Tafuta

Prof. Jerry Pillay, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC aliyechaguliwa tarehe 17 Juni 2022. Prof. Jerry Pillay, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC aliyechaguliwa tarehe 17 Juni 2022. 

Prof. Jerry Pillay Katibu Mkuu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limemchagua Mchungaji Prof. Jerry Pillay kutoka Afrika ya Kusini, kuwa Katibu mkuu mpya wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Mchungaji Prof. Jerry Pillay alizaliwa kunako mwaka 1965 huko Afrika ya Kusini. Kabla ya kuchaguliwa kwake, alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Taalimungu na Dini, Chuo Kikuu cha Pretorio, Afrika ya Kusini. Changamoto zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia! Hizi ni juhudi zinazolenga kutoa ushuhuda wa Makanisa katika kusimamia: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kujikita katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, lilianzishwa kunako mwaka 1948 likiwa na Makanisa wanachama 147 na tangu wakati huo, zaidi ya Makanisa na Madhehebu ya Kikristo yapatayo 200 yamejiunga na kuwa ni sehemu ya Baraza hili yakiwa na waamini zaidi ya milioni 560. Umoja wa Wakristo duniani, kinapaswa kuwa ni chombo makini cha kujibu changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwaliko wa kujibu kilio cha watu wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia kutokana na: vita, njaa, umaskini na maradhi, maadui wakubwa wanaonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani katika matendo kama ilivyokuwa wakati wa Mwaka 1920. Hii ni fursa kwa Wakristo kujikita katika mchakato wa haki, amani, upatanisho na mshikamano; mambo makuu yanayofumbatwa katika Habari Njema ya Wokovu.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vipaumbele vya Makanisa Ulimwenguni
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vipaumbele vya Makanisa Ulimwenguni

Ni katika muktadha huu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, tarehe 17 Juni 2022 limemchagua Mchungaji Prof. Jerry Pillay kutoka Afrika ya Kusini, kuwa Katibu mkuu mpya wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na anatarajiwa kuanza utume huu, Januari 2023. Mchungaji Prof. Jerry Pillay alizaliwa kunako mwaka 1965 huko Afrika ya Kusini. Kabla ya kuchaguliwa kwake, alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Taalimungu na Dini, Chuo Kikuu cha Pretorio, Afrika ya Kusini. Ni Mchungaji wa Kanisa la “Uniting Presiberian Church”. Kati ya vipaumbele vyake kwa sasa ni kujenga na kudumisha haki na umoja unaoonkena, ili kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwani Kanisa lililogawanyika linatoa ushuhuda dhaifu na dhaifu zaidi katika ulimwengu uliosambaratika na kusingana hata katika mambo msingi. Umoja na Haki ni chanda na pete kwani ni tunu zinazotegemeana na kukamilishana. Hii ni pamoja na haki ya kuwajali na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Changomoto nyingine ni kung’oa ubaguzi ndani ya Kanisa, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini wote.  Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kumbe uwepo wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kipindi chote hiki ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya Makanisa duniani.

Lengo ni kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano kati ya Makanisa katika ngazi mbalimbali, ili siku moja, Wakristo wote waweze kuwa chini ya Mchungaji mmoja, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.  Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. limekuwa ni jukwaa la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Wakristo wanaalikwa kuzingatia kanuni zifuatazo kila wanapotafuta kutimiza utume wao wa Kikristo kwa namna inayofaa, hususani katika muktadha wa mahusiano ya majadiliano ya kidini. Kwa kutenda katika upendo wa Mungu. Wakristo wanaamini kuwa Mungu ni asili ya upendo wote na, kwa hiyo, katika ushuhuda wao wanaalikwa kuishi maisha ya upendo na kuwapenda jirani zao kama wanavyojipenda wenyewe (Rej. Mathayo 22:34-40; Yohane 14:15). Kumfuasa Kristo. Katika nyanja zote za maisha, na zaidi sana katika ushuhuda wao, wakristo wanaalikwa kufuata mfano wa mafundisho ya Yesu Kristo, wakishiriki upendo wake, wakimtukuza na kumheshimu Mungu Baba katika nguvu ya Roho Mtakatifu (Yohane 20:21-23). Wakuze na kudumisha Fadhila za kikristo. Wakristo wanaitwa kuishi kiadilifu, kwa upendo, huruma, unyenyekevu na kushinda kiburi, kujishusha na kuwa na kiasi (Rej. Wagalatia 5:22). Wazingatie matendo ya utumishi na haki. Wakristo wanaalikwa kutenda kwa haki na kupenda kwa wema (Rej. Mika 6:8). Wakristo wanaalikwa zaidi kuwahudumia wengine na kwa kufanya hivyo kumtambua Kristo katika kaka na dada walio wadogo (Rej. Mathayo 25:45). Matendo ya utumishi, kama vile kutoa elimu, huduma ya afya, misaada na matendo ya haki na utetezi ni sehemu ya msingi katika kuishuhudia Injili. Kujinufaisha kupitia hali za umaskini na uhitaji wa wengine hakuna nafasi katika utume wa kikristo. Wakristo wanapaswa kupinga na kujizuia na namna zote za kushawishi, iwe ni kushawishi kwa fedha au zawadi, wanapofanya matendo ya utumishi.

WCC: Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni muhimu katika kukuza amani duniani
WCC: Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni muhimu katika kukuza amani duniani

Utambuzi katika utume wa uponyaji. Kama sehemu ya msingi ya ushuhuda wa Injili, wakristo wanatoa huduma ya uponyaji. Wakristo wanaalikwa kutambua kwamba wanapotoa huduma hizi wanapaswa kuheshimu kikamilifu hadhi ya mwanadamu na kuhakikisha kuwa udhaifu wa watu na uhitaji wao wa kuponywa havitumiwi. Kupinga vurugu. Wakristo wanaalikwa kupinga aina zote za vurugu katika ushuhuda wao, iwe ni za kisaikolojia au za kijamii, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka. Wakristo wanapinga vurugu, ubaguzi na ukandamizaji unaofanywa na dini yoyote au mamlaka ya kisekulari, ikiwa ni pamoja na kunajisiwa au kuharibiwa maeneo ya ibada, sanamu na vitabu vitakatifu. Uhuru wa dini na kuabudu. Uhuru wa kuabudu, ikiwa ni pamoja na haki ya kukiri imani na kuiishi wazi wazi, kuisambaza au kubadili dini, ni matokeo ya hadhi hasa ya mwanadamu ambayo ina msingi wake katika mwanadamu kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Rej. Mwanzo 1:26). Kwa hiyo, wanadamu wote wana haki na wajibu sawa. Pale dini yoyote inapotumika kwa minajili ya siasa au pale madhulumu ya kidini yanapotokea, wakristo wanaalikwa kutoa ushuhuda wa kinabii kwa kupinga matendo kama hayo. Kuheshimiana, kujenga na kudumisha mshikamano. Wakristo wanaitwa kujitoa kikamilifu ili kushirikiana na watu wote kwa kuheshimiana, kukuza kwa pamoja haki, amani na mafao ya wengi. Ushirikiano baina ya dini mbalimbali ni jambo la muhimu katika wajibu huu.

Heshima kwa watu wote. Wakristo wanapaswa kutambua kwamba Injili inatoa changamoto inayotajirisha tamaduni. Hata pale Injili inapotoa changamoto kwa baadhi ya nyanja za tamaduni, wakristo wanaalikwa kuwaheshimu watu wote. Wakristo wanaalikwa pia kutambua mambo ambayo kwayo injili inayapa changamoto. Wakristo wanahamasishwa kusimama kidete kupinga ushuhuda wa uongo. Wakristo wanapaswa kuongea kwa heshima na unyofu; wanapaswa kusikiliza ili kujifunza na kuelewa imani na namna za imani za watu wengine, na wanahimizwa kutambua na kuenzi kile kilicho cha kweli na kizuri katika imani hizo. Wajibu wowote au ukosoaji unapaswa kufanywa katika hali ya heshima, na kuhakikisha hawashuhudii uongo juu ya dini nyingine. Kusaidia mang’amuzi binafsi. Wakristo wanapaswa kutambua kwamba mtu kubadili dini yake ni hatua ya uamuzi ambayo inapaswa kusindikizwa na muda wa kutosha wa tafakari na maandalizi, kupitia hatua inayohakikisha uhuru binafsi. Kujenga mahusiano ya dini mbalimbali. Wakristo wanapaswa kuendelea kujenga mahusiano ya heshima na ya kuaminiana na watu wa dini mbalimbali, ili kuwezesha kufahamiana kwa kina, kuridhiana na kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni
22 June 2022, 14:10