Tafuta

Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo na msamaha. Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo na msamaha. 

Ibada Kwa Damu Azizi ya Yesu ni: Mto wa Rehema, Shule ya Utakatifu

Damu Azizi ya Kristo ni: mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo na msamaha. Damu Azizi ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kileloe cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Dickson Simon Komba, C.PP.S. – Roma.

Mama Kanisa katika huruma yake kuu, ametenga mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo na msamaha. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni Ibada ambayo inaenezwa kwa namna ya pekee kabisa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC, Mashirika ya Kitawa pamoja na waamini walei. Fumbo la upendo wa Kristo Yesu limekuwa ni kivutio kikubwa cha waamini na waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa kama vile Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mathias, kiasi kwamba, fumbo hili la upendo na huruma ya Mungu limekuwa ni msingi wa maisha na utume wa Mashirika haya. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kileloe cha maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha Kristo Yesu kuwakirimia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitambua kama watu waliotiwa muhuri ili kushiriki katika utume wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni mwanga na baraka inayofufua na kupyaisha; mwanga unaoponya na kumweka mtu huru; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Papa Francisko: Waamini watambue dhamana na wajibu wao wa kutangaza Injili ya matumaini.
Papa Francisko: Waamini watambue dhamana na wajibu wao wa kutangaza Injili ya matumaini.

Waamini wawe tayari kuwashirikisha jirani zao, tunu na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ni mtakatifu wa Mungu anayestahili kuonjeshwa upendo wa dhati. Rej Evangelii gaudium 273-274. Padre Terenzio Pastore, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi Kanda ya Italia, anakazia utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu, katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza na kutenda; kusamehe na kusahau sanjari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro, kinzani na vita kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni ajenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake unaofungamanishwa na maisha ya binadamu.

Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu. Ni katika muktadha huu, Padre Terenzio Pastore, kama sehemu ya kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre, ameamua kuandika Kitabu na mapato yote yanapania kusaidia katika kugharimia mradi wa maji safi na salama kwa watu wa Mungu Mkiwa, Wilayani Manyoni, Mkoani Singida. Koinè ni ushirika wa wanafamilia ya Damu Azizi ya Yesu, wenye lengo la kushirikishana tone la upendo wa Damu Azizi ya Yesu. Ushirika huu, unajumuisha mapadre, masister na watu wote wenye kuisifu, kuiabudu, kuitukuza, kuiheshimu, kuishukuru, kuithamini na kuitangaza kwa watu wengine Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tarehe 2-3 Julai 2022 katika Hoteli ya Antonella, Pomezia, iliyoko Jimbo kuu la Roma, Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia, liliitisha ushirika huu wa Damu Azizi ya Yesu na kushirikishana tunu bora za Damu Azizi ya Yesu. Tukio hili linaadhimishwa Mwezi Julai kwa sababu ni mwezi uliotengwa maalumu kwa ajili ya kutafakari upendo na huruma ya Munu inayobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Yesu.

Utambulisho wa wafuasi wa Kristo katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Utambulisho wa wafuasi wa Kristo katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Katika siku hizi mbili ushirika huu wa Damu Azizi ya Yesu, ulitafakari upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katka Damu Azizi ya Yesu kwa kutoa mafundisho ya Kibiblia kutoka kwa mapadre walioandaliwa, pamoja na kusikiliza au kutoa mang’amuzi kwa waamini walei kutoka maparokiani au kutoka sehemu za kazi (maofisini), kama ushuhuda wa jinsi wanavyojitahidi kuiishi tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Huu ni ushuhuda wa ushiriki katika Maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalofumbatwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Tarehe 2 Julai 2022 siku ya ufunguzi, mafundisho ya kibiblia yalitolewa na padre Roberto Pasolini. Ujumbe mzito wa mafundisho yake ulikuwa ni kanisa: nyumba yenye malango wazi. Katika maelezo yake, mtoa mada alisema kuwa “watu wote kwa ubatizo wanaalikwa kuingia kwenye nyumba ya Mungu yaani Kanisa, Kanisa kama jengo na pia Kanisa kama moyo wa mtu.” Katika Biblia, fundisho hili tunalipata pale mtume Fillipo alipomsaidia mpagani kuyaelewa maandiko aliyekuwa anasoma. Mtume Fillipo alimuuliza “unaelewa unachosoma, yeye akajibu nitaelewaje pasipokuwa na mtu wa kunielewesha.” Padre mtoa mada alisisitaza kuwa, nyumba hii ya Mungu, yaani Kanisa kama jengo na kanisa moyo, siku zote hutoa upendo na matumaini ambayo ndiyo hayo hayo tunapaswa kuyapeleka kwa wengine waliokuwa nje ya Kanisa jengo na nje ya Kanisa moyo.

Kanisa-nyumba yenye milango wazi tafsiri yake ni kwamba, Mkristo aliyebatizwa na akapata mafundisho sahihi ya Kanisa yaliyosheheni utume na matumani, huyo pia anapaswa kutoka nje ya Kanisa jengo kwa ajili ya kuwahubiria na kuwashuhudia wengine hayo aliyopata ndani ya Kanisa Katoliki. Vile vile mtu huyo aliyepata mafundisho sahihi ya KanisaKkatoliki anapaswa kutoka nje ya Kanisa moyo kwa ajili ya kuwakarimu wengine au kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili yaani kuwajali wahitaji, au kwa maneno mengine kujibu kilio cha Damu kutoka kwa watu wa nyakati hizi.  Katika kutoka nje ya Kanisa Moyo, mtoa mada, alimshukuru sana na kumpongeza Padre Terenzio Pastore Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S Kanda ya Italia, kwa maamuzi yake ya kuandika kitabu kwaajili ya kupata fedha itakayosaidia kuchangia gharama za mradi wa maji safi na salama ambao hapo ulipangwa kutekelezwa kwenye Kijiji cha Chinangali, kilichoko Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida, sasa umeanza kutekelezwa kwenye Kijiji cha Mkiwa, kilichoko Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida.

Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu
Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu

Huu ndio ushuhuda wa Kanisa moyo linalotoka moyoni, kusoma alama za nyakati, kwa kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha Damu, kwa kuguswa na mahitaji halisi ya watu wa Mungu katika eneo husika. Hii ni faida ya kiroho na kimwili. Nia hii njema inayosimikwa katika mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, ilungwa mkono na wajumbe waliohudhuria pamoja na watu wa vitabu, kuchangia fedha kwa ajili ya kufanikisha mradi wa maji Kijijini Mkiwa, kama sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji yam tu: kiroho na kimwili. Kwa upande wake Padre Roberto Pasolini katika tafakari yake, alitoa mwaliko kwa watu wote wenye kumfahamu Kristo Yesu, kumbeba na kumpeleka kwa watu wengine kwa ajili ya kuendeleza pendo na tumani la Mungu kwa watu wote. Itakumbukwa kwamba, uponyaji wa maisha ya kiroho huanza kwanza kabisa kwa kusikilizwa kama alivyofanya Kristo Yesu kwa yule Mwanamke Msamaria pale Kisimani, au kama Kristo Yesu alivyojibiwa na yule mtu aliyekuwa amepooza pale Kisimani, kwani hakuwa na mtu wa kumtumbukiza Kisimani, wakati maji yanaporibuliwa. Kwa maneno mengine, hakuwa na mtu wa kusikiliza shida na mahangaiko yake ya ndani.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Padre Luigi Maria Epicoco. Wakristo wajenge utamaduni wa kusikiliza na hatimaye, kutoa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watu: kiroho na kimwili. Kusikiliza ni kumthamini mtu katika utu na mahangiko yake ya ndani. Roho Mtakatifu ndio msingi wa uponyaji. Roho Mtakatifu ndiye anayetuongoza kuyafanya na kutekeleza mapenzi ya Mungu, kunakowaletea watu uponyaji wa Roho. Kumsikiliza Roho Mtakatifu ndio msingi wa kuyaelewa na kuyafanya mapenzi ya Mungu. Ni ukweli usiopingika kuwa, mtu asipopewa nafasi ya kusikilizwa basi hujihisi yuko peke yake, na hivyo basi kusikilizwa kunampa mtu tumaini la kuendelea kuishi. Tumaini la kuishi vizuri linatokana na kupewa nafasi ya kusikilizwa, hivyo basi waamini kama Mabalozi waaminifu wa Damu Azizi ya Yesu, wanapaswa kuwa mawakili wa upendo na ukumbozi wa watu uliopatikana kutokana na Damu ya Yesu. Mkristo ni Kanisa linalo sikiliza na mkristo ni Kanisa linalo tibu na kufariji, changamoto kubwa ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kujenga umoja na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ibada ya Damu Azizi
11 July 2022, 15:57