Masista Wamisionari wa Ekaristi Na Uinjilishaji Mpya: Jimbo Kuu la Arusha, Tanzania
Na Sr. Gisela Upendo Msuya, Arusha, - Tanzania
Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Kuu la Arusha, Tanzania, tarehe 20 Julai 2022 anatarajia kuongoza Ibada ya Misa takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mtume, Baraa Moshono, Jimbo kuu la Arusha, ambamo Masista wanne Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya, wataweka nadhiri zao za kwanza. Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya, lilianzishwa rasmi mnamo tarehe 02 Februari 2016 katika Jimbo Kuu Katoliki la Arusha nchini Tanzania na Sr. Gisela Upendo Msuya. Kwa sasa Shirika linao Masista 9, wanovisi wa mwaka wa kwanza 7, wanovisi wa mwaka pili ni 4, wapostulanti ni 10 na watakaji ni 7. Hata katika uchanga wake, Shirika linaendelea kuchakarika usiku na mchana ili kujitegemea pamoja na kuwaendeleza vijana katika fani mbalimbali za maisha. Ni katika muktadha huu, Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya, linaendelea kukamilisha Chuo cha Ufundi Stadi cha Jitegemee, “Jitegeme Technical School.” Chuo kinatarajia kutoa kozi ya ufundi seremala, chuma, ushonaji, maarifa ya nyumbani pamoja na computer.
Utangulizi: Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mwokozi wetu, Kristo Yesu katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake Azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibiarusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo na ufufuko wake: Sakramenti ya utakatifu (Sacramentum pietatis), ishara ya umoja, kifungo cha mapendo karamu ya Pasaka “ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa amana ya uzima wa milele”. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Kwa sababu hiyo, Mama Kanisa anajibidiisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie maadhimisho ya fumbo la imani kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala.
Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao ili hatimaye, Mungu awe yote katika wote. Rej. SC. 47-49. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha. Shirika letu la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya, lilianzishwa rasmi mnamo tarehe 02-02-2016 katika Jimbo Kuu Katoliki la Arusha. Mwanzilishi wa Shirika hili ni Sr. Gisela Upendo Msuya (07/05/1974). Sista huyu, baada ya kujiunga na Shirika la Masista Wakarmeli wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu na kuwa sehemu ya shirika hilo kama mwanamalezi kuanzia mwaka 1991 hadi 1995 alipoweka nadhiri zake za kwanza na baadaye akaendelea na shughuli za Utume kwenye Shirika hilo hilo hadi mwaka 2008.
Ni katika mwaka huo wa 2008 Sr Gisela aligundua kwamba Mungu alikuwa anamwita kufanya utume wa zaidi ya kuwa mtawa wa kawaida kama ambavyo alikuwa tangu kuweka nadhiri za kwanza hadi mwaka huo wa 2008. Bila kusita Sr Gisela aliomba muda wa “sabatical” yaani muda wa kukaa nje ya Shirika la Wakarmeli ili akatafakari zaidi juu ya msukumo na wito aliokuwa anauhisi ndani ya moyo wake ambao daima ulikuwa una msumbua na pia kumtafakarisha juu ya Uinjilishaji Mpya, jambo ambalo kwake halikuwa rahisi kuelewa. Sista alitumia muda mwingi mbele ya Ekaristi Takatifu ili kumwomba Yesu amfunulie ni kitu gani hasa anataka kutoka kwake na kama ni yeye (Yesu) kweli alikuwa akimpatia hayo maono. Baada ya muda wa kutosha wa kutafakari, kuongozwa kiroho, na kushauriwa, na wakati wa Bwana ulipowadia, Sr Gisela alijitosa kimaso maso bila woga wala kusita katika kufanya kazi hiyo ya Mungu na kuanzisha shirika hili jipya kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya. Jina la Shirika (Ekaristi na Uinjilishaji Mpya) linapata chimbuko lake katika wito ambao Sr. Gisela alikuwa anauhisi ndani na ambao aliung’amua baada ya kuwa na muunganiko wa karibu zaidi na Yesu katika Ekaristi Takatifu.
Karama: Karama ya Shirika letu ni Uinjilishaji Mpya; yaani USHUHUDA WA INJILI KWA MATENDO! Hii ni kusema kwamba ili mmsionari wa Ekaristi aweze kupeleka Injili kwa watu ni lazima aongee kwanza na Yesu katika Ekaristi na kuchota neema na nguvu kutoka kwenye hiyo chemchemi ya Ekaristi, ndipo akawatangazie wengine kile ambacho amekiona, yaani Yesu mzima katika Ekaristi; kile ambacho amekisikia kutoka kwa Yesu (Injili), ili kwa ushuhuda huo wa maisha yake aweze kumsaidia mwanadamu kujikomboa kiroho, kimwili na kimaisha kwa namna mbali mbali kwakuzingatia mafundisho ya Injili Yesu anayosema kwamba “Roho wa Bwana Mungu yu juu yangu kwa maana amenituma kuwahubiri maskini Habari Njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa na vipofu kupata kuona tena” (Lk 4:18). Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu ndiyo inayo tusukuma sisi wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya kujikita pia katika shughuli za kijamii ambazo zinaweza kumkomboa mwanadamu aliyezama katika lindi la umaskini na ujinga, na hivyo kumfanya awe kama mfungwa kwa sababu ya hali yake duni ya Maisha. Hali duni ya maisha kamwe haiwezi kumkomboa mwanadamu kiroho kwani, kama hawezi kupata mahitaji yake ya kimwili hataweza kufikiria wala kuhangaikia mahitaji yake ya kiroho. Mwanadamu akiwa na mwili wenye afya hata roho yake itakuwa na afya! Yaani wawe na “uzima tele” (Yoh. 10:10). Hivyo basi, karama ya shirika hili la wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya ni kumnyanyua mwanadamu kutoka katika uhitaji wake: kirho na kimwili kwa njia ya USHUHUDA wa maisha.
CHANGAMOTO: Kazi ya Mungu haikosi changamoto! Hata Yesu Kristo mwenyewe alikutana na changamoto za kutosha katika maisha na Utume wake. Hivyo basi, hata mimi, kama mwanzilishi changamoto nimekutana nazo nyingi hasa katika hatua za mwanzoni mwa uanzilishi wenyewe kama vile: kukatishwa tamaa, kutukanwa, kudharauliwa, kusengenywa na kusingiziwa mengi. Ila yote hayo niliyaona kama sehemu ya uthibitisho kwamba kazi ninayo ifanya ni ya Mungu na si ya binadamu, kwani Ingekuwa kazi ya binadamu, sifa zingekuwa nyingi sana. Kwa kuwa kazi ya Mungu inao wapinzani, tukianzia na yule muovu mwenyewe, basi sikukata tamaa na wala sitakata tamaa, nasonga mbele nikijua kwamba Mungu aliye anzisha kazi yake ndani mwangu, mimi niliye kiumbe dhaifu tu, ataikamilisha mwenyewe. Nje na changamoto hizo binafsi, kuna changamoto zinazotokana na miito.
Mabinti wengi wanaitikia wito wa utawa na wanajiunga nasi, ila misingi mibovu ya familia ambamo baadhi yao wanatoka inasumbua sana katika mchakato mzima wa malezi ya utawa na kazi za kitume. Misingi hiyo mibovu ni pamoja na kutegemea nguvu za giza, ushirikina, hali duni ya maisha iliokithiri kiasi kwamba baadhi ya mabinti wanaona kwamba kujiunga na mashirika katika hali hiyo kuna wahakikishia walau kupata mahitaji yao ya kila siku na sio kumfuasa Yesu. Kazi kubwa hapa ni kulea watu ili waweze kuwa wakweli na wazi juu ya malengo yao ya kujiunga na shirika, kuwafanya wale walioshikamana na imani za kishirikina kuachana nazo mambo ambayo yanachukua muda mwingi kwani sio rahisi kumwaminisha mtu aliyelelewa katika ushirikina kwamba Yesu pekee ndiye tegemeo na mlinzi wa mwanadamu na kwamba hakuna mwanadamu anaweza kumhakikishia mwanadamu mwenzake ulinzi wa kiroho na kimwili kama sio Muumba wake mwenyewe. Lakina pamoja na yote hayo naendelea “Kutweka mpaka kilindini”, na kwa neno la Yesu nitazishusha nyavu! Lk 5:5. Matarajio: Ni matarajio yangu kwamba shirika hili, pamoja na kuwa changa kama mbegu ya haradali, litakua na kukomaa na kuenea ulimwenguni kote katika Utume wake huu wa kumfanya Yesu Kristo aliye hai katika Ekaristi atambulike na kuabudiwa kama Bwana na Mwokozi wa Ulimwengu wote.