Tafuta

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, akitabaruku Kanisa na Altare ya Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio Jimbo kuu la Dar es Salaam. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, akitabaruku Kanisa na Altare ya Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

Askofu mkuu Ruwa'ichi: Jengeni Hekalu la Mungu Kwa Sala, Ibada na Uchaji wa Mungu

Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi tarehe 2 Julai 2022, ametabaruku Kanisa na kuweka wakfu Altare ya Kanisa la Mtakatitu Yohane Paulo II, Ununio, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Amewataka waamini kutambua kuwa kwa Sakramenti ya Ubatizo wameunganishwa na Mungu na kufanywa kuwa sehemu ya Kanisa na Hekalu la Mungu na hivyo wasiruhusu miili yao kutawaliwa na dhambi.

Na Damian Kongwa, -Dar Es Salaam.

Maneno “QAHAL” ed “EKKLESÌA” yaani “Kanisa” lina maana ya “kusanyiko” linaloonyesha mkutano wa wale ambao Neno la Mungu limewakusanya kuunda Taifa la Mungu, na ambao, wakilishwa mwili wa Kristo, nao wenyewe wanakuwa mwili wa Kristo. Kanisa wakati huo huo ni njia na mpango wa Mungu, lililofikiriwa katika uumbaji, lililotayarishwa katika agano la kale, lililojengwa kwa njia ya maneno na matendo ya Yesu Kristo, lililodhihirishwa kwa njia ya msalaba wake wa ukombozi na ufufuko wake, nalo limedhihirishwa kama fumbo la wokovu kwa kumimina Roho Mtakatifu (Rej. KKK 777 – 778). Kanisa linatimilika katika utukufu wa mbinguni kama kusanyiko la wote waishio duniani waliokombolewa (Rej. Ufu 14:4). Mtakatifu Irenaeus anafundisha kuwa paji la Mungu limekabidhiwa kwa Kanisa ambalo ndani yake kimewekwa kiungo na Kristo, yaani Roho Mtakatifu, amana ya kutoharibika, uthibitisho wa imani yetu na ngazi yetu ya kupandia kwa Mungu. Kwa kweli pale lilipo Kanisa, ndipo pia alipo Roho wa Mungu, na pale alipo Roho wa Mungu, ndipo lilipo Kanisa na neema zote. Kristo Yesu “alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote na kujisafishia watu wake wawe milki yake mwenyewe” (Rej. Tito 2:14).

Kanisa la Parokia ya Mt. Yohane Paulo Ununio limetabarukiwa tarehe 2 Julai 2022.
Kanisa la Parokia ya Mt. Yohane Paulo Ununio limetabarukiwa tarehe 2 Julai 2022.

Ni katika muktadha huo, Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, nchini Tanzania, Jumamosi, tarehe 2 Julai 2022, ametabaruku Kanisa na kuweka wakfu Altare ya Kanisa la Mtakatitu Yohane Paulo II, Ununio, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Ruwa’chi amewakumbusha na kuwataka waamini kutambua kuwa kwa Sakramenti ya Ubatizo wameunganishwa na Mungu na kufanywa kuwa sehemu ya Kanisa na Hekalu la Mungu na hivyo wasiruhusu miili yao kutawaliwa na dhambi wala uovu wowote bali wadhihirishe neema za Mungu na ukuu wake siku zote za maisha yao. Akizika masalia ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Altare, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema Mtakatifu Yohane Paulo II anakuwa mwombezi na msaada wa daima kwa wanaparokia wote katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ibada hiyo ilihudhuriwa na Kardinali Polycarp Kadinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mapadre, Watawa, Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.

Akisoma taarifa fupi ya Ujenzi wa Kanisa mbele ya Askofu mkuu, Katibu wa Halmashauri ya Walei Parokia Dr. Vandelin Tarmo amesema mchakato wa ujenzi wa Kanisa ulianza rasmi mwaka 2010 na mnamo tarehe 11 Mei 2014 Kardinali Polycarp Pengo aliweka jiwe la msingi tukio ambalo liliwasukuma waamini kuzidi kujitoa katika kuchangia ujenzi wa Kanisa. Hadi kukamilika kwake Kanisa hilo kwa zaidi ya asilimia 95% limejengwa kwa fedha, michango na majitoleo ya wanaparokia wenyewe hali inayodhihirisha mwamko mkubwa, umoja na mshikamano wa wanaparokia katika kulitegemeza Kanisa mahalia.   Kwa upande wake Mheshimiwa George Simbachawene Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu aliyemwakilisha mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amewapongeza waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio kwa kukamilisha ujenzi wa Kanisa na kuwaomba wazidi kujitoa bila kuchoka katika kuchangia maendeleo, ustawi na mafao ya Kanisa zima.

Kardinali Pengo aliweka Jiwe la Msingi tarehe 14 Mei 2014
Kardinali Pengo aliweka Jiwe la Msingi tarehe 14 Mei 2014

Padre Emmanuel Haule, CM, Paroko wa Parokia ya Yohane Paulo II, Ununio kwa niaba ya wanaparokia wote amemshukuru Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi kwa kukubali kutabaruku Kanisa hilo lililojengwa kwa kipindi cha takribani miaka 12. Pia amewashukuru Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., kwa kuratibu na kusimamia zoezi la upatikanaji wa viwanja na hatimaye kuanzisha ujenzi wa Kanisa. Shukrani za pekee kwa Padre Mathew Twimanye - CM, Padre Ahadi Mgedzi - CM na waamini wote wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio kwa kujitoa kwa hali na mali katika kuratibu, kusimamia na kuchangia ujenzi wa Kanisa lililotabarukiwa. “Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele…! Amina.” (Rej. Efe 3:20-21).

Ununio Dar es Salaam

 

06 July 2022, 15:51