Mashahidi wa Uganda:ushuhuda wa damu ya kiekumene!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Leo ni siku kuu kubwa ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake! Siku hii inaongozwa na kauli mbiu iliyochaguliwa mwaka huu 2022: "Kubatizwa na kutumwa kumshuhudia Kristo kwa matumaini”. Wafiadini wa Afrika, waliouawa nchini Uganda kati ya Mei 1886 na Januari 1887, wanakumbukwa tarehe hii kwa sababu mnamo tarehe 3 Juni 1886, Karoli Lwanga alichomwa moto hadi kufa huko Rubaga. Wafiadini hawa ni matunda ya kwanza ya Wakristo, mia moja Wakatoliki na Waanglikani, wahanga wa mateso ya Mfalme Mwanga mbaya, katika eneo la Maziwa Makuu na kwa maana hiyo tunaweza kusema ni damu ya kiekumene kwa sababu Makanisa yote yamebahatika kuwa na mashuhuda wa imani watu ambao walijitoa maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Uekumene wa damu ni ushuhuda wa nguvu kwa ajili ya Makanisa yote ya kikristo kama ilivyo kwa Nchi ya Uganda na kwingineko mahali ambapo wamekufa, waanglikani, na madhehebu mengine ya kikristo kwa ushuhuda wa imani katika Kristo.
Karoli Lwanga, alikuwa mstari wa mbele wa mahakama, alilazimika kutetea usafi wa wengine wenzake, dhidi ya mfalme, na baada ya hukumu hiyo aliwatayarisha wafuasi wake waaminifu kwa ajili ya kifo cha kishahidi. Kufuatia hukumu hiyo ya kifo, vijana hao wenye umri wa chini ya miaka ishirini, wana wa watu mashuhuri, walipanda kilima cha Namugongo kila mmoja akiwa amebeba mzigo wa kuni mabegani, ambao ulitumika kwa nguzo iliyowachoma wakiwa hai. Kulingana na mila ya zamani, wakati wa mwisho, watatu kati yao, kwa kura, walisamehewa. Ushuhuda wa wale watatu walionusurika uliweza kutoa historia ya kifo chao cha kishahidi. Mauaji haya yalikuwa ni kielelezo cha historia tukufu na chungu kwa wakati mmoja, ambapo uinjilishaji na ukoloni ulifungamana na matukio ya ufalme wa Buganda, eneo ambalo sasa ni sehemu ya Uganda. Kuchanua kwa Kanisa nchini Uganda ni tunda la damu ya mashahidi wake. Karoli Lwanga alitangazwa kuwa Msimamizi wa Chama Katoliki cha Vijana wa Afrika mnamo mwaka 1934.
Hata hivyo takwimu rasmi zinaonesha kwamba, Mashahidi wa Uganda waliouwawa kwa amri ya Kabaka Mwanga wa Pili, walikuwa ni 45 na kati yao Wakatoliki walikuwa ni 22, waliouwawa kati ya mwaka 1885 na mwaka 1887 kwa kuchomwa moto wakiwa hai! Leo Mama Kanisa anapowakumbuka kwa namna yapekee, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya ushuhuda wa uekumene wa damu unaowaunganisha Wakristo wote kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa watu wote, na zaidi katika nchi ya Uganda, Bara la Afrika na kwa ulimwengu mzima.
Vatican ikihojiana na mmisionari wa Mapadre wa Afrika
Vatican News ikizungumza na Padre Richard Niombi, mmisionari wa mapadre na Afrika anayetoa huduma yake katika parokia ya Mapeera-Nabulagala huko Kampala, mji mkuu wa Uganda amethibitisha jinsi ambavyo mwaka huu wamefika mahujaji wengi kutoka ndani ya Uganda na kutoka nchi nyingine, Kwake yeye, utajiri huu unafafanuliwa hasa na kiu ya kiroho na ujuzi na ufahamu walio nao Wakristo sasa kuhusu wafiadini hao. Baada ya miaka miwili ya ugonjwa UVIKO-19, Wakristo wanakwenda Namugongo kuombea mema ya ulimwengu na kushuhudia matumaini yao. Baadhi wameandaliwa kiroho majimboni mwao kwa kutafakari hasa mada inayoadhimisha hija ya mwaka huu 2022: “kubatizwa na kutumwa kumshuhudia Kristo kwa matumaini”.
Sherehe ya kiekumene, licha ya ugumu unaohusishwa na janga la uviko
Sifa mojawapo ya hija ya Namugongo ni kipengele chake cha kiekumene, kwani Wakristo wa madhehebu mbalimbali wanakwenda huko, wakiwemo Wakatoliki na Waanglikani. Kila mwaka kunakuwa na kumbukumbu ya pamoja au mafungo yanayoandaliwa na maaskofu wa Kikatoliki na Kianglikani na maaskofu hukutana kwa mkutano wa pamoja. Pia kuna maombi ya kawaida katika makanisa ya Kianglikani na Katoliki. Lakini mwaka huu 2022, vizuizi vya kiafya vilivyohusishwa na janga la UVIKO-19 vilikuwa kikwazo kikubwa kwa shirika la kushughulikia hatua hizo. Hata hivyo, Wakristo Wakatoliki, Anglikani na Waprotestanti waliweza kufanya hija pamoja ili kujikabidhi kwa maombezi ya mashahidi, amethibitisha Padre Niombi.