AMECEA:Maazimio makuu ya kutunza mazingira ni uwajibikaji!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) ulioanza tarehe 10 Julai na kunamalizika mjini Dares Salam Tanzania utarehe 17 Julai, 2022, Maaskofu wa eneo lote la AMECEA wanaamini kwamba kuna mgogoro wa kiikolojia ambao kwa kiasi fulani umesababishwa na mwanadamu katika eneo hilo. Wakati wa kusoma Risala katika Misa ya kufunga iliyofanyika katika Kituo cha Msimbazi, Jimbo Kuu la Dar es, Mwenyekiti wa AMECEA Askofu Charles Kasonde wa Jimbo la Zilowezi, nchini Zambia, alisema kwa kushikilia sana maliasili mara nyingi kumesababisha migogoro na vita, jambo ambalo linafanya kuwepo ‘kilio cha Mama Dunia na maskini kuongezeka zaidi.
Rais wa Amecea alisema katika ukanda wa Afrika Mashariki, msukosuko wa kiikolojia kwa sasa unathibitishwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi ambayo ni pamoja na ukame, mafuriko na vimbunga, pamoja na majanga mengine ambayo yanazidi kuwa tishio kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi na kwa maendeleo endelevu. mustakabali wa maisha ya watu. Maaskofu hao zaidi ya 100 pia wameeleza kusikitishwa na kasi ya misitu kuharibika haraka kutokana na matumizi ya kuni, uchomaji mkaa na shughuli za ujenzi wa miundombinu huku wananchi wakiwa hawafanyi jitihada za kutosha kupanda miti upya. Kwa niaba yao, Askofu Kasonde alisema walivyo na wasi wasi kuhusu uchimbaji madini na ukosefu wa mifumo madhubuti ya usimamizi wa taka. Wanafahamu kwamba kushughulikia masuala haya kunagusa haki ya kiuchumi na haki. Kwa maana hiyo haziwezi kushughulikiwa vya kutosha bila kuzingatia ipasavyo kutoa njia mbadala kama vile kukuza matumizi ya nishati ya jua na upepo na njia zingine za kujipatia riziki. Hata hivyo, haya yote yanachangia uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa mazingira katika eneo la AMECEA.
Maaskofu wa AMECEA walilipongeza zaidi Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), serikali, majimbo, Jumuiya za Kikatoliki, wanaume, wanawake na watu wote wenye mapenzi mema ambao wanachukua hatua za kulinda viumbe hai kama vile upandaji miti na kusafisha miji. Maaskofu pia wamesisitiza wito wa kampeni kali ya uhamasishaji wa mazingira katika ngazi ya msingi ya jamii ili kuongeza uelewa na kuboresha mawasiliano yao na watu kuhusu utunzaji wa mazingira katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na ngazi ya familia. Na kuhusu elimu, Maaskofu walikazia maana ya Mafundisho Jamii Katoliki kuhusu utunzaji bora wa mazingira na umuhimu wa kuunganisha shughuli za elimu ikolojia na ikolojia katika mtaala wa elimu kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watoto katika shule zote na nyumba za malezi hadi uhuhani na utawa na kwamba vijana lazima waelimishwe ili wawe mabalozi wa maadili mema ya ikolojia.
Uzinduzi wa Mwongozo
Maaskofu walisisitiza kuhusu haja ya Kanisa Katoliki katika ukanda wa AMECEA kushirikiana na serikali, madhehebu mengine na jumuiya za imani, familia, sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na mashirika ya maendeleo ya jamii na watu wote wenye mapenzi mema katika kuhamasisha juu ya huduma kwa mabadiliko ya kifikra na mazingira. Aidha wamesisitiza haja ya Mabaraza yote ya Maaskofu katoliki katika kanda ya AMECEA kuimarisha wajibu wao wa utetezi ili serikali ziweze kuibua sera na sheria za utunzaji wa mazingira zitakazozuia mila potofu za binadamu lakini kwa namna ambayo ni nyeti kwa ustawi wa watu wao. Na Maaskofu wameonesha mshikamano na jumuiya zote zilizokumbwa na mafuriko, ukame na vimbunga katika ukanda wa AMECEA; katika bara la Afrika na katika mabara mengine ulimwenguni. Hata hivyo, Maaskofu hao wameombea amani iendelee kuwepo katika nchi za Ethiopia, Eritrea, Sudan, Sudan Kusini, Kaskazini mwa Nigeria na Ukraine.
Hatimaye, Maaskofu wa AMECEA hawakusahau nchi ambayo inatarajia kufanya uchaguzi mwezi ujao nchin Kenya na hivyo waliwatakia uchaguzi uwe huru, wa haki, wa kuaminika na wa amani. Maaskofu wa Kanisa Katoliki wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki inajumuisha Kenya, Uganda, Malawi, Tanzania, Sudan Kusini, Sudan, Ethiopia, na Eritrea. Djibouti na Somalia ni wanachama washirika. Askofu Charles Kasonde hata hivyo amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa AMECEA, Padre Anthony Makunde kuwa Katibu Mkuu wa AMECEA kwa miaka minne ijayo. Askofu Kasonde alitangaza kwamba, Mkutano ujao wa 21 wa AMECEA utafanyika nchini Uganda mwaka 2026.