Tafuta

Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ni chombo cha uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika ushuhuda na mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ni chombo cha uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika ushuhuda na mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili 

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Jumuiya Ndogondogo za Kikristo

Mwaka 2024, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Jumuiya hizi ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani: Koinonia, Kerygma na Diakonia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu” uliofunguliwa rasmi tarehe 10 na unahitimishwa tarehe 18 Julai 2022, Jijini Dar es Salaam kwa kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 270. Kauli mbiu ya maadhimisho haya inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” AMECEA inabainisha kwamba, kuna mambo makuu matatu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza yaani: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Padre Stefano Kaombe wakati wa Misa ya Ufunguzi wa Mkutano wa AMECEA
Padre Stefano Kaombe wakati wa Misa ya Ufunguzi wa Mkutano wa AMECEA

Kimsingi, wajumbe wamekazia: Ushuhuda wa imani tendaji katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Umuhimu wa kulea dhamiri nyofu ili kuendeleza kazi ya uumbaji kwa kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na wadau mbalimbali kushirikiana na kushikamana katika kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kwa sababu haya ni mambo tete katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu Charles Sampa Kasonde, Rais wa AMECEA amewataka wajumbe kuongozwa na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” katika kujitathmini, kama Kanisa Ukanda wa AMECEA, ili kukabiliana kikamilifu na masuala ya haki, amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kusikilizana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Utunzaji bora wa mazingira anasema Askofu Kasonde ni sehemu ya uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko

Wakati huo huo AMECEA imetambua na kukiri mchango wa Padre Joseph Graham Healey wa Shirika la Wamisionari wa Maryknoll aliyezaliwa tarehe 29 Aprili 1938 na kwa sasa ana umri wa miaka 84, katika maisha na utume wake kwa Kanisa la Afrika Mashariki na Kati. Padre Joseph Graham Healey, “Mwana MAC na Mwanajumuiya halisi” amejipambanua sana kuwa ni kati ya wataalam wabobezi wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zilizoanzishwa na AMECEA kama sehemu ya mbinu mkakati wa Uinjilishaji Afrika Mashariki. Ni jaalimu na mtafiti nguri katika tasnia ya mawasiliano ya jamii Afrika Mashariki na Kati. Ameandika na kuchapisha vitabu vingi kama sehemu ya uinjilishaji Barani Afrika. Itakumbukwa kwamba, ujenzi na uimarishaji wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni changamoto ya kichungaji iliyovaliwa njuga na Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA tangu mwaka 1973 na kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kunako mwaka 1974. Kumbe mwaka 2024, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ni shule ya uinjilishaji wa kina.
Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ni shule ya uinjilishaji wa kina.

Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani” Koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia”. Lengo kuu ni kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Kimsingi, Jumuiya ndogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, zinazosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

AMECEA DSM 2022
13 July 2022, 17:33