Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA:Kard Tagle ahimiza umuhimu wa kusaidiana!
Na Angella Rwezaula – Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Kardinali Luis Antonio Tagle amewaomba waamini Wakristo ulimwenguni kote kuwa na upendo usio na masharti kwa ajili ya kazi ya viumbe vyote vilivyoumbwa na Mungu. Ushauri huo ameutoa wakati wa ufunguzi rasmi wa Misa ya Mkutano wa 20 wa Baraza la Maaskofu Afrika Mashariki katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar Salaam-Tanzania Dominika tarehe10 2022. Mkutano huo unaongozwa na mada kubwa mno juu ya “Utunzaji wa mazingira kwa ajili ya Maendeleo endelevu ya Mwanadamu”kutoka Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko wa Laudato Si.
Misa iliudhuriwa na maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya Dar Es Salaam. Kardinali Tagle aliwahamasisha watu wenye mapenzi mema kupenda kazi za ajabu za Mungu kupitia kazi yake ya uumbaji wake. Kardinali Tagle akiwashukuru waamini waliokusanyika katika uwanja huo alisema Wakristo lazima wawe na moyo wa kujaliana wao kwa wao na kwa viumbe vyote vilivyo hai ambavyo Mungu ameumba. Ameomba wajiulize ni kwa nini siku hizi wengi wanajali kidogo. Na zaidi aliongeza kuuliza kwa wenzi wa ndoa kwamba wale walio kwenye ndoa, wanapotazamana mume au mke wanaona sura ya Mungu au kitu kingine?”
Kwa njia hiyo alisisitiza kushughulikia kiini cha matukio ya mazingira yanayoletwa na uharibifu wa mazingira. “Tunahitaji kujadili chanzo cha uharibifu wa mazingira ili kuwa na maazimio madhubuti baada ya Mkutano, la sivyo tutakuwa na maazimio ya vipodozi kutoka katika mkutano. Hii ina maana ya kutofikia maamuzi stahiki ambayo hayadumu badala ya kushughulikia kwa dhati utunzaji bora wa mazingira nyumba yetu ya pamoja. Kardinali Tagle akiendelea na mahubiri yake aligusia hata suala la migawanyiko na chuki kati ya viumbe na binadamu kwamba inatokana na kutotunza mazingira na kusababisha watu kutokuwa na uwezo duniani.
Kardinali alibainisha kuwa ukosefu wa utunzaji wa mazingira umesababisha migogoro, vurugu na migawanyiko duniani, na pia hata kutaja athari za mazingira kama vile mafuriki, vimbunga, matetemeko na mvua za kutisha. Hata hivyo alishukuru kwamba Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wakleri, watawa na walei kutoka Nchi za Afrika Mashariki wamekusanyika nchini Tanzania ili kutangaza Habari Njema ambayo binadamu anahitaji kukutana kwa pamoja.
Kutotunza mazingira kunajidhihirisha katika kutojaliana kama inavyoonekana katika migogoro mingi ulimwenguni. Lakini Mungu anataka tuwe karibu zaidi sisi kwa sisi kwa sababu ndani ya Yesu, na Roho Mtakatifu Mungu yuko karibu nasi. Na tunapaswa kuvumiliana sisi kwa sisi, alisistiza sana Kardinali. Akirudia katika masomo matatu yaliyoongoza siku hiyo, somo la kutoka la Kumbukumbu la Torati (30:10-14), Wakolosai (1:15-20) na Luka (10:25-37), alikumbusha jinsi ambavyo masomo yote walizungumzia kuhusu ukaribu wa Mungu kwa kazi ya uumbaji na ubinadamu. Kardinali aliuliza kwa nini wanadamu wanapaswa kuharibu uumbaji ikiwa kila kitu kilichoumbwa kisichoonekana na kinachoonekana kina kuwapo kwa Kristo?
Wakati huo huo na Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan Kasini, Askofu Mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen wakati wa kutoa neno lake, alipongeza uanachama wa Shirikisho la Maaskofu Afrika Mashariki AMECEA kwa ushirikiano wake kati ya Wakatoliki kutoka eneo hilo. Kwa kuonesha ushirikiano huo Balozi wa Kitume alitaja matumizi ya lugha za kienyeji kwa ajili ya sala wakati wa Misa Takatifu kama ishara ya kuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa wanachama katika eneo lote la AMECEA. Hata hivyo alisema kukosekana kwa lugha ya kiarabu wakati wa maombi, kwa sababu alisema ndiyo lugha inayozungumzwa pia Sudan Kusini anakotoka. Hiyo ni kutokana na kwamba wakati sala ya waamini zilisikika lugha mbali mbali za Makanisa ya Afrika Mashariki kama vile: Chichewa- Malawi, Hamariki - Ethiopia, Kiswahili-Tanzania, Tigrinya-Eritrea Zambia, Runyoro- Uganda, Kiingereza. Wakati wa matoleo ulikuwa mzuri sana, wanaumea na wanawake wakicheza na kupeleka vipaji.
Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga anayo matumaini kwamba Mkutano wa 20 wa AMECEA utaendelea vizuri kwa kuwa anaamini kuwa neema za Mungu zitaambatana na mashauri hayo katika muda wote wa maskofu. Askofu Mkuu Nyaisonga alisema hayo alipokuwa akitoa neno la shukrani wakati wa misa takatifu “Tumemaliza adhimisho la Misa Takatifu inayoadhimisha uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA hapa Tanzania. Neema tulizopata kutoka katika Misa Takatifu zitatusaidia katika kufanya maazimio mazuri wakati wa kikao hiki”. Askofu Mkuu Nyaisonga aliwashukuru wale wote walioshiriki Ibada ya Misa Takatifu, kwa namna ya pekee alitoa shukrani kwa Askouf Mkuu Mstaafu wa Jimbo la Nairobi Kenya Kardinali John Njue na mhubiri wa siku Kardinali Antonio Tagle.
Askofu Mkuu alibainsha jinis ambavyo misa hiyo ilikuwa ya kushangaza na kwamba mshereheshaji mkuu aliadhimisha misa kwa taadhima. Akimgeukia Kardinali Tagle, Askofu Mkuu Nyaisogna alisema kuwa amekidhi kiu na matarajio ya waamini katika mahubiri aliyotoa kwa mtindo wa moja kwa moja. “Asante ujo wako, ushiriki kikamilifu wa makadinali wote, maaskofu wakuu, maaskofu, mapadre, watawa na waamini wote ulitoa msisimuo, asante na pongezi”. Alihitimisha kwa kuwatakia wajisike vema nchini Tanzania wanaposhiriki Mkutano huo. Kati ya waliotoa salamu ni Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar Es Salaam Tanzania, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, na Mwenyekiti wa AMECEA Charles Kasonde,