Tafuta

Askofu Wolfgang Pisa (OFM Cap) wa Jimbo Katoliki la Lindi ni shuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania Askofu Wolfgang Pisa (OFM Cap) wa Jimbo Katoliki la Lindi ni shuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania 

Askofu Wolfgang Pisa ni Shuhuda Wa Ukomavu wa Kanisa la Tanzania

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma anasema, Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. ni mgeni anayepaswa kujifunza na kuendelea kusoma alama za nyakati. Uteuzi, ukubali, uwepo na hatimaye, kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Lindi ni ushuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania katika mchakato wa kumwilisha upendo wa Mungu usio na mipaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Askofu ana wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Uwepo wa karibu wa Mungu ni chemchemi ya utume wa Askofu kama unavyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Ili kuonja ukaribu wa Mungu kuna umuhimu wa kupata mang’amuzi ya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Maaskofu wajenge utamaduni wa kusali na kutafakari mbele ya Kristo Yesu, ili kuwawezesha kuishi kati pamoja na watu wa Mungu. Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kiaskofu, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kukimbilia katika sala na tafakari makini ya Neno la Mungu ili kujenga tena: imani na matumaini mapya, kwa kumtegemea na kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Ukaribu wa Mungu unajionesha kati ya watu wake kwa njia ya utambulisho wa Maaskofu, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kama sadaka safi inayotolewa Altareni.

Askofu Wolfgang Pisa, anatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.
Askofu Wolfgang Pisa, anatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Maaskofu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya ulimwengu. Kristo Yesu anataka kuwa kati pamoja na watu wake kwa njia ya Maaskofu. Ukaribu wa Mungu unajionesha katika Neno na maadhimisho ya Mafumbo mbalimbali ya Kanisa. Lakini zaidi, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kupenda bila kujibakiza pamoja na kuendelea kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Ni katika muktadha huu, Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anapenda kutoa pongezi na shukrani kwa Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. Aliyewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Dominika tarehe 25 Juni 2022, kwenye viwanja vya Ilulu, Lindi. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, akisaidiana na Askofu mkuu Damiani Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea pamoja na Askofu mstaafu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi.

Kwa upande wake Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC amewataka watu wa Mungu nchini Tanzania kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti 2022. Ameitaka Serikali kuunga mkono juhudi za Kanisa katika kuwahudumia watanzania: kiroho na kimwili; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wake, Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, Serikali ya Tanzania itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa dini na madhehebu mbalimbali katika mchakato wa ujenzi wa mustakabali wa Tanzania. Inakazia: ushirikiano na ushirikishwaji wa wananchi wote. Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. wa Jimbo Katoliki la Lindi, amewashukuru watu wa Mungu kwa kushuhudia ushiriki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kufanya kazi kwa pamoja. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa imara katika Imani; kwa kukuza na kudumisha mila, desturi na tamaduni njema. Kamwe wasikubali kuzolewa na upepo wa utandawazi.

Askofu Msonganzila ametoa shukrani za dhati kabisa kwa Askofu mstaafu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, aliyezaliwa kunako tarehe 8 Agosti 1945 huko Magaura. Tarehe 8 Novemba 1974 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 6 Oktoba 1990 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi na kuwekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II, Sherehe ya Tokeo la Bwana tarehe 6 Januari 1991, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Na ilipogota tarehe 9 Aprili 2022 akang'atuka kutoka madarakani. Katika maisha na utume wake kama Askofu mahalia amefanya mengi na makubwa. Kanisa Katoliki limesimikwa katika urika wao unaowawezesha kurithishana mema na mazuri kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. ni mgeni anayepaswa kujifunza na kuendelea kusoma alama za nyakati. Uteuzi, ukubali, uwepo na hatimaye, kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Lindi ni ushuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania. Kanisa linatambua na kukiri kwamba, huduma kwa watu wa Mungu haina mipaka.

Maaskofu waoneshe ukaribu wa Mungu kwa waja wake.
Maaskofu waoneshe ukaribu wa Mungu kwa waja wake.

Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Lindi, kumkaribisha, kumpokea, ili waweze kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu usiokuwa na kifani kwa waja wake. Askofu Msonganzila anakaza kusema, hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Huu ni upendo endelevu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kumchagua Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. kuwa Mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki la Lindi. Watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Lindi waendelee kumuunga mkono na kushikamana naye kwa dhati kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa; daima ikiwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. amekabidhiwa dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ili kuendeleza ile kazi ya uumbaji na ukombozi kwa watu wa Mungu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Yote haya yanawezekana, ikiwa kama watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Lindi watajenga na kudumisha: upendo, ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Lengo liwe pia ni kuimarisha Injili ya familia. Watu wa Mungu wampokee Askofu wao kwa moyo mnyofu; wapokee mafundisho na maelekezo yake, anapotekeleza wajibu na dhamana yake ya Kiaskofu, ili kazi ya Mungu iweze kusonga mbele bila kuyumba. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila anawaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki Lindi “Mpeni moyo wenu ili awahudumie bila kuchoka; mpeni maisha yenu apate kuyaongoza ya kuyatakatifuza kwa: Sala, Neno na Sakramenti na Mafundisho ya Kanisa. Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. ndiye mteule wa Bwana ambaye ameitwa na kutumwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza wa Mungu kwa wakati huu. Amefika Lindi huku akiwa amembeba Kristo Yesu ili apate kuwainjilisha watu kwa kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni Injili anasema Askofu Msonganzila inayokita mizizi yake katika ushuhuda wa maisha; Majadiliano ya kitamaduni, kidini na kiekumene.

Askofu Wolfgang Pisa, ni shuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania
Askofu Wolfgang Pisa, ni shuhuda wa ukomavu wa Kanisa la Tanzania

Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. anahimizwa na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, huruma, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Lengo ni kushirikiana, kushikamana na kukamilishana kama watoto wa Mungu licha ya tofauti kubwa zinazoweza kuwepo kati yao. Wote hawa wanahitaji huduma ya kichungaji ya Askofu Wolfgan John Pisa O.F.M. Cap. Itakumbukwa kwamba, Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. wa Jimbo Katoliki la Lindi alizaliwa tarehe 6 Julai 1965 huko Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro aliweka nadhiri za daima tarehe 15 Agosti 1998 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Septemba 1999. Tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre amewahi kutekeleza shughuli zake za kichungaji na kitume kama Jalimu na Mlezi, Seminari Ndogo ya Maua, Jimbo Katoliki la Moshi kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2000.

Baadaye alitumwa na Shirika la Wakapuchini kujiendeleza zaidi katika masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hapo akajipatia Shahada ya Uzamili. Akateuliwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Maua kati ya mwaka 2005-2008. Baadaye alijiendeleza zaidi katika masomo ya maadili Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Marekani, Catholic University of Amerika huko Washington, DC kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011. Akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Kanda ya Tanzania na kuwaongoza tangu mwaka 2011 hadi mwaka 2017. Baadaye kati ya mwaka 20017-2019 akarejea tena darasani huko "Catholic University of America" huko Washington, DC na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Maadili. Amewahi kufanya shughuli zake za kichungaji Parokiani Kibaigwa, Jimbo kuu la Dodoma kati ya mwaka 2019-2020. Tangu wakati huo, hadi kuteuliwa kwake, Askofu Wolfgang John Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha. Na Tarehe 26 Juni 2022 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, tayari kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Lindi.

Jimbo Katoliki Lindi
28 June 2022, 16:16