Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Askofu mstaafu Telesphore Richard Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, yatafikia kilele chake tarehe 21 Julai 2022. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Askofu mstaafu Telesphore Richard Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, yatafikia kilele chake tarehe 21 Julai 2022. 

Askofu Mstaafu Telesphore R. Mkude Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre!

Askofu Mstaafu Mkude: Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa zawadi na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre kwa muda wa miaka 50. Ni kipindi cha kuomba toba na msamaha wa dhambi na mapungufu ya kibinadamu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 ya Daraja Takatifu na Miaka 34 ya huduma ya Kiaskofu katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Wahenga wanasema "Ecce Sacerdos magnus, qui in diebus suis placuit Deo” yaani “Tazama kuhani mkuu, ambaye siku zake alimpendeza Mungu.” Anayezungumziwa hapa ni Askofu mstaafu Telesphore Richard Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania ambaye alizaliwa tarehe 30 Novemba 1945. Tarehe 16 Julai 1972 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 18 Januari 1988 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na kusimikwa na Kardinali Laurien Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam tarehe 26 Aprili 1988. Tarehe 5 Aprili 1993, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Tarehe 30 Desemba 2020 Baba Mtakatifu Francisko akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mstaafu Telesphore Richard Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, anabainisha kwa ufupi historia ya maisha na wito wake wa daraja Takatifu ya Upadre, inayopata utimilifu wake kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu. Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa zawadi na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre kwa muda wa miaka 50. Ni kipindi cha kuomba toba na msamaha wa dhambi na mapungufu yote ya kibinadamu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 ya Daraja Takatifu na Miaka 34 ya huduma ya Kiaskofu katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Mahojiano haya maalum yananogeshwa zaidi na Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., wa Jimbo Katoliki la Morogoro anayepembua kwa kina na mapana kuhusu zawadi na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Askofu mstaafu Telesphore Richard Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, yatafikia kilele chake tarehe 21 Julai 2022, kwa kutanguliwa na Masifu ya Jioni, tarehe 20 Julai 2022 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Patrisi, Jimbo Katoliki la Morogoro. Anakazia umuhimu wa: kuwatunza, kuwaenzi, kuwathamini na kuwashirikisha wazee katika maisha na utume wa Kanisa, miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre si haba kama kiatu cha raba! Ukichanganya na miaka 33 ya huduma ya Kiaskofu, watu wa Mungu nchini Tanzania wanayo haki ya kusema, “Mzee Mkude” umeupiga mwingi! Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., anamwombea mtangulizi wake, afya njema, ili aendelee kuchakarika kutoa huduma za kiroho kwa watu wa Mungu, huku wakiendelea kujenga na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa linalojibidiisha kujenga Kanisa la Kisinodi. Mwenyezi Mungu amkirimie neema na baraka za kuendelea kudumu katika maisha na wito wake. Na katika uzee uliotukuka, kwa hekima na busara zake aendelee kulijenga Kanisa na kuwafaidisha watu wa Mungu kwa njia ya huduma zake za maisha ya kiroho.

Askofu mstaafu Mkude: Miaka 50 ya Daraja na 33 ya Uaskofu
Askofu mstaafu Mkude: Miaka 50 ya Daraja na 33 ya Uaskofu

Kutoka Morogoro Frank Castory & Angela Kibwana wanaendelea kutujuza zaidi. Unapozungumzia Chimbuko la Ukristo Tanzania Bara bila shaka yoyote unalizungumzia Jimbo Katoliki Morogoro ambalo limekuwa na historia ndefu kuhusiana na namna ukristo ulivyoingia na namna ulivyosambaa katika maeneo mengi ya Tanzania ambayo awali ilifahamika kama Tanganyika kabla ya kupata Uhuru wake kunako tarehe 9 Desemba 1961. Jimbo katoliki Morogoro limepata neema ya kuupokea Ukristo mwaka 1864 kutoka kwa Wamisionari wa kwanza wa Shirika la Roho Mtakatifu kutoka Zanzibar ambapo waliingia Bagamoyo mwaka huo wa 1864 kwa ajili ya uinjilishaji na huo ndio ukawa mwanzo wa kuzaliwa Jimbo Katoliki Morogoro. Mji wa Bagamoyo ni alama ya ukinzani kwani ni kielelezo cha watu waliokata tamaa ya maisha, kiasi hata cha kubwaga moyo wao na hii ndiyo maana halisi ya jina “Bagamoyo, yaani Bwagamoyo.” Bagamoyo unabaki kuwa ni Mlango wa Imani kwa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki. Hapa ni mahali ambapo wamissionari wa kwanza walitua nanga ya: imani, matumaini na mapendo na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo Afrika Mashariki. Bagamoyo ni alama ya ukombozi, mahali ambapo mwanadamu amepata tena fursa ya kuinua moyo wake kwa imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Tangu kutangazwa rasmi kuwa Jimbo Katoliki Morogoro mnamo tarehe 25.03.1953 na askofu wake wa kwanza akiwa ni Bernardo Gerardo Hilhorst CSSp hadi sasa Jimbo la Morogoro limeongozwa na Maaskofu wafuatao baada ya Askofu Bernado Hilhorst kuongoza kuanzia (25.03.1953-11.08.1954), Askofu wa pili ni Mhashamu Herman Jan Van Elswijk CSSp (18.07.1954-15.12.1966), Askofu wa tatu ni Mhashamu Adrian Uliza Mkoba (02.07.1967-06.11.1992), Askofu wa nne ni Mhashamu Telesphor Richard Mkude (05.04.1993-30.11.2020) ambaye leo amekusudia kumzungumzia anaposherehekea miaka 50 ya Upadri wake, na Mhashamu Lazarus Vitalis Msimbe SDS ( Septemba 2021 hadi sasa) Akizungumza na wandishi wa makala hii kuhusiana na kuadhimisha miaka 50 tangu kupata Daraja Takatifu ya Upadre Askofu Mstaafu Telesphor Richard Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anaanza kwa kusema kuwa alizaliwa Novemba 30, 1945 katika kijiji cha Pinde Parokia ya Mgeta Jimboni Morogoro katika familia ya Baba Richard Fabian Kobelo na Mama Emilia Cassian Mlungwana. Askofu Mkude amesema kuwa amepata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi Pinde iliyopo huko Mgeta kuanzia Darasa la kwanza hadi la nne, na baadaye Darasa la tano hadi kumi katika Seminari ya Mtakatifu Petro Bagamoyo (kwa sasa Seminari ya Mtakatifu Petro Morogoro) baadaye alijiunga na Seminari ya Mtakatifu Charles (Itaga-Tabora), Seminari ya Kibosho, na Seminari kuu ya Kipalapala na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 16 Julai 1972.

Mashirika ya Kimisionari yamechangia sana katika uinjilishaji nchini Tanzania
Mashirika ya Kimisionari yamechangia sana katika uinjilishaji nchini Tanzania

Akizungumzia namna ambavyo wito wa Upadre ulivyochipua ndani yake Askofu Mstaafu Mkude amesema kuwa akiwa darasa la pili shule ya Msingi Pinde ndipo alipopata taarifa ya kuwepo shule ya Bagamoyo ambayo kwa kipindi hicho ndiyo ilikuwa inapokea wanafunzi wote waliokuwa wanahitaji kuwa mapadre katika Kanisa. “Niwashukuru wazazi kwa sababu walinilea kama familia ya kikristu na walinielekeza katika malezi ya Kikristo kama mtoto na hatimaye nilipata kusikia nikiwa darasa la pili, Mwalimu wangu Pius Makuwege mwenyeji wa Langali pale Mgeta Madukani, ambaye alikuwa anainisha pale darasani watu wanaweza kufanya kazi mbalimbali na akifundisha hayo kutuelekeza tupate hamu ya kuchagua kwenda Middle School gani baada ya kumaliza masomo yetu ya darasa la nne. Katika mafundisho yake alielekeza kwamba iko shule moja ya pekee sana na akaiandika ubaoni “Bagamoyo” naikumbuka picha hiyo  vizuri sana na akasema hii ni shule ya pekee kwa sababu ukitaka kujua mapadre wanapatikana wapi hapa  ndipo wanapoenda kujifunza katika shule hii, anayetaka kuwa Padre hapa ndiyo mahali pa kwenda kujifunza, kwa hiyo ikanivutia kwani niliona katika shule ambayo nilikuwa nimeanza pale hakuna waliowahi kwenda katika upande huo wa Bagamoyo na niliona kama ni vizuri niende huko na basi nilienda kule.”

Askofu Mstaafu Mkude ameongeza kuwa awali kabla ya kupata wazo hilo alifikiria kufanya kazi ya afya kama manesi au wahudumu wanaofunga vidonda na siyo daktari ambapo alisema kuwa hali hiyo ilichochewa na mmoja wa wazee wake aliyefahamika kwa jina la Mzee Thomas Msing’a aliyekuwa akitoa huduma eneo la Mgeta Madukani ambapo alikuwa akimpatia mavazi yake ya huduma ya afya pindi anapokuwa amepata vazi jipya. Amesema hali hiyo ya kupewa mavazi na mzee Msing’a ilimfanya avutiwe na kutamani kufanya kazi uuguzi hadi pale alipopata wazo jipya baada ya mwalimu Pius Makuwege kueleza kazi nyingine yaani Upadre ambayo alivutiwa nayo na hatimaye kujiunga na Seminari ya Bagamoyo. “Lakini niliposikia maelezo haya ya Mwalimu Pius Makuwege juu ya shule hii ya Bagamoyo inayofundisha mapadre hamu yangu ilibadilika kwenda kule, kwa hiyo tulifanya mitihani kama wanafunzi wanane kwenda Seminari ya Bagamoyo na kati yetu kutoka Pinde tulifanikiwa wawili na mwenzangu hakuendelea sana na hakujiunga hata na Seminari  na kutoka pale ndiyo nikajiunga na Seminari Bagamoyo na kisha kumaliza kidato cha pili tulipewa mitihani kutoka Itaga na baada ya kufaulu nikapelekwa Itaga nikasoma miaka mwili nilipomaliza ndipo nikaenda masomo ya Falsafa na kuendelea mbele zaidi na masomo ya Taalimungu.

Askofu Mstaafu Mkude amesema kuwa katika kufanikisha hamu yake ya kuwa Upadre, hawezi kuwasahau wazazi wake Mzee Richard Fabiani Kobelo na Mama Emilia Cassiani Mlungwana kwa kuwa alivyowashirikisha juu ya hamu yake ya kutaka kujiunga na Seminari ili awe Padre walimuunga mkono kwa asilimia zote na ndipo walipoanza kumuwezesha kumlipia ada ya masomo yake hadi alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 16 Julai 1972. Amesema kila mtu Mwenyezi Mungu anamwita kwa wito wake maalum hapa duniani hii inajidhihirisha kwake yeye binafsi pamoja na awali kutamani kuwa muhudumu wa afya lakini Mwenyezi Mungu alimwita kwenye wito wa Daraja Takatifu ya Upadre ambao ameutumikia hadi sasa anaposherehekea miaka 50 ya Upadre; wito muhimu katika kuongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu Akizungumzia juu ya kukua kwa miito mitakatifu ya Upadre na Utawa Jimboni Morogoro Askofu Mkude amesema pamoja na kuwa kwa sasa kuna mapadre wengi wazalendo ndani ya Jimbo lakini ni wazi kuna kila sababu ya kuwashukuru Wamisionari na Watawa ambao wamefanya kazi kubwa na wanaendelea kufanya kazi kubwa ndani ya Jimbo kwa kutambua kuwa Jimbo la Morogoro ni kubwa na limepata maendeleo makubwa na fungamani kwa uwepo na ushiriki wa Mashirika ya Kimisionari.

Ameeleza kuwa Wamisionari na Watawa wa Mashirika mbalimbali Jimboni wamefanya kazi kubwa katika sekta ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii hivyo kuna kila sababu ya kuwashukuru kwa utume wao ndani ya Jimbo huku akiwaomba waendelee kufanya utume ndani ya Jimbo “Kama tungekuwa hatuna Wamisionari hawa tungekuwa na upungufu mkubwa sana wa Mapadre, nataka kusema natoa shukrani kubwa kwa Wamisionari bado na siwaambii waondoke Mungu anataka wabaki waendelee kufanya kazi katika Jimbo, nishukuru lakini nikuombe mzazi kama mtoto anasema anataka kwenda Upadre  kwanza ungeshukuru ukijua kuwa wewe ni Mkristo hata kama siyo Mkristo utapata baraka nyingi sana, muda huu tunaona kwamba tunaongezeka tungeomba Mapadre waongezeke pasipo kujali Padre wa Jimbo au Shirika.” Pamoja na mambo mengi mazuri aliyofanya Askofu mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro ni pamoja na kuwaruhusu Mapadre wenzake kwenda kufanya utume katika Mabara mengine nje ya Afrika ikiwemo Australia. Akizungumza juu ya dhamiri iliyokuwa ikimsukuma kuwaruhusu Mapadre kwenda Mataifa mengine kuinjilisha anaeleza kuwa ni uhaba mkubwa wa mapadre katika mataifa hayo ambapo amesema kuwa amewahi kutembelea Australia na kutembea kwa zaidi ya masaa sita kwa gari kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kupata huduma ya padre jambo ambalo aliona kuna kila sababu ya kuwasaidia licha ya kwamba Jimboni kwake kulikuwa na uhitaji pia.

Papa Yohane Paulo II aliteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga 1988
Papa Yohane Paulo II aliteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga 1988

“Nimewahi kutembea mwendo wa masaa sita na gari kufika waamini wakokaa kwenye Parokia mojawapo, unafikiria katika Jimbo umbali wa kiasi hicho Padre atembee kwenda kuwahudumia waamini tutakuwa na wangapi ambao tunaweza kuwahudumia? kwahiyo walihitaji msaada mkubwa zaidi kuliko ya kwetu.” Amesema kuwa katika kipindi cha utume wake kama Askofu na mchungaji mkuu wa Jimbo la Morogoro alikuwa akitoa Mapadre wawili hadi wanne kwenda kufanya utume Austaralia ambapo wengine hadi sasa bado wanaendelea kutoa huduma hiyo ya kichungaji katika maeneo hayo huku wengine wakiwa tayari wamerejea Jimboni Morogoro. Miongoni mwa Mapadre aliyowahi kuwatuma Askofu Mkude kwenda kufanya utume katika mataifa mengine ni pamoja na Padre Anacklet Mloka, Padre Benjamini Mkuchu, Padre Medard Mikisi, Julius Chamlungu, Ephrem Dikwe, Agapito Mhando na Padre Chediel Mloka ambaye hadi sasa anaendeleza utume wake Australia.

Askofu Mstaafu Mkude aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 18 Januari 1988, kuwa askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na kuwekwa Wakfu tarehe 26 Aprili 1988 na hayati Kardinali Laurean Rugambwa. Akizungumzia namna alivyopokea uteuzi huo Askofu mstaafu Mkude ameeleza kuwa alipokea kwa mshtuko mkubwa na kuanza kujitafakari kama kweli ataweza kufanya kazi ya Uaskofu na kufikiria kukataa kwa vile huenda asifaulu katika nafasi hiyo lakini wazo liliomjia kuwa endapo kama angekataa angekuwa ameamua kwa utashi wake binafsi na siyo utashi wa Mungu ndipo aliamua kukubali na kujibu kuwa yupo tayari kutumika kama Askofu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Tanga. Amesema kuwa baada ya kuwekwa wakfu aliamua kufanya ziara za kushtukiza katika Parokia mbalimbali kila Dominika ili kujifunza kwa haraka mazingira ya Jimbo Katoliki la Tanga kwa vile alikuwa mgeni kabisa Jimboni humo hivyo ziara hizo zilimsaidia kuyafahamu mazingira ya Jimbo kwa urahisi zaidi. Hata hivyo Askofu Mkude amesema kuwa utendaji wake wa kazi Jimbo Katoliki la Tanga ulikwenda vizuri zaidi kutokana na ukweli kwamba alikuwa mgeni katika jimbo hivyo kila mmoja alifuata maelekezo yake kwa kushirikiana na Mapadre wa Jimbo hilo ambao walikuwa wakitenda kazi katika shamba la Bwana. Amesema kuwa tangu awali namna wanajimbo Katoliki la Tanga walivyompokea kwa shauku kubwa kuanzia mpakani mwa Jimbo Katoliki Morogoro na Tanga kulimpatia moyo zaidi wa kutenda kazi ya kuinjilisha kwa hali na moyo mkuu zaidi.

Miongoni mwa vyama vya kitume ambavyo aliviruhusu kuanzishwa katika Jimbo Katoliki la Tanga ni pamoja utume wa Mama wa Shauri Jema ambao uliwasaidia kukoleza utume kwa waamini walei katika Jimbo la Tanga. Baada ya Utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki laTanga kwa takribani miaka mitano hatimaye, tarehe 5 Aprili 1993 kwa mara nyingine tena Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua tena kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro, Jimbo lake ambalo amezaliwa ambapo amesema baada ya uteuzi huo aliona kama anapoteza kitu kwa sababu alishaanza namna yake ya kuendesha Jimbo la Tanga na walishazoeana na watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Tanga. Askofu Mstaafu Mkude ameongeza kuwa pili aliona kufanya utume Jimboni Tanga kulimrahisishia utendaji kazi kwa vile watu wote walikuwa wageni kwake lakini kurudishwa Jimboni Morogoro kulimfanya kukosa Uhuru kutokana na kusongwa na ndugu wengi jambo ambalo wakati mwingine walimfuata kutaka kazi au upendeleo wa namna yoyote ile ambapo ni kinyume na utaratibu wa Kanisa. Hata hivyo tarehe 5 Aprili 1993 Askofu Mstaafu Telesphor Mkude alianza utume wake rasmi Jimboni Morogoro kama Askofu wa nne wa Jimbo hilo hadi 30 Novemba 2020 Baba Mtakatifu Francisko aliporidhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani baada ya kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa. Miongoni mwa amana na utajiri mkubwa ambao Askofu Mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo la Morogoro ameliachia Kanisa la Afrika Mashariki na wote wanaozungumza Lugha ya Kiswahili ni tafsiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki kwa Lugha ya Kiswahili ambapo alitekeleza dhamana hiyo wakati akiwa Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC.

Jubilei 50 Morogoro

 

20 July 2022, 16:55