuta niko mbali na Mungu kuliko Mungu alivyo kuwa karibu nami. Bwana tufundishe kusali. Tusali katika famili zetu, jumuiya ndogo ndogo na kanisani. Sala binafsi na sala za jumuiya ni muhumu. Sala za mishale, zaburi na tenzi, bila kuacha ibada kwa Bikira Maria. Sala za watakatifu wasimamizi wa familia na jumuiya. Waamini tujitahidi kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali mara kwa mara katika maisha yetu. Tujibidiishe kuwafundisha wengine kusali vizuri zaidi, tukimwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya pekee katika maisha yetu.