Sherehe za Ekaristi Takatifu:Neno Ekaristi ni kushukuru!
Padre.Efrem Msigala, OSA, Shirika la Mt. Augustino Roma.
Kwa mara nyingine mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican news nakukaribisha katika Tafakari ya Liturjia ya Neno la Mungu Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo. Ni sherehe inayoadhimishwa baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Lakini pia ni sherehe ambayo inaadhimishwa siku ya Alhamisi Kuu ndani ya siku tatu kuu za Pasaka. Siku hiyo hatuadhimishi kwa shangwe sababu tunaanza kutafakari mateso na kifo cha Kristo. Hivyo Kanisa likaweka nafasi nyingine ili kuadhimisha kwa shangwe zaidi. Ndiyo alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu au Jumapili inayofuata kuwezesha ushiriki wa waamini. Ni sherehe ambayo tunaandamana na Yesu katika mitaa mbalimbali. Sherehe ya Ekaristi. Kwa hiyo tunatafakari Ekaristi ni nini? "Ekaristi" ni neno la Kiyunani, ambalo linamaanisha, "kushukuru". Katika desturi ya Kiyahudi, kila mlo ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa mambo yake mema. Katika kila Misa, tunatenda kama makuhani wa uumbaji, tukitoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya uhai, na kwa ajili ya mambo mengi anayotujalia. Hata hivyo maneno yaliyotumika na Wakristo wa kwanza katika Matendo ya Mitume kuhusu Ekaristi ni "kuumega mkate", Karamu ya Bwana, na Mkutano wa Ekaristi.
Halafu Neno “Mwili wa Kristo” linaweza kumaanisha mambo matatu: mwili wa kimwili , mwili wa fumbo, na mwili wa sakramenti. Kwa maana zifuatazo: Mwili wa kimwili wa Yesu tayari umetukuzwa na umeketi mkono wa kuume wa Baba. Lakini anaweza kuwepo kimwili popote na popote anapotaka kwa sababu tayari ni mwili uliotukuka. Hakuna lisilowezekana kwa Yesu. Mwili wa fumbo wa Yesu ni Kanisa, jumuiya ya waamini. Yeye ndiye kichwa cha Mwili huu. Yupo pamoja nasi katika Kanisa: ndiyo maana alisema “Walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo katikati yao.” Mwili wa Sakramenti ya Yesu ni Ekaristi, sakramenti ya Mwili na Damu yake. Ekaristi ni uwepo halisi wa Yesu katika maumbo ya Mkate na divai.
Somo la kwanza Mwa 22:1-18 linatuambia kwa ufupi kwamba: “Abramu akamtolea Melkizedeki sehemu ya kumi ya vitu vyote.” Hakuitoa kwa nia ya kupokea kitu kama malipo. Badala yake, alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe., Melkizedeki alimbariki, na kutoa shukrani kwa Mungu kwa niaba yake kwa mkate na divai. Haya yalikuwa matoleo ya mtu binafsi kwa namna ya vitu vya kimwili. Kwa hakika, Abramu ni mtaalamu wa kujitolea. Somo la pili Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26). Ni maelezo ya Paulo kuhusu tukio la Karamu ya Mwisho ya Yesu na wanafunzi wake. Lakini pia umuhimu wa Ekaristi kama ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo unaletwa tena nyumbani kwa Wakorintho. Injili inahusu muujiza wa kuzidisha mikate Lk.9:11-17. Yesu aliwalisha wanaume zaidi ya 5000 bila kuhesabu wanawake na watoto kwa mikate mitano na samaki wawili. Wakala na kushiba. Muujiza huu, hasa katika Injili ya Yohana sura ya 6 ulitumika kama utangulizi wa Hotuba ndefu ya Yesu juu ya Ekaristi. Katika Injili ya Luka na Injili nyingine pacha, kipindi hiki kilisimuliwa katika muktadha wa mafunzo ya wanafunzi. Hata hivyo, kuna dokezo la Ekaristi.
Katekismu ya Kanisa Katoliki inaeleza kwa upana juu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hapa ni baadhi ya nukuu zinataja kuwa: hapo awali, Kristo alijitoa kisakramenti kwetu. Hii ni njia rahisi ya kuonyesha upendo wake usio na masharti kwetu. Anatuamuru hivi: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu!” Kwa hiyo kanisa linatufundisha: “Amri ya Yesu ya kurudia matendo na maneno yake hadi atakapokuja (CCC 1341), halafu pia inasema "Ekaristi ni 'chanzo na kilele cha maisha ya Kikristo.' CCC.1106. Pia CCC 1378. Inataja kuwa "Ibada ya Ekaristi. Katika liturujia ya Misa tunadhihirisha imani yetu katika uwepo halisi wa Kristo chini ya maumbo ya mkate na divai tukisujudi kwa kina kama ishara ya kumwabudu Bwana. Hata hivyo "Kanisa Katoliki daima limetoa na bado linatoa nafasi ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, sio tu wakati wa Misa, hata nje ya Misa ndiyo maana sehemu nyingi kila alhamisi au jumapili kuna kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Misa na kuna maabudu ya daima. Pia sherehe hii kuna kufanya maandamano na Ekaristi kwa heshima na ibada katika maeneo mbalimbali.
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili Papa alitukumbusha kwamba katika kuadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Kristo, Kanisa “haliadhimishi Ekaristi pekee, bali huibeba kwa taadhima, likitangaza hadharani kwamba dhabihu ya Kristo ni kwa wokovu wa ulimwengu wote.” Hivyo ni sahihi kuandamana na Yesu katika Ekaristi Takatifu. Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo (Corpus Christi), ambayo Kanisa linaadhimisha leo inatukumbusha sote zawadi ya ajabu ya Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo katika Sakramenti Takatifu. Ingawa lengo kuu la sherehe hii ni juu ya lishe ya kiroho ambayo Kristo anatupa, lengo lake la pili ni kwa Mwili wa Kristo ambao ni Kanisa. Mwili na Damu ya Kristo (Ekaristi), ni zawadi bora sana ambayo tumepewa na Kristo.
Sherehe ya Ekaristi iliigwa baada ya Mlo wa Pasaka ya Wayahudi. Tunakumbuka kwamba Yesu alikuwa Myahudi na alifanya karamu ya mwisho katika pasaka ya wayahudi. Karamu ya Mwisho iliyofanywa na mitume wake ambapo alianzisha Sakramenti ya Ekaristi ilikuwa Mlo wa Pasaka. Hii ndiyo sababu tarehe ya kusherehekea Wiki Takatifu inatofautiana kila mwaka kwani inabidi ifanane na sherehe ya Kiyahudi ya Pasaka wakati Yesu alipoadhimisha Karamu ya Mwisho. Sherehe ya Pasaka ya Kiyahudi imepangwa kwa mwezi kamili (Nisan). Kwa maneno mengine sherehe ya Pasaka kila mwaka inategemea Alhamis Kuu inaangukia lini kadri ya kalenda ya wayahudi. Mambo husika katika Mlo wa Pasaka ya wayahudi: ni mwana-kondoo, mkate usiotiwa chachu, divai kutoka mzabibu na mboga chungu. Mwana-kondoo ndiye mnyama wa dhabihu kama inavyoonyeshwa katika Sheria ya Musa. Mkate usiotiwa chachu ni ukumbusho wa kukimbia kwa Watu Waliochaguliwa kutoka Misri. Mkate hauna chachu kwa sababu walipaswa kufanya haraka na hakuna wakati tena wa kufanya unga uumuke. Mvinyo ilikuwa ni jadi, ishara ya furaha na sherehe. Mimea ya uchungu inawakumbusha watu juu ya mateso na mapambano yao wakati wa utumwa wao huko Misri.
Katika Karamu ya Mwisho, Yesu na mitume walikuwa na mkate usiotiwa chachu na divai ya zabibu tu. Hakuna haja tena ya mwana-kondoo wa dhabihu, kwa kuwa Yesu mwenyewe ni Mwana-Kondoo wa Mungu: Yeye ndiye mhusika anayetolewa kama dhabihu, na wakati huo huo, Kuhani Mkuu akitoa dhabihu. Ndiyo maana Mt. Augustino anasema: “Kristo alikuwa amebebwa kwa mikono yake mwenyewe alipoutoa mwili wake, akisema, ‘Huu ni mwili wangu’; maana alikuwa ameushika mwili huo mikononi mwake alipokuwa akisema maneno hayo. Kwa hiyo basi, Mtakatifu Augustino anasisitiza faida sahihi ya Ekaristi, ambayo ni umoja wa Mwili wa Fumbo. Upendo unaoliunganisha Kanisa ni matokeo sahihi ya kupokea Mwili na Damu ya Kristo. Ekaristi inaweza kujenga Mwili wa Kristo katika mapendo (baadaye itaitwa res tantum) kwa sababu yenyewe ndiyo Mwili wa Kristo uliopo kisakramenti (res et sacramentum).
Pia Augustino anasema mkate na divai inayoonekana kwenye madhabahu, "iliyogeuzwa kwa neno la Mungu," ni Mwili na Damu yake. Kwa kuupokea kwa uchaji Mwili huo na Damu ile iliyomwagika kwa ajili yetu, tunakuwa Mwili huo, ambao ina maana kwamba tunaunganishwa katika muungano wa karibu wa Mwili wa Fumbo. Msisitizo mwingine wa Mtakatifu Agustino ni kuabudu Ekaristi kabla ya kupokea Komunyo Takatifu ni kukiri wazi uwepo wa kutosha wa Mwili na Damu ya Kristo katika Ekaristi. Hivyo Augustino anasema wakati ule wa Mageuzo ni wakati unaostahili kumwabudu Kristo kimya kimya. Ekaristi inastahili kuabudiwa tu kwa sababu ina uwepo mkubwa wa ubinadamu wa Neno, yaani Kristo, Umwilisho. Pia anasistiza kumpokea Yesu kwa ibada na heshima.
Pamoja na hayo wakati wa Karamu ya Mwisho, Yesu pia aliweka Sakramenti ya Ukuhani wa Kihuduma yaani daraja takatifu. Daraja lenye ngazi tatu ambazo ni Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Hawa huwekwa wakfu kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu ambao wana Ukuhani wa Pamoja wanaopokea katika Ubatizo. Hili linadhihirika sana katika maadhimisho ya Ekaristi. Sababu ya Yesu kuanzisha Sakramenti ya Daraja Takatifu wakati wa Karamu ya Mwisho ambapo Sakramenti ya Ekaristi ilianzishwa ilikuwa ni kuhakikisha kuna wahudumu ambao wataendelea kuadhimisha Ekaristi baada ya yeye kuondoka: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Hivyo Daraja Takatifu linamuunganiko muhimu sana na Sakramentii ya Ekaristi Takatifu. Hivyo basi tuwaombee makasisi wetu ili waweze kuadhimisha maadhimisho kwa heshima na ibada. Pia waepushwe na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kipindii hiki. Mama kanisa anatuhimiza tuwasaidie na kuwaombea mashemasi, mapadre na maaskofu wetu. Ni walengwa wa adui na wengi wao huanguka katika mtego wa shetani wa kiburi, uchu wa mali, starehe, tamaa na mambo mengine. Wanahitaji maombi yetu, usaidizi, kuwategemeza au kuwawezesha lakini marekebisho ya kindugu pale tunapoona hawaendi vizuri.