Tanzania,Mbeya:hacheni mahangaiko ya dunia,mlipakwa mafuta ya ubatizo
Na Thompson Mpanji na Sr. Martha Mwalugala; - Mbeya,Tanzania.
Mapadre zaidi ya 100 wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Tanzania, walishiriki katika hija iliyoanza tarehe 6-9 Juni 2022 katika Parokia ya Mtakatifu Boniface, Mkulwe ambalo ni kitovu cha imani jimboni humo, tangu kuingia Wamisionari wa Afrika mnamo mwaka 1898 jimboni Mbeya na kujenga Kanisa mnamo mwaka 1974. Katika tukio hilo, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Katoliki la Mbeya, na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ndiye aliongoza adhimisho Misa Takatifu. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Nyaisonga aliwaalika familia ya Mungu kutafakari kuhusu miito mbalimbali ikiwemo ya mapadre, Watawa, Walei hata kwa wasiobatizwa kwa sababu nao wanaitika kwa namna mbalimbali kwani roho wa Mungu anafanyakazi mahali popote.
Askofu Mkuu akiendelea na mahubiri yake aliweza kutaja na kufafanua baadhi ya vipengere kadhaa ambavyo, awali ya yote kuhusu kuitwa, kutumwa kutekeleza, kujikita katika huduma ama shughuli yoyote ambayo mtu anaitwa na kukabiliana na changamoto inayotokana na kazi ya utume. Hatimaye alielezea juu ya kukamilisha kazi na kupata thawabu. Askofu Mkuu Nyaisonga aliwakumbusha na kuwaalika mapadre kwamba hija ni safari ya kiroho katika kujitathmini, kujisahihisha na kujitakatifuza huku akiwasihi wakristo wote kuendelea kuwaombea mapadre katika safari ya Utume wao.
Siku ya pili Mahujaji wakiongozwa na Askofu Mkuu Nyaisonga waliweza kushiriki Njia ya Msalaba kwa umbali wa Kilomita 19 kwenda kupanda hadi kituo cha mwisho cha njia ya Msalaba katika kilele cha Mlima uitwao ‘Tukamlozye’ na kurudi Parokiani ambako ilifuatia Ibada ya Mwanga. Akiwa katika kilele cha Mlima, ‘Tukamlozye’, Askofu Mkuu Nyaisonga, wakati wa tafakari yake ilikuwa ni kuwakumbusha waamini, kuacha mahangaiko ya dunia kwa kukimbilia sauti zisizoeleweka na kukanyaga mafuta ambayo wao walipakwa tangu kubatizwa kwao.
Upotofu huu ni kutokana siku hizi kuibuka dini mbali mbali ambazo wakristo kutokana na kuwa na imani haba, wanaopeperushwa na upepo huo kama bendera ifuatayo upepo katika mahangaiko ya kutafuta uponyaji. Kwa kusahau kabisa neema waliopokea awali kwa kuzaliwa upya katika maji na roho Mtakatifu tangu kubatizwa. Askofu Mkuu Nyaisonga, kwa njia hiyo, alisema: “Msihangaike na sauti ama maneno yanayosikika yasiyoeleweka…ninyi muwe kama Eliya muombe na kusali kwa mwenyezi Mungu kwa sauti ya upole na unyenyekevu na ikiwezekana mkiwa chumbani wala watu wengine wasisikie sauti zenu, msikimbilie mnakoambiwa maji mliyobatizwa ni machache ama mafuta mliyopakwa ni kidogo, ninyi ndiyo, mliyoanza sasa iweje muanze kudanganyika?
Akiendelea na tafakari hiyo, Askofu Mkuu alizungumzia namna ambavyo Nabii Eliya alivyotoa “ushuhuda wa Nguvu ya Mungu kushinda mambo ya kibahari na mahangaiko” ambayo Binadamu wanakumbana nayo “kwa sasa hata kufikia kumsahau Mungu huku akiwaalika kuendelea kusadiki Kanisa moja Takatifu Katoliki la Mitume”. Katika hija hiyo mahujaji Mapadre hao walipata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali katika Semina, kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja ikiwa na kushiriki njia ya msalaba kupanda Mlima ‘Tukamlozye’ uliopo katika safu ya Milima ya ‘Kalambanzite’.