Tafuta

2022.05.31 Kardinali Mteule Peter Okpaleke of Ekwulobia, Nigeria 2022.05.31 Kardinali Mteule Peter Okpaleke of Ekwulobia, Nigeria 

Kard.Mteule Okpaleke:Mungu wetu ni wa majaliwa!

Askofu Peter Okpaleke wa Ekwulobia,Nigeria,ni miongoni mwa makadinali 21 wapya ambapo Papa Francisko aliwatangaza tarehe 29 Mei.Kardinali mteule amezungumzia jinsi alivyopokea taarifa ya kuteuliwa kwake na jinsi uzoefu wake wa kichungaji unavyochangia kumtia moyo katika jukumu lake jipya.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Akiwashangaza wote siku ya Dominika 29 Mei 2022 kwenye hitimisho la Sala ya Malkia wa Mbingu, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Papa Francisko alitangaza kwamba ataunda Makardinali wapya 21 kwenye Mkutano wa tarehe 27 Agosti. Miongoni mwa Makadinali hao wapya walioteuliwa ni Askofu Peter Eberechukwu Okpaleke wa Ekwulobia, katika eneo la Mashariki mwa Nigeria. Askofu Okpaleke anajiunga na Baraza la Makadinali ambalo kwa sasa lina makardinali 208, kati yao 117 ni wapiga kura. Pamoja na kuongezwa kwa Makardinali hao wapya 21 walioteuliwa mwezi Agosti, Baraza la Makardinali litakua na kufikia Makardinali 229, kati yao, 131 watakuwa wapiga kura. Kardinali mtarajiwa alizungumza na Vatican News kuhusu jinsi alivyopokea habari hizo, maeneo anayozingatia katika jukumu lake jipya na jinsi mang’amuzi na majukumu yake ya zamani yalivyomjenga katika huduma yake ya kichungaji.

Wakati wa tangazo la Papa Francisko, Askofu Okpaleke alikuwa katika huduma yake ya kiaskofu katika Jimbo la Ekwulobia. Alikuwa katika parokia moja, akitoa sakramenti ya kipaimara kwa watu 138, bila kuondolea na hisia kali zaidi na kilichotokea. Baada ya Misa, alipokelewa na katibu wake akiwa amebeba taarifa za uteuzi wake mpya. Kufuatia hayo, habari ziliendelea kuenea kutoka pande moja na nyingine tofauti. Ameeleza kwamba itikio lake la kwanza lilikuwa ni kufikiria kutostahili kwake mwenyewe na mapungufu yake, lakini kwa neema ya Mungu, ikiwa imempendeza Roho Mtakatifu anayefanya kazi katika Kanisa na kwamba anafarijiwa na maneno ya Maandiko kutoka Warumi 8:28 kwamba: “Twajua ya kuwa mambo yote hufanya kazi pamoja na wale wampendao Mungu katika kuwapatia mema". Kwa nafasi hii mpya, Askofu Okpaleke anakuwa Kardinali wa nne kutoka Nigeria, taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambalo linakabiliwa na changamoto zake katika ngazi tofauti.

Kanisa nchini limekuwa likipiga kelele katika masuala kadhaa na limekuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki za kijamii. Akitafakari juu ya Kanisa la Nigeria, Askofu amebainisha kwamba changamoto yake kuu ni “kuishi kwa uaminifu kwa wajibu wake mkuu wa kushuhudia maisha ya Yesu Kristo na ukweli na upendo wake unaobadilisha.” Haya yote, katika muktadha wa matatizo ya kiuchumi, ubinafsishaji wa rasilimali za nchi na watu wachache kwa gharama ya walio wengi, ukosefu wa usalama wa maisha na mali, na kudhoofisha taasisi za serikali, miongoni mwa mambo mengine. Kutokana na hali hiyo, Kardinali mteule anasisitiza haja ya wachungaji kuwa “washiriki wa utamaduni” ili kuruhusu “Injili ya Yesu Kristo kupenya tamaduni hizo, na kubadilisha, na kujenga mazungumzo kati ya Injili na utamaduni. Mbali na maeneo mengine ya mwitikio wa kichungaji, Askofu huyo kwa upande wake, anasema atazingatia kwa namna ya pekee uinjilishaji katika maeneo ya Wakristo, malezi shirikishi ya binadamu kwa ajili ya mageuzi ya kijamii katika nguvu ya Injili, na majadiliano ya kidini nchini ambayo ni kugawanyika pamoja na mgawanyiko wa kidini wa Kikristo na Kiislamu.

Huduma ya kichungaji ya Askofu Okpaleke haikukosa changamoto zake yenyewe. Mnamo 2012, aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Ahiara, katika Serikali ya Imo lakini hakuweza kuchukua umiliki wa Jimbo hilo kwa kukataliwa. Miaka iliyofuata ilikuwa migumu na mnamo 2018, Baba Mtakatifu alikubali kujiuzulu kwake kama askofu wa Ahiara. Baadaye, Jimbo la Ekwulobia iliundwa tarehe 5 Machi 2020 na Askofu Okpaleke aliteuliwa kuwa Askofu wake wa kwanza. Akirejea kuhusiana na uzoefu huo, Kardinali mteule anabainisha kwamba, pamoja na nyakati ngumu na uadui anaouona kuwa si wa mtu binafsi, Mungu alimjalia amani ambayo hajawahi kuipata. “Yesu anazungumza kuhusu aina hii ya amani kwa Mwinjili Yohana 14:27,” yeye amesema, Sasa anajua Yesu alimaanisha nini, kwamba yeye anapatiwa amani, si aina ya amani ambayo ulimwengu hutoa.

Katika kipindi hicho bila malipo ya kuwasimamia watu wa Mungu, anaeleza kwamba alichukua muda wa “kutafakari, kuomba na kusoma” na kujishughulisha katika ngazi ya ndani zaidi. Licha ya uzoefu huu, Askofu Okpaleke anasisitiza: “Mungu wetu ni wa majaliwa” ambaye, licha ya kuonekana kuchanganyikiwa na kubahatisha, anaelekeza historia kwenye kusudi lake na kuwaalika wote “kujifungua na kuchangia nguvu, maarifa na talanta walizopewa na Mungu  kwa mpango wa kimungu  wa kufanya uso wa Dunia uakisi kwa uwazi zaidi Ufalme wa Mungu.” Kwa kuhitimisha alisema kwamba Kanisa pendwa la Ahira liko moyoni mwake na litaendelea kuwa hivyo kwa sababu hata sasa kama alivyo sema Kardinali mteule kwamba “Nilipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa waamini wa Jimbo la  Ekwulobia na wengi kutoka Jimbo la Ahiara.

03 Juni 2022, 10:39