Tafuta

Katika Sadaka ya Misa Takatifu tunapaswa kutoa mioyo yetu pamoja na vitu tulivyonayo yaani sehemu ya mali yetu kama ishara ya nje ya sadaka yetu ya moyo. Katika Sadaka ya Misa Takatifu tunapaswa kutoa mioyo yetu pamoja na vitu tulivyonayo yaani sehemu ya mali yetu kama ishara ya nje ya sadaka yetu ya moyo.  

Dominika ya XIII Mwaka C:Wito wa kumfuasa Kristo ni sadaka

Katika maisha yetu ya kumfuasa Kristo daima tusikilize maneno ya Paulo akisema:“Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu,itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai,takatifu na ya kumpendeza Mungu,ndiyo ibada yenu yenye maana.” Dhabihu hii iliyo hai katika miili yetu ni kujitoa kwa kila namna na kuruhusu miili yetu itumike mbele za Mungu kwa ajili ya utukufu wake.Kuitoa miili kuwa dhabihu ni kuruhusu miili yetu kutii na kufuata makusudi ya Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Itakumbukwa kuwa tulipoanza kipindi cha Kwaresima Jumatano ya majivu tuliishia dominika ya 8. Kumbe masomo ya dominika nne yaani ya 9, 10, 11 na 12 hatuja yatafakari. Hii ni kwasababu mwaka huu una dominika chache. Dominika ya 9 tuliiruka na kuiacha kabisa ili kutoa nafasi kwa dominika nne za kipindi kijacho cha majilio ili Krismasi iangukie 25 Desemba. Dominika ya 10 tuliadhimisha Pentekoste na kuhitimisha kipindi cha Pasaka. Dominika ya 11 tuliadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu na ya 12 tukaadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo - Ekaristi Takatifu. Masomo ya Dominika hii ya 13 Mwaka C yanatukumbusha kuwa kumfuasa Kristo ni kujitoa sadaka. Na sadaka iliyo safi sio ya shuruti bali ni ya kujitoa kwa uhuru kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kama anavyotuambia Mtume Paulo katika waraka kwa Warumi akisema; “Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Rm 12:1).

Mungu amemwandalia kila mmoja wetu namna ya maisha ambayo kwayo tunapaswa kumtumikia. Mpango huu wa Mungu ni kwa kila mwanadamu na unaanza hata kabla ya kuzaliwa ndivyo alivyomwambia Yeremia; “Kabla hujaumbwa, nalikujua, kabla hujazaliwa, nalikutakasa uwe nabii kwa mataifa” (Yer.1:5). Ni katika kumtumikia Mungu kwa uaminifu tunaitwa kuwa watakatifu kushiriki furaha ya milele mbinguni. Wito huu sio wa shuruti. Kila mmoja yuko huru kuitika na kukubali kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa kila binadamu amejaliwa mwili, roho, akili, utashi na uhuru kamili ili awajibike kwa matendo yake mwenyewe. Ni kwa njia ya mwili tunamtumikia Mungu kwa kuwahudumia wenzetu na kuutiisha ulimwengu. Roho ndiyo itiayo uzima katika mwili na ni kwa njia ya roho tunaweza kuwasiliana na Mungu Baba yetu aliyetuumba. Ni kwa njia ya akili tunaweza kunga’amua, kufahamu, kutambua na kujua kati ya lililo jema na baya na kwa utashi tunachagua kutenda kwa uhuru kile tunachokijua.

Uhuru unaweza kutumika vizuri au vibaya. Adamu na Hawa walikuwa na uhuru wa kuchagua kula tunda au kutolila kama Mungu alivyokuwa amewaamuru. Wao wakachagua kula tunda. Walichagua kwa uhuru wao wenyewe kwani maandiko matakatifu yanatuambia “Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia kwa macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe naye pia akala” (Mwa.3:6). Kumbe, hawakulazimishwa bali walichagua walichokipenda wao. Kwa kufanya hivyo walitumia vibaya uhuru wao kwani kuchagua kwa uhuru si kuchagua unachokipenda. Kuchagua vizuri na kwa uhuru ni kuchagua mapenzi ya Mungu bila kulazimishwa au kushurutishwa. Ni kuyatambua, kuyapenda, na kuyatimiza mapenzi ya Mungu Baba kwa moyo wa upendo.

Elisha katika somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha wafalme (1Waf 19.16,19-21), ni mfano hai wa kuitika wito wa kumtumika Mungu bila shuruti. Elisha alipoitwa na Mungu kupitia Elia, aliacha yote na kuanza safari ya utumishi kwa ajili ya wokovu wa watu wake wakati ambapo Ahabu na Yezebeli waliwatesa waisraeli wakiwashurutisha wamkane Mungu wao wa kweli na wamwabudu Baali. Tunaambiwa, Eliya alipopita karibu na Elisha, akatupa vazi lake juu yake, Elisha akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata na kukutumikia. Elia akamwambia, enenda, urudi, naye akaenda akamrudia. Ndiyo ya Elisha inakuwa ndiyo kweli, akainuka, akamfuata Eliya akamhudumia na Mungu akapendezwa naye.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka kwa Wagalatia (Gal 4:31b-5:1, 13-18) anasema; “Ninyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za dunia. Uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako” (Gal 5:13-14). Huku ndiko kuenenda kwa roho na kuvithibiti vilema vya mwili, ikiwa ni pamoja na tamaa zake. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zinapingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka (Gal 5:16-17). Lakini dereva wa maisha yako akiwa Roho wa Mungu, utaruhusu ndani yako moyo usio na ubaguzi na kujitoa kwa upendo bila kujibakiza. Na huu ndio ukweli kwamba, tukiongozwa na Roho hatupo tena chini ya sheria (Gal 5:18). Huko ndiko kuitika wito wa kumpenda, kumjua na kumtumikia Mungu kwa uhuru, ni kumfuasa Kristo na ndiyo sadaka iliyo hai na ya kupendeza.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 9. 51-62), inaeleza kuwa maisha ya kikristo ni ya sadaka. Ni kujitoa bila kujibakiza na bila kigeugeu kwani lengo la Kristo kujimwilisha na kukaa nasi sio ushindi wa kidunia bali kujitoa sadaka yeye mwenyewe kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Yesu akielekea Yerusalemu kutimiza fumbo la ukombozi, njiani anakutana na watu wanaomwomba kuwa wafuasi wake. Lakini Yesu hatoi jibu la ndio au hapana. Anachokifanya anawaambia nini maana ya kumfuata yeye na nini cha kufanya. Kwa mtu wa kwanza anambwambia, bweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Maana yake kipaumbele cha kumfuata Kristo sio maisha ya raha bali ni kujikatalia malimwengu kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Ni kujitoa sadaka iliyo hai na ya kumpendeza Mungu. Kwa mwingine anamwambia waache wafu wawazike wafu wao. Ni jibu gumu na la kukatisha tamaa, lakini linatufundisha kuwa kifo ni kweli isiyopingika na hivyo shughuli zake na mazingira yake, isiwe sababu ya kuiacha na kuikana imani yetu, tuwe tayari kuacha yote kwa ajili ya ushuhudi wa imani yetu. Kwa wa mwisho anamwambia, mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu. Tunafundishwa kuwa na msimamo thabiti katika imani na kutokuwa ndumilakuwili au kigeugeu katika maisha ya imani. Tunalopaswa kufanya ni kujenga uaminifu na utayari wa kutimiza kile tulichoitiwa na kukubali bila shuruti kwa sifa na utukufu wake Mungu.

Kwa Ubatizo wetu tuliitwa kuacha yote na kumfuata Kristo. Ubatizo si lelemama bali ni wajibu msingi na wa kwanza katika maisha yetu ya kuujenga muunganiko na Mungu wetu mtakatifu sana. Ni kukubali kujitoa sadaka sisi wenyewe. Sakada ni nini? Ni kile kinachotolewa na kuteketezwa kwa heshima ya Mungu, ili laana zifungwe, neema na baraka zifunguliwe. Sadaka kubwa na halisi ni ya Kristo msalabani (1Kor 5:7). Misa Takatifu ndilo tambiko kubwa na la pekee kwa maisha ya Kikristo. Ndiyo maana Padri Kabla ya kuanza mageuzo (kabla ya kutolea tambiko hili kwa ajili ya dhambi zetu na zake mwenyewe) anatualika sote akisema: “salini ndugu ili sadaka yangu na yenu ikubaliwe na Mungu Baba mwenyezi.”

Hivyo ili tuzipate baraka na neema zitokanazo na sadaka hii, tambiko hili takatifu, ni lazima katika azimisho la misa kwanza tuwe makini katika sala, pili lazima tuwe na moyo wa ibada kwa Mungu, tukijitoa kabisa mwili na roho, kujitoa nafsi zetu pamoja na Kristo kwa Mungu kama anavyotuambia mzaburi, “sadaka yangu Ee Mungu ni moyo mnyoofu na uliopondeka” (Zab 51:17). Moyo mnyoofu na uliopondeka ndicho anachoangalia Mungu. Katika Sadaka ya Misa Takatifu tunapaswa kutoa mioyo yetu pamoja na vitu tulivyonayo yaani sehemu ya mali yetu kama ishara ya nje ya sadaka yetu ya moyo. Pesa au sehemu ya mali tunayotoa inaitwa sadaka kwa sababu ni kile kinachotolewa kuwakilisha kilicho ndani ya moyo mnyoofu na uliopondeka. Sadaka hii haipimwi kwa wingi bali kwa unyoofu wa moyo. Ndiyo maana Yesu alimsifia Mjane aliyetoa vyote alivyokuwa navyo kwa moyo mnyoofu na nafsi yake, vyote analimtolea Mwenyezi Mungu na kumtegemea yeye peke yake (Mk 12:41-44).

Katika maisha yetu ya kumfuasa Kristo daima tusikilize maneno ya Paulo akisema; “Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Dhabihu hii iliyo hai katika miili yetu ni kujitoa kwa kila namna na kuruhusu miili yetu itumike mbele za Mungu kwa ajili ya utukufu wake. Kuitoa miili kuwa dhabihu ni kuruhusu miili yetu kutii na kufuata makusudi ya Mungu, na pia ni kukubali kuishi kwa ajili ya injili. Tunapojitoa katika kufanya kazi ya Mungu kwa moyo na upendo tunatoa dhabihu iliyo hai. Tunapofanya kazi za Kanisa kwa majitoleo bila shuruti, tunajitoa sadaka. Paulo anaongezea kusema sadaka hii itakuwa takatifu na ya kumpendeza Mungu, na ndiyo itakayotupa hadhi ya kuvikwa taji ya utukufu mbinguni.

Tafakari ya Dominika ya XIII mwaka C kipindi cha kawaida cha Mwaka

 

24 June 2022, 16:12