Tafuta

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu Siku ile ya Alhamisi Kuu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu Siku ile ya Alhamisi Kuu. 

Ekaristi Takatifu Sakramenti: Upendo, Umoja na Karamu ya Pasaka

Ni Sakramenti ya upendo, umoja, Karamu ya Pasaka ambamo Yesu, huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni Sakramenti ya sadaka, shukrani, kumbukumbu na uwepo kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu. Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, Roma.

Kristo Yesu, Usiku ule alipotelewa, aliweka Sadaka ya Ekaristi Takatifu ya Mwili na Damu yake Azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya Msalaba siku zoter mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake. Hii ndiyo Sakramenti ya upendo, umoja, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo Yesu, huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni Sakramenti ya sadaka, shukrani, kumbukumbu na uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu. Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao. Rej. KKK 1322 – 1419. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni karamu ya Bwana, kusanyiko la Kiekaristi, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa, Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka. Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote!

Kwa mara nyingine mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican news nakukaribisha katika Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo. Ni sherehe inayoadhimishwa baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Lakini pia ni sherehe ambayo inaadhimishwa siku ya Alhamisi Kuu ndani ya siku tatu kuu za Pasaka. Siku hiyo hatuadhimishi kwa shangwe sababu tunaanza kutafakari mateso na kifo cha Kristo. Hivyo Kanisa likaweka nafasi nyingine ili kuadhimisha kwa shangwe zaidi. Ndiyo alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu au Jumapili inayofuata kuwezesha ushiriki wa waamini. Ni sherehe ambayo tunaandamana na Yesu katika mitaa mbalimbali. Sherehe ya Ekaristi. Kwa hiyo tunatafakari Ekaristi ni nini? "Ekaristi" ni neno la Kiyunani, ambalo linamaanisha, "kushukuru". Katika desturi ya Kiyahudi, kila mlo ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa mambo yake mema. Katika kila Misa, tunatenda kama makuhani wa uumbaji, tukitoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya uhai, na kwa ajili ya mambo mengi anayotujalia. Hata hivyo maneno yaliyotumika na Wakristo wa kwanza katika Matendo ya Mitume kuhusu Ekaristi ni "kuumega mkate", Karamu ya Bwana, na Kusanyiko la Kiekaristi.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Halafu  Neno “Mwili wa Kristo” linaweza kumaanisha mambo matatu: mwili wa kimwili , mwili wa fumbo, na mwili wa sakramenti. Kwa maana zifuatazo: Mwili wa kimwili wa Yesu tayari umetukuzwa na umeketi mkono wa kuume wa Baba. Lakini anaweza kuwepo kimwili popote na popote anapotaka kwa sababu tayari ni mwili uliotukuka. Hakuna lisilowezekana kwa Yesu. Mwili wa fumbo wa Yesu ni Kanisa, jumuiya ya waamini. Yeye ndiye kichwa cha Mwili huu. Yupo pamoja nasi katika Kanisa:  ndiyo maana alisema “Walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo katikati yao.” Mwili wa Sakramenti ya Yesu ni Ekaristi, Sakramenti ya Mwili na Damu yake.  Ekaristi ni uwepo halisi wa Yesu katika maumbo ya Mkate na divai.

Somo la kwanza Mwa 22:1-18 linatuambia kwa ufupi kwamba: “Abramu akamtolea Melkizedeki sehemu ya kumi ya vitu vyote.” Hakuitoa kwa nia ya kupokea kitu kama malipo. Badala yake, alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe., Melkizedeki alimbariki, na kutoa shukrani kwa Mungu kwa niaba yake kwa mkate na divai. Haya yalikuwa matoleo ya mtu binafsi kwa namna ya vitu vya kimwili. Kwa hakika, Abramu ni mtaalamu wa kujitolea. Somo la pili Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26). Ni maelezo ya Paulo kuhusu tukio la Karamu ya Mwisho ya Yesu na wanafunzi wake. Lakini pia umuhimu wa Ekaristi kama ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo unaletwa tena nyumbani kwa Wakorintho. Injili inahusu muujiza wa kuzidisha mikate Lk.9:11-17. Yesu aliwalisha wanaume zaidi ya 5000 bila kuhesabu wanawake na watoto kwa mikate mitano na samaki wawili. Wakala na kushiba.  Muujiza huu, hasa katika Injili ya Yohana sura ya 6  ulitumika kama utangulizi wa Hotuba ndefu ya Yesu juu ya Ekaristi. Katika Injili ya Luka na Injili nyingine pacha, kipindi hiki kilisimuliwa katika muktadha wa mafunzo ya wanafunzi. Hata hivyo, kuna dokezo la Ekaristi.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Katekismu ya Kanisa Katoliki inaeleza kwa upana juu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hapa ni baadhi ya nukuu zinataja kuwa: hapo awali, Kristo alijitoa kisakramenti kwetu. Hii ni njia rahisi ya kuonyesha upendo wake usio na masharti kwetu. Anatuamuru hivi: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu!” Kwa hiyo kanisa linatufundisha: “Amri ya Yesu ya kurudia matendo na maneno yake hadi atakapokuja (KKK 1341), halafu pia inasema "Ekaristi ni 'chanzo na kilele cha maisha ya Kikristo.' KKK.1106. Pia KKK 1378. Inataja kuwa "Ibada ya Ekaristi. Katika liturujia ya Misa tunadhihirisha imani yetu katika uwepo halisi wa Kristo chini ya maumbo ya mkate na divai tukisujudi kwa kina kama ishara ya kumwabudu Bwana. Hata hivyo "Kanisa Katoliki daima limetoa na bado linatoa nafasi ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, sio tu wakati wa Misa, hata nje ya Misa ndiyo maana sehemu nyingi kila alhamisi au jumapili kuna kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Misa na kuna maabudu ya daima. Pia sherehe hii kuna kufanya maandamano na Ekaristi kwa heshima na ibada katika maeneo mbalimbali. 

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anatukumbusha kwamba katika kuadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Kristo, Kanisa “haliadhimishi Ekaristi pekee, bali huibeba kwa taadhima, likitangaza hadharani kwamba dhabihu ya Kristo ni kwa wokovu wa ulimwengu wote.” Hivyo ni sahihi kuandamana na Yesu katika Ekaristi Takatifu. Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo (Corpus Christi), ambayo Kanisa linaadhimisha leo inatukumbusha sote zawadi ya ajabu ya Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo katika Sakramenti Takatifu. Ingawa lengo kuu la sherehe hii ni juu ya lishe ya kiroho ambayo Kristo anatupa, lengo lake la pili ni kwa Mwili wa Kristo ambao ni Kanisa. Mwili na Damu ya Kristo (Ekaristi), ni zawadi bora sana ambayo tumepewa na Kristo.

Sherehe ya Ekaristi iliigwa baada ya Mlo wa Pasaka ya Wayahudi. Tunakumbuka kwamba Yesu alikuwa Myahudi na alifanya karamu ya mwisho katika pasaka ya wayahudi. Karamu ya Mwisho iliyofanywa na mitume wake ambapo alianzisha Sakramenti ya Ekaristi ilikuwa Mlo wa Pasaka. Hii ndiyo sababu tarehe ya kusherehekea Wiki Takatifu inatofautiana kila mwaka kwani inabidi ifanane na sherehe ya Kiyahudi ya Pasaka wakati Yesu alipoadhimisha Karamu ya Mwisho. Sherehe ya Pasaka ya Kiyahudi imepangwa kwa mwezi kamili (Nisan). Kwa maneno mengine sherehe ya Pasaka kila mwaka inategemea Alhamis Kuu inaangukia lini kadri ya kalenda ya wayahudi. Mambo husika katika Mlo wa Pasaka ya wayahudi: ni mwana-kondoo, mkate usiotiwa chachu, divai kutoka mzabibu na mboga chungu. Mwana-kondoo ndiye mnyama wa dhabihu kama inavyoonyeshwa katika Sheria ya Musa. Mkate usiotiwa chachu ni ukumbusho wa kukimbia kwa Watu Waliochaguliwa kutoka Misri. Mkate hauna chachu kwa sababu walipaswa kufanya haraka na hakuna wakati tena wa kufanya unga uumuke. Mvinyo ilikuwa ni jadi, ishara ya furaha na sherehe. Mimea ya uchungu inawakumbusha watu juu ya mateso na mapambano yao wakati wa utumwa wao huko Misri.

Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya waja wake.
Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya waja wake.

Katika Karamu ya Mwisho, Yesu na mitume walikuwa na mkate usiotiwa chachu na divai ya zabibu tu. Hakuna haja tena ya mwana-kondoo wa dhabihu, kwa kuwa Yesu mwenyewe ni Mwana-Kondoo wa Mungu: Yeye ndiye mhusika anayetolewa kama dhabihu, na wakati huo huo, Kuhani Mkuu akitoa dhabihu. Ndiyo maana Mt. Augustino anasema: “Kristo alikuwa amebebwa kwa mikono yake mwenyewe alipoutoa mwili wake, akisema, ‘Huu ni mwili wangu’; maana alikuwa ameushika mwili huo mikononi mwake alipokuwa akisema maneno hayo. Kwa hiyo basi, Mtakatifu Augustino anasisitiza faida sahihi ya Ekaristi, ambayo ni umoja wa Mwili wa Fumbo. Upendo unaoliunganisha Kanisa ni matokeo sahihi ya kupokea Mwili na Damu ya Kristo. Ekaristi inaweza kujenga Mwili wa Kristo katika mapendo (baadaye itaitwa res tantum) kwa sababu yenyewe ndiyo Mwili wa Kristo uliopo kisakramenti (res et sacramentum).

Pia Augustino anasema mkate na divai inayoonekana kwenye madhabahu, "iliyogeuzwa kwa neno la Mungu," ni Mwili na Damu yake. Kwa kuupokea kwa uchaji Mwili huo na Damu ile iliyomwagika kwa ajili yetu, tunakuwa Mwili huo, ambao ina maana kwamba tunaunganishwa katika muungano wa karibu wa Mwili wa Fumbo. Msisitizo mwingine wa Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa ni kuabudu Ekaristi kabla ya kupokea Komunyo Takatifu ni kukiri wazi uwepo wa kutosha wa Mwili na Damu ya Kristo katika Ekaristi. Hivyo Augustino anasema wakati ule wa Mageuzo ni wakati unaostahili kumwabudu Kristo kimya kimya. Ekaristi inastahili kuabudiwa tu kwa sababu ina uwepo mkubwa wa ubinadamu wa Neno, yaani Kristo, Umwilisho. Pia anasistiza kumpokea Yesu kwa ibada na heshima.

Ni karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao.
Ni karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao.

Pamoja na hayo wakati wa Karamu ya Mwisho, Yesu pia aliweka Sakramenti ya Ukuhani wa Kihuduma yaani daraja takatifu. Daraja lenye ngazi tatu ambazo ni Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Hawa huwekwa wakfu kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu ambao wana Ukuhani wa Pamoja wanaopokea katika Ubatizo. Hili linadhihirika sana katika maadhimisho ya  Ekaristi. Sababu ya Yesu kuanzisha Sakramenti ya Daraja Takatifu wakati wa Karamu ya Mwisho ambapo Sakramenti ya Ekaristi ilianzishwa ilikuwa ni kuhakikisha kuna wahudumu ambao wataendelea kuadhimisha Ekaristi baada ya yeye kuondoka: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.  Hivyo Daraja Takatifu linamuunganiko muhimu sana na Sakramentii ya Ekaristi Takatifu.  Hivyo basi  tuwaombee makasisi wetu ili waweze kuadhimisha maadhimisho kwa heshima na ibada. Pia waepushwe na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kipindii hiki. Mama kanisa anatuhimiza tuwasaidie na kuwaombea mashemasi, mapadre na maaskofu wetu. Ni walengwa wa adui na wengi wao huanguka katika mtego wa shetani wa kiburi, uchu wa mali, starehe, tamaa na mambo mengine. Wanahitaji maombi yetu, usaidizi, kuwategemeza au kuwawezesha lakini marekebisho ya kindugu pale tunapoona hawaendi vizuri.

Corpus Christi
22 June 2022, 08:04