Sherehe ya Pentekoste:Roho Mtakatifu anajionesha kwa njia mbalimbali
Na Padre Efrem Msigala, OSA, Shirika la Mt. Augustino,Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Redio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturjia ya Neno la Mungu sherehe ya Pentekoste. Siku ya hamsini baada ya Pasaka Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume. Ni siku ambayo Kanisa lilizaliwa rasmi na kuanza utume wake. Ni siku tunapohitimisha kipindi cha Pasaka na kuanza kipindi cha kawaida cha liturjia ya mwaka wa kanisa. Tunasherehe Pentekoste ambayo ni utimilifu wa ahadi ya Kristo kuwatumia Roho Mtakatifu mitume wake, ambayo ilitokea siku ya 50 baada ya ufufuko wake. Roho Mtakatifu alipowashukia mitume, ilikuwa ni siku ya sherehe ya mavuno ya wayahudi. Lilikuwa ni tukio la kila mwaka, tukio lenye mkusanyiko wa watu wengi, kutoka sehemu mbalimbali. (Kutoka 23:16: “Nawe utaiadhimisha sikukuu ya mavuno ya nafaka pamoja na mazao ya kwanza uliyopanda shambani, na hatimaye sikukuu ya mavuno ya mazao mwishoni mwa mwaka unapokusanya mazao ya mashambani”. Kwa hiyo kitabu cha kutoka sura 23:16 kinaamuru waisraeli waiadhimishe sikukuu ya mavuno. Halafu kitabu cha Walawi 23:15-22 pamoja na Kumbukumbu la Torati 16:9-12 vinaeleza jinsi ya kufanya maadhimisho hayo. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku baada ya sabato.
Mtahesabu siku hamsini hadi siku baada ya sabato ya saba (…) Mtaleta kutoka katika makao yenu mikate miwili (...). Pia beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka mmoja, kuwa dhabihu ya sadaka. Naye kuhani atavitakasa pamoja na mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kuteketeswa mbele za Bwana, pamoja na wale wana-kondoo wawili.” Kwa hiyo siku ya Pentekoste ya ujio wa Roho Mtakatifu kwa mitume ilikuwa ni rahisi kuwa na umati wa watu wengi na kushuhudia mitume wakiongea kwa lugha zao na kuelewana kwa sababu watu walikusanyika kwa sherehe ya mavuno wakitoka sehemu mbalimbali. Lakini kuanzia siku hiyo ikachukua sura nyingine siyo mavuno tena bali ujio wa Roho Mtakatifu siku ya 50 baada ya pasaka.
Somo la Kwanza Matendo ya Mitume 2:1-11 linahusiana na matukio ya kuja kwa Roho Mtakatifu kama dhihirisho kuu la nguvu za
Mungu. Kunena kwa lugha mbalimbali kulikoeleweka kwa Wayahudi wote waliokuja Yerusalemu kwa ajili ya kuadhimisha sikukuu ya Pentekoste kwa lengo la shukrani ya mavuno. Ilikuwa ni uthitisho wazi wa utume wa kanisa kwa ulimwengu wote. Ni wito kwa kanisa kuwa ishara ya umoja wa wanadamu. Hii ni bila kujali rangi, au lugha.
Katika somo la pili, barua yake Paulo kwa Wagalatia 5:16-25 anatukumbusha kwamba kwa sakramenti ya ubatizo na kipaimara tumetiwa alama isiyofutika juu yetu. Kwa hiyo, tumeundwa mahsusi kwa Utume wa Mungu. Hii ina maana kwamba ni Roho Mtakatifu ambaye hutoa uzima na kuongoza utume wetu. Kwa hiyo, kwa kumiminiwa kwa Roho Mtakatifu, tunatiwa alama kamili kama watoto wa Mungu wakati wa ubatizo na kipaimara. Pamoja na hayo tunakumbushwa juu ya majukumu makuu ya Roho Mtakatifu kama: kutetea, kufundisha, na kutukumbusha mambo ambayo tunapaswa kujua. Hata hivyo, ili jambo hilo liwezekane, ni lazima tuwe tayari kushirikiana naye. Anaweza kutufundisha tu ikiwa tunazingatia mashauri yake. Anaweza tu kutukumbusha mambo tunayopaswa kujua, ikiwa tutamwambia na kumwomba kwa unyenyekevu, na kwa hiari kila wakati. Roho Mtakatifu ndiye anayetutia nguvu na kutufanya kuwa watoto wa Mungu. Hii ina maana kwamba tuna ujasiri wa kumwita Mungu Abba Baba. Roho Mtakatifu ametolewa kwetu ili tuweze kuzaa matunda mema yatakayodumu (Gal 5, 22).
Katika injili ya Yohane 20:19-23 Yesu aliwatia moyo wanafunzi na kuwapa utume wa kuondoa dhambi. akisema: "Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi. Akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, "mpokeeni Roho Mtakatifu, wo wote mtakaowaondolea dhambi zao, wameondolewa. Na wo wote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa”. Sisi ni viumbe vya Mungu, Sisi ndio wafaidika wakuu wa ujio wa Roho wa Mungu ulimwenguni kwa sakramenti ya kitubio: Mitume na waandamizi wao ndio waliopewa thamani hiyo na uwezo wa kuondolea dhambi, kwa kipawa cha Roho Mtakatifu, ni uwezo ambao Yesu hakutoa kwa kila mtu bali kwa Mitume wake na waandamizi wao, ambao sasa ni maaskofu na mapadre. Hawa ndiyo waliopewa uwezo huo ambao pia wanafanya utume huo kwa jina la kanisa na ndani ya kanisa.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News, hapa ni baadhi ya sifa za Roho Mtakatifu: ni Roho wa ukweli, mfariji, mshauri, wakili, mwenye kukumbusha yote, mponyaji, mpaji wa upendo na mtoaji wa vipaji saba. Pia mjaza ujasiri, aliwafanya mitume wawe na ujasiri wa kuongea bila woga ingawa kabla yake walijifungia kwa hofu. Pia Roho Mtakatifu anajionesha kwa njia mbalimbali: kwa lugha za ndimi za moto, kama njiwa, upepo, katika rangi nyekundu na pia kwa lugha tofauti lakini walielewana, tofauti na wale wa mnara wa babeli ambao lugha ilitumika kuwafarakanisha. Roho Mtakatifu alitumia lugha tofauti kuwa unganisha.
Roho Mtakatifu anafanya upya watu wa kale. Kwa kuwa Roho Mtakatifu ni Roho wa hekima na ufahamu, Roho wa shauri na uweza, Roho wa maarifa na utauwa, Roho ambaye anapelekea kuzaa matunda mema kama upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhila , uaminifu, unyenyekevu na kujitawala. Mpendwa katika Kristo, na kama Roho wa Mungu hana nafasi kwetu matunda yake ni chuki, kukosekana upendo, dharau, mauaji, masengenyo, migawanyiko, mafarakano pia machafuko na mengine.
Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii tutambue kuwa ni wakati wakujitambua sisi ni nani nathamani tuliyonayo kama wanakanisa katoliki ambalo ndiyo Kanisa lililoanza rasmi siku ya Pentekoste. Hivyo tutambue kuwa kanisa hili linasifa au alama nne tofauti na makanisa mengine kama tunavyokiri kwenye Kanuni ya Imani ya Nicea. Ni kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Tumwombe Roho Mtakatifu atuimarishe ili tusimame imara na tusipeperushwe na kusahau misingi ya imani yetu. Kwa ubatizo tumefanywa kuwa wanakanisa. Hakuna sababu ya kuhangaika mara leo huku kesho kule. Kanisa Katoliki ndiyo mama.