Tafuta

Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu.   (Vatican Media)

Kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio Jimbo Kuu la Dar es Salaam linatabarukiwa Jumamosi tarehe 2 Julai 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, OfmCap. wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, nchini Tanzania. Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Waamini washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Na Damian Kongwa, -Dar Es Salaam na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S., -Vatican.

Kutabarukiwa kwa Kanisa maana yake ni kutenga Kanisa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, kwa ajili ya sifa, utukufu na ukuu wa Mungu. Na ni katika mantiki hii, Kanisa linaitwa Nyumba ya Mungu, Makao ya watu wa Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu wanakutanika kusali, kuabudu, kumtukuza, kumwomba na kumshukuru Mungu kwa wema, huruma na ukarimu wake wa daima. Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anasubiri kukutana na waje wake, lakini inasikitisha kuona kwamba, kuna Kanisa lililojengwa vizuri na la kupendeza, lakini hakuna waamini wanaokwenda kusali ndani mwake. Hivyo basi, Liturujia inayoadhimishwa kila siku, iwajenge waamini waliomo katika Kanisa ili wawe ni Hekalu Takatifu la Bwana, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia yawaimarishe waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Rej. SC, 2. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda Kanisa ili kuchuma, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, uwepo wa waamini Kanisani humo, itakuwa ni baraka na neema tosha kabisa. Ujenzi wa jengo kama Kanisa unakamilika kwa haraka, lakini inachukua muda mrefu kujenga na kuimarisha Jumuiya ya waamini, wenye tabia, ari na mielekeo tofauti. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini inayoimarishwa kwa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Parokia ya Ununio iko chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yohane Paulo II
Parokia ya Ununio iko chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yohane Paulo II

Baba Mtakatifu Francisko anakazia: Liturujia ya Neno la Mungu: Kukutana, Kusikiliza na Kung’amua kwa pamoja. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujizatiti kikamilifu ili waweze kuwa ni wajenzi wa sanaa ya watu kukutana. Huu ni muda muafaka wa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu katika: Sala, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa kwa nyakati hizi. Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume. Ni makutano yanayohitaji ukweli na uwazi, ujasiri na uwepo ili kukutana na wengine. Huu ni mwelekeo mpya unaowataka waamini kutoka katika ubinafsi na mazoea yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye yuko na anatembea pamoja nao katika ukweli na uwazi! Ni wakati wa kusiliza Neno la Mungu na waamini kusikilizana wao kwa wao! Ni muda wa kumsikiliza Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunulia njia na lugha mpya, ili kuzama katika ukweli wa mambo. Roho Mtakatifu anawataka waamini kusikiliza maswali ya watu waliokata tamaa, matumaini ya watu na Makanisa mahalia! Mkazo ni sanaa ya kusikiliza kwa makini. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho, ili kweli maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa yaweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani.

Waamini watambue na kukumbuka kwamba, Kristo Yesu ndiye Jiwe kuu la pembeni na kila mwamini anapaswa kujengeka na kuwa ni jiwe hai, ili waamini wote waweze kutembea kwa pamoja katika umoja, ushirika na utume, kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Bila uwepo wa Kristo Yesu kati yao, Kanisa kama Jengo litageuka na kuwa ni uwanja wa fujo, “patashika nguo kuchanika” aliwahi kusema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, ambaye anawataka waamini kuwa mawe hai katika Kanisa kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha, kwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza pamoja nao kutoka katika undani wa nyoyo zao, yaani dhamiri nyofu. Waamini wamwachie nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika kufikiri na kutenda! Waamini wenyewe wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwa kuwa ni sadaka safi inayompendeza Mungu pamoja na jirani zao. Kanisa, Nyumba ya Mungu na Hekalu la Roho Mtakatifu ni mahali ambapo Kristo Yesu anaendelea kujitoa sadaka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Na waamini wanaompokea Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai wanapaswa na wao kugeuka na kuwa ni “Ekaristi” Mkate uliomegwa na kutolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Kristo katika sala, Neno na Ekaristi
Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Kristo katika sala, Neno na Ekaristi

Waamini wajenge utamaduni wa kusali na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho kwani hizi ni Sakramenti Pacha. Waamini waache ubinafsi na tabia ya kujitafuta wenyewe na badala yake, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Wajitahidi kuufia ubinafsi wao! Ni katika muktadha huu: “Kwa kadri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi wenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo” (1 Kor 3:10-11). Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio Jimbo Kuu la Dar es Salaam linatabarukiwa Jumamosi tarehe 2 Julai 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, OfmCap. wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, nchini Tanzania. Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Mababa wa Kanisa wanasema, Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu.

Altare ni sura ya mwili wa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha umuhimu wa kuzunguka Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Altare hai ni Kristo Yesu mwenyewe, hivyo, wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare. Ndiyo maana kila mmoja anapaswa kuwa sadaka, kwa Mungu na kwa jirani yake. Aidha, chochote kinachotabarukiwa kinapaswa kutumika kwa ajili ya Mungu tu, kama vile kila mbatizwa anavyopaswa kuwa ni kwa ajili ya Mungu, kinyume chake ni kujiteketeza. Altare ina maana sana katika maisha ya mwamini. Altare ni kielelezo makini cha Kristo katika hali yake yote. Ni Kristo Yesu: anayeganga na kuponya, anayesamehe na kutakasa; Kristo anayefundisha, kuonya na kuongoza.

Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Yesu katika: Sala, Neno na Ekaristi
Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Yesu katika: Sala, Neno na Ekaristi

Ikumbukwe kuwa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Ununio ilianza kama Jumuiya ya waamini wachache mnamo mwaka 1996 ikiwa chini ya usimamizi wa Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wanaohudumia Parokia ya Damu Azizi ya Yesu Tegeta. Kutokana na ongezeko la idadi ya waamini mnamo mwaka 2005 Jumuiya ilipata hadhi ya kuwa Kigango na baadae mwaka 2014 kupandishwa hadhi na kuwa parokia kamili. Mzee David Komba mmoja kati ya waanzilishi wa Parokia ya Ununio amesema hapo mwanzo eneo la Ununio lilikuwa na waamini wakatoliki wachache sana ambao walikuwa wanalazimika kwenda kusali Parokiani Tegeta au Boko kwa sababu hizo ndiyo zilikuwa Parokia pekee zilizokuwepa kipindi hicho na hivyo anashukuru sana uongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa kukubali na utayari wao wa kuanzisha huduma za sala na hatimaye Parokia jambo ambalo liliwaondolea changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma ya maisha ya kiroho. Shukrani za pekee kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa kupanda mbegu ya ukatoliki Ununio mwaka 1996 mpaka mwaka 2015 walipokabidhi rasmi Parokia ya Ununio kwa Mapadri wa Shirika la Mtakatifu Vincent ambao ndio wanaendelea kutoa huduma katika Parokia hii.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wamechangia sana katika uinjilishaji nchini Tanzania
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wamechangia sana katika uinjilishaji nchini Tanzania

Tangu kuanzishwa kwake Parokia ya Ununio imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya waamini kutoka waamini 30 hapo awali hadi sasa ambapo Parokia inajivunia kuwa na waamini wanaokadiriwa kufikia idadi ya watu 1,453. Idadi ya Jumuiya nayo imeongezeka sana kutoka Jumuiya tatu mpaka ishirini na nne zilizopo kwa sasa. Sanjari na kuongezeka kwa waamini, huduma za maisha ya kiroho; sala na ibada mbalimbali zimeboreshwa kutokana na ushiriki mzuri wa waamini pamoja na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya Parokia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II – Ununio Padri Emmanuel Haule, CM katika kujiandaa na tukio la kutabaruku Kanisa amewashukuru sana waamini wote wa Parokia ya Ununio na watu wote wenye mapenzi mema waliochangia kwa hali na mali kufanikisha ujenzi wa kanisa huku akiwakaribisha kushiriki katika misa takatifu ya Kutabaruku Kanisa itakayofanyika Jumamosi ya tarehe 2 Julai 2022.

Kutabaruku Kanisa
30 June 2022, 16:12